NA FATMA HAMAD – PEMBA.
Wananchi wametakiwa kuendelea kuutunza Umoja na mshikamano uliopo sasa ili kuona Amani imetawala na nchi inapiga hatua katika nyanja mbali mbali za kimaendeleo.
Akizungumza na watendaji wa azaki za kiraia Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Masoud wakati akifungua kongamono la kumpongeza Rais mwinyi kwa kipindi cha mwaka mmoja alichokaa madarakani lililofanyika ukumbi wa baraza mji Chake chake Pemba.
Alisema suala la kutunza Umoja ni jukumu la kila mtu, hivyo ni vyema kila mmoja kwa nafasi yake kuendeleza umoja huo ili kuona hakuna vitendo vyovyote viovu vinavyojitokeza.
‘’Nawasihi wananchi tuutunzeni umoja wetu na mshikamano wetu ili tuweze kufanya kazi zetu kwa uhuru’’ alisema Mattar.
Alisema bila ya kuepo kwa amani si rahisi kupatikana kwa maendeleo, hivyo aliitaka Jamii kujiepusha kufanya vitendo viovu ambavyo vinaashiria uvunjifu wa amani.
Alisema Rais Mwinyi kwa kuwajali Wananchi wake ndio akamua kuunda umoja wa kitaifa ili kuwaunganisha Wazanzibar wote kuwa kitu kimoja bila ya ubaguzi wowote.
Aidha alifahamisha kuwa tokea kukaa kwake madarakani Rais Mwinyi kumeanzishwa miradi mbali mbali ya kimaendeleo nchini ambayo italeta manufaa kwa Wananchi pamoja na Taifa.
Mapema mratibu wa tumaini jipya [TUJIPE] Pemba Tatu Abdala Mselemu alisema katika utawala wa dk Mwinyi Asasi za kiraia zimepata mafanikio makubwa kwani zimeweza kutambulika zaidi katika mpango wa Sera, Sheria na mipango ya kimaendeleo.
Aidha alieleza kuwa kwa sasa asasi za kirai zimepata fursa kubwa ya kutekeleza shuhuli zake mbali mbali za kimaendeleo bila ya kuwekewa vizuizi vyovyote.
Kwa upande Hidaya Mjaka Ali kutoka jumuia ya watu wenye ulemavu, amempongeza Rais Mwinyi kwa kuanzisha mahakama maalumu inayosikiliza kesi za udhalilishaji jambo ambalo tasaidia kupatiwa ufumbuzi kwa haraka kesi za watu hao.
Kongamano hilo limeandaliwa na mtandao wa asasi za kiraia [ PACSO] ambapo ujumbe wa kongamano hilo unasema ‘Neema ya Amani na Umoja wetu, safari ya ujenzi wa Uchumi mpya inaendelea’.