NA ABDI SULEIMAN.
WANANCHI wa Shehia ya Ndagoni Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, wameamua kusamehe miti na vipando vyao ili iwe rahisi kwa serikali kutekeleza ujenzi wa barabara ya Ndagoni hadi Mkumbuu yenye urefu wa KM 11.
Wananchi hao wamesema kwa sasa wanachokihitaji wao ni ujenzi wa barabara, ndio maana wameamua kusamehe malipo ya miti na vipando vyao ili kuipanguvu serikali kuwatekelezea kilio chao hicho cha muda mrefu.
Kauli hiyo waliitoa mbele ya mkutano wa jamii, uliowashirikisha wananchi wa shehia hiyo, Mwakilishi wa jimbo la Ziwania na watendaji kutoa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na uchukuzi wakiongozwa na waziri wa Wizara hiyo.
Mohamed Mmanga Hamid alisema ndagoni inavijiji 10 hivyo kutokana na umuhimu wa barabara katika shehia yao, wamelazimika kusamehe vipando na miti yao ili kuharakisha ujenzi huo.
Alisema kwa sasa wananchio wanatarajia kuona ujenzi unaanza wa barabara hiyo, kwani wananchi wako tayari kushirikiana na serikali kwa kila kitu, ili kuona ujenzi huo unamalizika kwa wakati kabla ya kipindi cha mvua hakijafika.
“Barabara ni kilio cha muda mrefu kwetu, kipindi cha mvua hali inakua ngumu kungia katika kijiji chetu, wanawake ndio waathirika wakubwa wanapotaka kujifungua zaidi mvua zinazponyesha na iwe usiku ndio shuhuli”alisema.
Naye Mwanakhamis Saidi Mkaazi wa Ndagoni, alisema Rais Dk.Miwnyi aliahidi mambo mengi kuwafanyia wananchi hali iliyopelekea kuwa na imani katika uongozi wake, jambo lililowavutia kusamehe vipando na miti yao ili kupisha ujenzi wa barabara kijijini kwao.
Alisema kujengwa kwa barabara hiyo kutarahisisha na kungariasha zaidi uchumi wa buluu, ikizingatiwa Mkumbuu ndio eneo pelee kwa Pemba nzima linalotoka umeme.
Kwa upande wake Said Abrahman Mohamed aliyomba serikali kuwajengea barabara ya njia mbili ili iwe rahisi kwa gari ziweze kupishana, ikizingatiwa tayari kuna mwekezaji ameshajitokeza kutaka kuekeza matangi ya mafuta.
Aidha alimuomba waziri huyo katika ujenzi wa barabara hiyo, kuhakikisha inafika katika vijiji vinne ambavyo viko ndani ya shehia hiyo kama ilivyo kwa barabara ya birikau.
Mdhamini wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Pemba Ibrahim Salehe Juma, alisema kujengwa kwa barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi hususan Kisiwa cha Pemba kwani umeme wote wa Pemba unatoka katika aneneo hilo.
Alisema mara nyingi barabara hiyo ilikuwa ikifanyiwa mategenezo, lakini barabara za tope ikipita mvua shida inabakia pale pale, tayari dhamira kubwa kwa sasa ni kuitengeneza kwa kiwango cha lami.
“Katika hutuba ya Rais sekta ya ujenzi imeguswa kwa asilimia kubwa, sekta hii ndio sekta muhimu kwa uchumi wa Zanzibar bila ya barabara nzuri za kisasa hakuna kitakacho fanyika”alisema.
Naye Waziri wa Wizara hiyo Rahma Kassim Ali, aliwapongeza wananchi wa ndagoni kwa uamuzi wao wa kusamehe malipo ya vipando na miti yao ili kurahisisha ujenzi wa barabara ya kijijini kwao.
Alisema huo ni mwanzo mzuri wa kuelekea kwenye matumaini, sambamba na kuwahidi kuwa barabara hiyo itakuwa ya kwanza katika kisiwa cha Pemba kujengwa, pale harakati za ujenzi zitakapoanza za barabara za ndani.
Hata hivyo aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanatoa mashirikiano ya dhati na wajenzi wakati utakapofika, sambamba kuorodhesha majina yao kwa wananchi walioamua kusamehee vipando na miti yao kwa ajili ya kupisha barabara hizo.
Miongoni mwa vijiji ambavyo vimo ndani ya shehia ya Ndagoni ni pamoja na Ndagoni Mjini, Jamvini, Utaani, buyuni, uchangani, kunguni, Kichangani, kichangani Depu, Ngagu, Ufinguni.