Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisoma hotuba ya kuahirisha mkutano wa tano wa Bunge la Jamahuri ya Muungano wa Tanzania (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga sh. trilioni moja kwa ajili ya mikopo kwa mabenki na taasisi za fedha kwa riba ya asilimia tatu ili mabenki na taasisi hizo zitoe mikopo kwa riba isiyozidi asilimia 10.
“Serikali imeendelea kulegeza masharti ya uanzishwaji wa ofisi za wakala wa mabenki, kushusha riba inayolipwa kwa akaunti za fedha za mitandao pamoja na kutenga shilingi trilioni moja kwa ajili ya mikopo kwa mabenki na taasisi za fedha kwa riba ya asilimia tatu ili mabenki na taasisi hizo zitoe mikopo kwa riba isiyozidi asilimia 10,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Novemba 12, 2021) wakati akiahirisha mkutano wa tano wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Februari mosi, mwakani. Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2022/2023.
Akizungumzia kuhusu, riba kubwa za mikopo kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha, Waziri Mkuu amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua madhubuti kupitia Benki Kuu ya Tanzania ikiwemo kupunguza kiwango cha akiba kinachowekwa na mabenki katika Benki Kuu.
”Hatua hizo zinalenga kupunguza kiwango cha riba kwenye mikopo ya mabenki ya kibiashara na taasisi za fedha, kupunguza riba katika shughuli za kilimo kwa kiwango kisichozidi asilimia 10 na kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi ili kuchechemua shughuli za kiuchumi.”
”Licha ya hatua hizo, bado kumekuwa na changamoto ya kutoshuka kwa kiwango cha riba kinachotozwa na mabenki na taasisi za fedha. Kwa mantiki hiyo, ninaiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ikutane na taasisi za fedha nchini kuona namna wanavyoweza kupunguza riba kubwa kwenye mikopo wanayotoa hususan kwa makundi ya wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo.”
Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ishirikiane na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha inatekeleza vema Mpango wa Serikali wa kuwajengea uwezo na kuwawezesha wakandarasi wa ndani pamoja na kuendelea kulipa madeni ya wazabuni kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa maagizo sita muhimu ambayo yanatakiwa kuzingatiwa kikamilifu na viongozi na watendaji wote wa Serikali wakati wa maandalizi na utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/2023.
Waziri Mkuu amewaagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu) ashirikiane na Waziri wa Fedha na Mipango kuhakikisha wanatatua changamoto ya upatikanaji wa mafao ya wastaafu kwa wakati.
Kuhusu udhibiti wa ongezeko la madeni ya Serikali, Waziri Mkuu amewaagiza Maafisa Masuuli wote wahakikishe madai yote ya watoa huduma yanahakikiwa na kuingizwa kwenye hesabu za fungu husika; amewaonya wasiingie mikataba ya miradi mipya bila kuwa na uhakika wa upatikanaji fedha; na kuwataka wazingatie matumizi ya hati za ununuzi zinazotolewa kwenye mfumo wa malipo ili kudhibiti ulimbikizaji wa madeni.
“…Kudhibiti matumizi na kupunguza gharama. Maafisa Masuuli endeleeni kuchukua hatua za kupunguza matumizi ya Serikali yasiyokuwa ya lazima na kuhakikisha kuwa taasisi za Serikali zinazojiendesha kibiashara, zinapata faida na kuacha kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu.”
Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato ya ndani, Waziri Mkuu amesema hilo ni miongoni mwa maeneo yaliyoibua hoja kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge. “Hivyo, nisisitize kuwa Wizara ya Fedha ishirikiane na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuimarisha matumizi ya vifaa vya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Serikali.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema mbali na uwasilishwaji wa Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2022/2023 pia Bunge lilipokea, kujadili, kushauri na kupitisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.
Amesema Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2022/2023 ni wa kwanza kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambao utaendelea kutekelezwa katika maeneo mahsusi ya kipaumbele.
Mheshimiwa Majaliwa ameyataja maeneo hayo kuwa ni ya kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza biashara na uwekezaji; kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.