NA ABDI SULEIMAN.
HUDUMA za ushauri nasaha na uchunguzi wa VVU ni huduma muhimu katika kupambana na maradhi ya UKIMWI, huduma hizi huwa ni mlango wa kunufaika na matibabu ni hatua muhimu ya kinga dhidi maambukizo ya VVU.
Mwaka 1986 wagonjwa watatu waligundulika Zanzibar, huku zanzibar ikiwa imepiga hatua nzuri kupambana na maradhi ya UKIMWI, ambapo kiwango cha maambukizo kikiendelea kuwa chini ya asilimia 1 kwa takriban miaka 35 (0.4%)
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa ZAC Zanzibar Dk.Ahmed Mohamed Khatib, idadi ya watu waliopima VVU Oktoba hadi Disemba 2020, Jumla ya wanawake waliopima afya zao Pemba ni 5,773 na waliogundulika ni 20 sawa na 0.3%, wanaume ni 4,482 na waliogundulika ni 17 sawa na 0.4%.
Kwa upande wa Unguja alisema wanawake waliopima afya zao ni 26,133 waliogundulika ni 259 sawa na 0.9%, wanaume ni 21,443 na waliogundulika 152 sawa na 0.7%.
Kuhusu uwiano wa wanawake na wanaume wanaoishi na VVU hadi Disemba 2020, wanawake ni 4,828 na wanaume 2,192, kwa upande wanaotumia dawa za ARVS hadi Disemba 2020 wanawake ni 4,774 na wanaume ni 2,166.
Hivyo Wanaume wanamchango mkubwa katika kupambana na maradhi ya Ukimwi, kwani idadi kubwa ya wanaume bado wapo nyuma katika kupata huduma za kinga na matibabu ya VVU/Ukimwi, huku jitihada maalumu zikihitajika ili kuweka uwiano wa upatikanaji wa huduma kwa wanaume na wanawake.
Tunapaswa kufahamu kuwa suala la upimaji wa afya kwa sasa bado ni hiyari kwa mtu yoyote, licha ya kuwepo kwa mitazamo mbali mbali katika jamii, ikiwemo mtazamo wa dini unasemaje katika suala la upimaji wa VVU.
WANANCHI WANASEMAJE
Juma Khamis Ali mkaazi wa kangani Wilaya ya Mkoani, anasema katika Qur-an hakuna aya wala hadithi iliyokataza kupima VVU, kwani ji jambo la afya limepewa nafasi yake.
Kwa sasa imekua ni ngumu kuwaona wananchi wanarudi nyuma katika upimaji wa afya, kwani ni jambo linalomfanya mtu kujuwa afya yake.
“Hivi sasa hata wanandoa hawawezi kuowana kama hakuna cheti kinachoonyesha juu ya suala zima la upimaji wa afya, kutokana na dunia ilivyobadilika”amesema.
Naye Jeremia Yohana kutoka jiwe moja Makangale, amefahamisha kuwa suala la kujuwa afya ni muhimu sana, linawapa matumaini na upendo wanandoa au wapendanao.
Anasema upimaji huo unaepusha wanajamii kutupiana lawama pale mmoja afya yake itakapobadilika, hivyo ulipamaji umekuja kuweka mustakabli mzuri wa wanandoa kabla ya ufungaji wa ndao.
“Kipindi cha miaka ya nyuma hakukua na mambo haya, ila kwa sasa dunia imebadilika uamunifu umekua ni mdogo maradhi mengi, vizuri kupima na kujua afya ya kila mmoja”,amesema
VIONGOZI WA DINI WANAYAPI WAO
Msaidizi Katibu wa Mufti Pemba Shekhe Said Ahmad Moahmed, anasema uislamu haupingani bali unaunga mkono suala la upimaji wa VVU, kwani malengo yaliyokusudiwa kuhamasisha watu katika upimaji wa VVU ni malengo mazuri.
“Hakuna kuambukizana wala kudhuriana, lengo ni kumfanya mtu ajitambue ikiwa amepata maambukizi asimuambuke mwenzake, asiweze kuathiri kiuchumi, kijamii, kiafya”amesema.
Amesema kuwa yapo maradhi yalitokea katika zama za Mtume (S A W), ambayo ni hatari hata VVU ni maradhi ya atwaaghun (korela) ni kuambukiza na kutoa maelekezo kwa masahaba, maelekezo hayo yatatusaidia kujikinga na kutokueneza kwa jamii.
Shekhe Said amefafanua kuwa njia salama ya kumuweka mtu kuwa salama ni kupima vipimo vya afya na kujitambua kuwa yupi yuko salama na yupi ameambikizwa, kama ilivyoelezwa katika kitabu kitakatifu cha Quran aya ya 195 ya suratul bakra.
Hata hivyo aliishauri jamii, kulipa umuhimu suala la kwenda kupima VVU, kwani itaweza kumpa uhakika kuwa salama na kumpa uhakika mwanandoa mwenzake na kukilinda kiumbe kinachotayariwa kuja.
Kwa upande wake Mchungaji Paschal Mtwana kutoka kanisa la wasobato la Waadventista Pemba, amesema wao wanaamini vitabu vya Taurat na Injili, yametajwa magonjwa makuba ya kuambukizwa ila ugonjwa uliotajwa ni Tauni unahusishwa kama ilivyo Ukimwi
Katika suala la kupimwa haijawekwa wazi, lakini kanuni ya afya mwanamke na mwanamme lazima wapime kama wako wazima na mchungaji hawezi kufungisha ndoa kama wawili hawajapima.
Pia wanaendelea kuelimisha waumini kupima na kujua afya, kwani ukimwi haupatikana kwa njia ya kujamiana tu bali zipo njia nyingi zinazopelekea
“3 Yohana 1:2, 15:26 inasema “Aawambia kwamba utasikiliza kwa bidii sauti ya bwana Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake” hayo ni maagizo ya Mungu kwa wana wa Israel anawaahidi kutokuwatia maradhi kwama watafata maagizo yake,”amesema.
Alishauri ni vyema kujitambua kwa vile afya ndio muhimili wa maisha, kupima na kutambua afya ni jambo la muhimu sana katika maisha ya mwanaadamu.
HALI HALISI YA MAAMBUKIZO YAKOJE
Makamu wa Kwanza wa Rais wa zanzibar Othman Massoud Othaman, amesema licha ya mafanikio yaliyofiki katika juhudimza kupambana na UKIMWI, bado janga hilo linabaki kuwa tishio kwa ustawi wa maisha ya watu na maendeleo nchini.
Katika watu 166,566 waliopatiwa huduma za ushauri nasaha na uchunguzi wa VVU kati ya Januari hadi Septemba 2021 Zanzibar, wengi wao ni wanawake 86,947 ukilinganisha na 79,619 idadi ya wanaume.
Aidha kati ya watu 7,481 wanaotumia dawa za ARVs hadi kufikia Septemba mwaka huu, 5,170 ni wanawake ukilinganisha na idadi ya wanaume 2,427, tofauti hizi zina athari kubwa katika kudhibiti maambukizi ya VVU na kulimaliza janga la UKIMWI”.
Kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama, amesema kiwango cha upimaji wa VVU kimeongezeka kutoka asilima 61 ya makisio ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU) mwaka 2016 hadi asilimia 83 mwaka 2019.
Matumizi ya dawa za kufubaza VVU (ARV) kwa WAVIU wanaojua hali zao za maambukizi yameongezeka kutoka 95% mwaka 2016 hadi 98% mwaka 2019, kiwango cha kufubaza VVU kwa wale wanaotumia ARV kimeongezeka kutoka 87% mwaka 2016 hadi 92% mwaka 2019.
Vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kwa 50% kutoka vifo 64,000 mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2020, wakati takwimu za kiwango cha maambukizi katika jamii (HIV prevalence) zinaonyesha kiwango kilishuka kutoka 7% mwaka 2003/04 hadi 4.7% manamo mwaka 2016/17.
Kwa Upande wa Maambukizi mapya ya VVU kwa watu wazima (miaka 15 na zaidi) nchini Tanzania yameshuka kutoka 110,000 mwaka 2010 hadi 68,000 mwaka 2020. Wakati Maambukizi mapya kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto (Mother to child transmission) yameshuka kutoka 18% mwaka 2010 hadi 7% mwaka 2020.