
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewasili Jijini Durban, nchini Afrika Kusini leo (Novemba 14,2021) kwa ajili ya kushiriki ufunguzi wa Mkutano wa Maonyesho ya Biashara baina ya nchi za Afrika, unaotarajiwa kuanza kesho Jijini hapa hadi Novemba 21.
Akiwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa King Shaka Jijini Durban, Rais Dk. Mwinyi alipokewa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Mashego Dlamini, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi. Pamoja na maafisa wengine wa Ubalozi pamoja na kupokewa kwa gwaride la Heshima la nchi hiyo.
Mkutano huo ambao ni mwaliko kutoka kwa Rais wa Afrika Kusini Cyric Ramaphosa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utafuatiwa na vikao mbali mbali ambavyo vitaeleza fursa za kibiashara, masoko katika nchi za Afrika ambapo viongozi kadhaa wanatarajiwa kuhudhuria wakiwemo Marais wa nchi mbali mbali za Afriika, Marais wastaafu, pamoja na viongozi wa Mashirika ya Kimataifa.
Viongozi wa nchi mbali mbali watapata nafasi maalum ya kueleza fursa zilizomo katika sekta ya viwanda, uwezeshaji, utalii pamoja na mambo ya kiutamaduni katika nchi zao husika ambapo pia, kutakuwa na maonyesho mengine madogo madogo ya utamaduni na maendeleo ya viwanda pamoja na programu mbali mbali za vijana.
Mkutano huo ambao ni wa Pili kufanyika katika nchi za Afrika ambao mkutano wa kwanza kama huo ulifanyika nchini Misri mnamo mwaka 2018, lengo kubwa la mkutano huo ni kuwakukutanisha viongozi,wawekezaji na wafanyabiashara mbali mbali wa Bara la Afrika pamoja na kupanga mikikakati ya kuimarisha na kukuza Biashara Huria.
Katika safari hiyo, Rais Dk. Mwinyi amefuatana na mkewe Mama Mariam Mwinyi, Waziri wa Biashara na Maedneleo ya Viwanda Omar Said Shaaban pamoja na viongozi na watendaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mapema akiondoka katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Rais Dk. Mwinyi aliagwa na viongozi mbali mbali wakiongozwa na Makamo waKwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Mawaziri pamoja na viongozi wengine wa vyama vya siasa na Serikali. Rais Dk. Mwinyi anatarajiwa kurejea nchini Novemba 16,2021.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,
Ikulu Zanzibar.