Saturday, December 28

TANZANIA ILIVYOSHIRIKI KATIKA MKUTANO WA 26 WA MKATABA WA UMOJA WA MATAIFA WA MABADILIKO YA TABIANCHI ULIOFANYIKA, GLASGOW, USKOCHI- WAZIRI JAFO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Selemani Jafo amekutana na wanahabari jijini katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)jijini Dar es Salaam na kutoa taarifa ya yaliyojiri katika Mkutano wa 26 wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika mjini Glasgow nchini Uskochi.

Amesema kuwa Mafanikio ya mkutano huo yatadhihirika zaidi pale ambapo mambo yaliyojadiliwa katika mkutano huu yatatekelezwa kwa vitendo maazimio na makubaliano yaliyofikiwa lakini zaidi utekelezaji wa mikakati ya kitaifa.

Aidha aliongeza kuwa ili kufanikiwa katika hili anatoa wito kama ifuatavyo:Watendaji katika Wizara, Taasisi na Sekta binafsi watekeleze majukumu yao katika kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya hatua za kuchukua yanayozihusu Wizara na Taasisi zao katika kukabiliana na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Kwa kuwa Tanzania kupitia Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Tanzania imeungana na jumuiya ya kimataifa kupitisha na kutekeleza azimio la kuhifadhi misitu duniani, natoa wito kwa wakuu wa mikoa, wilaya na Halmashauri zote nchini kutekeleza maagizo ya kupanda miti 1,500,000 kila mwaka ili kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na kufanikisha jitihada za kuhimili mabadiliko ya tabianchi” alisema.

Amesema kwa kuwa miradi ya Kimkakati ya Treni ya Umeme (SGR), Mradi wa Umeme wa Maji wa Mwalimu Nyerere na Mradi wa Mabasi yaendayo kasi (BRT) imekuwa ni miradi ya mfano kimataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ametoa wito kwa wananchi kwa ujumla kuunga mkono utekelezaji wa miradi hiyo na watendaji wa taasisi husika kuhakikisha miradi hii inasimamiwa vizuri ili kuwa na matokeo mazuri.

Amevitaka Vyombo vya Habari, taasisi na wadau wote waongeze jitihada za kutoa elimu kwa umma kuhusu mabadiliko ya tabianchi hususan katika maeneo ya mijini na vijijini ili wananchi waweze kuchukua tahadhari na kutumia mbinu za kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta mbalimbali.

Pia amesisitiza Sekta binafsi ishirikiane na Serikali na wadau wengine katika kutekeleza maazimio ya Mkutano wa 26 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya tabianchi na mikakati ya Serikali ya kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Amemaliza kwa kusema kuwaMkutano huo umekuwa muhimu na wa manufaa makubwa kwa Taifahususan katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi hapa nchini na duniani kwa ujumla. ”Katika mkutano huo sisi kama Taifa tumeweza kuwasilisha taarifa na mchango wetu katika kupunguza uzalishaji wa gesi joto zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi. Aidha, Tanzania imeungana na mataifa mengine kuwasilisha msimamo wa nchi katika maeneo na hatua mbalimbali za kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi duniani”.