TAARIFA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) MHE. SELEMANI JAFO WAKATI WA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI AKIELEZEA MAFANIKIO YA MUUNGANO NA MAZINGIRA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA 60 YA UHURU WA TANZANIA BARA
Ndugu Wanahabari,
Kwanza kabisa napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa leo tukiwa na afya njema ili sote kwa pamoja tuweze kuwapasha wananchi taarifa muhimu.
Tunatambua mchango wenu katika kuelimisha na kuwapasha habari wananchi kuhusu mchango wa Ofisi ya Makamu wa Rais kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira ambayo imepewa jukumu la kuyasimamia.
Ndugu Wanahabari,
Kama tunavyofahamu sasa hivi tuko katika kipindi cha maandalizi ya kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara itakapofika tarehe 9 Desemba, 2021. Sote tunafahamu kuwa katika kipindi hicho cha miaka 60 ya Uhuru, Utumishi wa Umma umeendelea kuwa uliotukuka katika kuchangia ustawi wa Taifa.
Kama tunavyofahamu tarehe 9 Desemba, 2021 tutaadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara ambao umekuwa na mafanikio makubwa kwa mustakabali wa Wananchi na Taifa letu kwa ujumla.
Ndugu Wanahabari,
Itambulike kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais ilianzishwa baada ya Muungano wa Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tarehe 26 Aprili, 1964 ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume. Baada ya Muungano, Hayati Nyerere alikuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Hayati Rashid Mfaume Kawawa alikuwa Makamu wa Pili wa Rais.
Majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais ni pamoja na kuratibu masuala ya Muungano na kuimarisha Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala yasiyo ya Muungano, Kuandaa na kusimamia Sera zinazohusu Mazingira.
Aidha, majukumu mengine ni Kukuza uzalishaji unaozingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Hifadhi ya Mazingira na uzingatiaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Kuratibu na kusimamia shughuli za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Ndugu Wanahabari,
Katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru mafanikio mengi yamepatikana kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ambayo ni chachu katika ustawi wa Taifa letu. Serikali inahakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa yenye umoja, amani na usalama na Muungano wetu unaendelea kulindwa, kudumishwa, kuendelezwa na kuimarishwa.
Muungano
Tukianza na mafanikio katika Muungano, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimefanikiwa kusimamia utekelezaji wa mambo ya Muungano kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuimarika kwa utaifa na umoja, amani na utulivu na hali ya maisha ya wananchi kutokana na ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili za Muungano.
Ndugu Wanahabari,
Mambo 22 ya Muungano, kama yalivyoainishwa katika nyongeza ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 yanatekelezwa na Wizara na Taasisi zenye dhamana ya kusimamia mambo hayo. Mambo hayo yanahusu Katiba, Bunge na Utawala Bora; Uchumi; Fedha na Biashara; Ulinzi na Usalama; Diplomasia na Ushirikiano wa Kimataifa; Usafiri na Usafirishaji; Utabiri wa Hali ya Hewa; na Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Katika kipindi cha miaka 60, Serikali zote mbili zimefanikiwa kusimamia utekelezaji wa mambo hayo kwa ufanisi mkubwa na mafanikio yanaonekana katika nayanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mafanikio ya kiuchumi
Ndugu Wanahabari,
Yamefanyika mageuzi makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kiutawala kwa lengo la kufufua uchumi, kuimarisha utendaji kazi serikalini na kukuza demokrasia na utawala bora. Utekelezaji wa programu mbalimbali za mageuzi ya kiuchumi na mipango yetu ya kupunguza umaskini na kukuza uchumi imezaa matunda tunayojivunia leo.
Mwaka 1996, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sura Namba 399. Mamlaka hiyo ina Ofisi pande zote mbili za Muungano (Tanzania Bara na Zanzibar) hivyo kurahisisha ukusanyaji wa mapato katika maeneo hayo.
Nchi imeimarisha miundombinu ya barabara, usafiri wa anga, usafiri wa majini na huduma za kijamii katika pande zote za Muungano na kuendelea kutumia maliasili vizuri kwa manufaa ya wananchi kuliko ilivyokuwa kabla ya Muungano. Mafanikio haya, bila shaka, ndiyo yaliwezesha Tanzania kutangazwa kuingia kundi la nchi za uchumi wa kati kutoka kundi la nchi maskini mwezi Julai, 2020.
Mafanikio ya Ulinzi na Usalama
Ndugu Wanahabari,
Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi wenyewe ni ngao muhimu ya kulinda na kutetea mipaka ya nchi, usalama wa nchi na usalama wa mali na raia.
Kwa kipindi chote cha Miaka 60 ya Uhuru, suala la kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Ardhini, Angani na Majini) limepewa kipaumbele. Mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwa salama kutokana na ulinzi madhubuti wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kushirikiana na vikosi vingine na wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Mafanikio ya Kijamii
tunashuhudia uwepo wa Utaifa na Umoja ambapo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeunganisha watu wa nchi mbili na kuunda Taifa moja la Tanzania. Historia ya uhusiano wa kidugu wa muda mrefu baina ya watu wa Tanganyika na Zanzibar, ulikuwa chachu muhimu ya kuibua hisia za utaifa na hivyo kupanda mbegu ya utaifa. Watanzania kwa ujumla wanajivunia utaifa wao popote wanapokuwa. Lugha adhimu ya Taifa, Kiswahili inayozungumzwa takribani na Watanzania wote imechangia kuwaunganisha Watanzania na kukuza utaifa.
Elimu ya Juu
Ndugu Wanahabari,
Tunashuhudia Ubora wa elimu ya juu ukiimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwepo kwa Taasisi za Elimu za Muungano kama vile Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na Baraza la Mitihani la Taifa.Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inatoa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu Tanzania Bara na Zanzibar. Kumekuwepo na ushirikiano mkubwa katika suala la elimu ya juu ambapo wanafunzi kutoka Zanzibar wanaodahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, wanapatiwa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
Ndugu Wanahabari,
Katika kusogeza huduma karibu na wananchi wa Zanzibar Serikali imezielekeza Taasisi za Muungano kujenga au kufungua Ofisi Zanzibar. Taasisi zilizojenga au kufungua Ofisi Zanzibar ni Tawi la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ofisi ya Makamu wa Rais, Uhamiaji, Makao Makuu na Ofisi za Bunge, Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa, eneo la Uwanja wa Ndege, Zanzibar, Makao Makuu ya Mamlaka ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari Kuu, Taasisi ya Sayansi za Bahari, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, TANTRADE, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma nazo zimefungua Ofisi Zanzibar, Tume ya Atomiki (TAEC) na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) zina Ofisi za kudumu.
Aidha, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), Baraza la Taifa la Mitihani la Taifa (NECTA), Idara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TAA), Kampuni ya Posta Tanzania, Kampuni ya Simu Tanzania, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tume ya Pamoja ya Fedha, Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na Mamlaka ya Bima Tanzania.
Utatuzi wa changamoto za Muungano,
Ndugu Wanahabari,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano iliyoundwa mwaka 2005 na kuanza vikao mwaka 2006, imekuwa ni nyenzo muhimu katika kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Vikao vinavyojumuisha wajumbe kutoka pande zote mbili za Muungano vimekuwa vikifanyika katika ngazi za Wataalamu, Makatibu Wakuu, Mawaziri na Kamati ya Pamoja ya SMT na SMT chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuhakikisha changamoto zinatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.
Tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa kushughulikia hoja za Muungano kupitia vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ mwaka 2006, hoja 25 zimejadiliwa na mpaka sasa hoja 18 zimepatiwa ufumbuzi.Hoja zilizopatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano ni pamoja na Utekelezaji wa Sheria ya Haki za Binadamu Zanzibar, Utekelezaji wa Sheria ya Usafirishaji Majini (Merchant Shipping Act) katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Uwezo wa Zanzibar Kujiunga na Shirika la Bahari Duniani (International Maritime Organisation – IMO).
Hoja nyingine ni Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asili, Ushiriki wa SMZ katika masuala mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda, Gharama za Kushusha Mizigo (Landing Fees) Bandari ya Dar es Salaam kwa Mizigo inayotoka Zanzibar, Usimamizi wa Ukokotoaji na Ukusanyaji wa Kodi kwenye Huduma za Simu unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Mikataba ya Mikopo ya Fedha za ujenzi wa miradi ya SMZ.
Pia, hoja za Uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu, Ajira kwa Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano, Mgawanyo wa mapato yatokanayo na: Misamaha ya Mikopo ya Fedha kutoka IMF, misaada ya kibajeti (General Budget Support – GBS), na Uwezo wa Zanzibar kukopa ndani na nje ya Nchi zimepatiwa ufumbuzi.
Mazingira
Ndugu Wanahabari,
Kwa upande wa Mazingira, tangu tupate Uhuru mwaka 1961, kumekuwa na juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira ambapo Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliweka mkazo katika kuhakikisha wananchi wanahamasishwa kushiriki kwa vitendo katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira.
Serikali imekuwa na kaulimbiu mbalimbali za kuhimiza hifadhi ya mazingira kama vile Mtu ni Afya na Kilimo cha Kisasa pamoja na kuanzisha miradi kama vile Hifadhi ya Ardhi Dodoma (HADO) mwaka 1973 na Hifadhi Ardhi Shinyanga (HASHI) mwaka 1986 kwa lengo la kuhifadhi ardhi; kuboresha kilimo na ufugaji; na kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Pia, Serikali ilianzisha na kuimarisha muundo wa taasisi zake kwa kuweka nyenzo muhimu za usimamizi wa mazingira. Ilianzisha Idara ya Mazingira, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kutungwa kwa Sera ya Mazingira ya Mwaka 1997 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004.
Serikali imefanikiwa kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na vifungashio na mifuko ya plastiki kwa kupiga marufuku uingizaji nchini, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya vifungashio hivyo kuanzia Machi mosi, 2017 na kufanikisha kuondosha matumizi ya viroba nchini.
Ilipiga marufuku Uzalishaji, Usambazaji, Uingizaji nchini, Usafirishaji nje ya nchi na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini kuanzia Juni mosi, 2019 na Ofisi imeendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa katazo hilo katika ngazi ya Kitaifa na Serikali za Mitaa hatua iliyosaidia kupunguza matumizi ya mifuko hiyo.
Kutokana na katazo hili, wajasiriamali na vikundi mbalimbali vya wajasiriliamali vimeanzishwa na vinatengeneza mifuko ya karatasi, nguo na vikapu ambapo hadi sasa, vikundi 2,772 vinavyotengeneza mifuko mbadala vimeanzishwa huku ikikadiriwa kuwa takriban ajira 50,000 zimetokana na usambazaji wa mifuko mbadala.
Ofisi imeendelea kuratibu utekelezaji wa Kampeni ya Upandaji Miti kwa lengo la kurejesha Uoto wa Asili na kupunguza hali ya kuenea kwa jangwa na ukame ambapo kila Halmashauri ya Wilaya imeelekezwa kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka. Hadi kufikia Mei 2020 takribani miti 608,494,464 ilipandwa katika mikoa yote 26 katika Halmashauri zote. Baada ya tathmini asilimia 62.8 ya miti iliyopandwa ndiyo iliyopona.
Pamoja na hayo kutokana na umuhimu wa kulinda hifadhi ya bahari, wananchi wameshirikishwa kupanda na kuhifadhi mikoko katika maeneo mbalimbali ya Pwani Tanzania Bara na Tanzania Visiwani hatua inayosaidia kupunguza changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
Ndugu Wanahabari,
Ofisi imeendelea kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya nishati mbadala wa kuni na mkaa hususani katika taasisi za Serikali zinazotumia kiwango kikubwa cha nishati ya kuni na mkaa.
Wizara na Taasisi zikiwemo Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa, Jeshi la Wananchi, Uhamiaji, Kurugenzi ya Huduma ya Wakimbizi pamoja na Vyuo na Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zimewasilisha mipango yao ya kupunguza matumizi ya kuni na mkaa. Uchambuzi unaonesha Taasisi nyingi zinatumia gesi ya kwenye mitungi (Liquefied Petroleum Gas – LPG) pamoja, vitofali vya mkaa (Briquettes) na umeme kwa ajili ya kupikia.
Elimu kwa Umma kuhusu Hifadhi ya Mazingira
Ndugu Wanahabari,
Katika kuhamasisha ushiriki wa jamii kwenye eneo la hifadhi na usimamizi wa mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 5 Juni, Siku ya Kuadhimisha Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 17 Juni na Siku ya Tabaka la Ozoni ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarahe 16 Septemba. Maadhimisho hayo huchagizwa na matukio mbalimbali yakiwemo maonesho ya shughuli za uhifadhi wa mazingira na upandaji miti.
Pia kupitia utoaji elimu, Mafunzo ya Tathmini ya Mazingira Kimkakati yamefanyika kwa Maafisa Mazingira wa Mikoa na Wilaya zote wapatao 220. Mafunzo hayo yamefanyika kwa kanda ambapo Kanda ya Mashariki yalifanyika mkoani Pwan, Kanda ya Kati (Morogoro), Kanda ya Ziwa (Mwanza), Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) na Kanda ya Magharibi (Kigoma).
Mafunzo haya yalihusu dhana na muktadha wa Tathmini ya Mazingira Kimkakati; mchakato wa Tathmini ya Mazingira Kimkakati; na ushirikishwaji wa wadau katika tathmini. Aidha, nakala 450 za Mwongozo zilisambazwa kwa wadau katika Kanda husika.
Aidha, Mafunzo kuhusu usimamizi na uzingatiaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira yalitolewa kwa Wakaguzi wa Mazingira wapya 429. Wakaguzi hao wanatoka katika Wizara za Mambo ya Ndani ya Nchi (3), Maji (35), na Afya (17); Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (14), Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (1), Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (40), NEMC (103) na Mamlaka za Serikali za Mtaa (216).
Ndugu Wanahabari,
Elimu kwa umma ilitolewa kuhusu utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya Plastiki kupitia vipindi vya redio na runinga, makala kwenye magazeti, mabango 50 na video fupi 30. Vile vile, takribani watumiaji wa mitandao ya simu kupitia kampuni mbalimbali walifikiwa na ujumbe mfupi wa katazo husika.
Mafunzo kuhusu udhibiti wa uingizaji nchini wa kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa ya Ozoni yalitolewa kwa Maafisa Forodha 31 kutoka katika vituo vya mipakani. Aidha, mafunzo yalitolewa kwa mafundi mchundo 80 kuhusu teknolojia mpya na njia sahihi za kuhudumia vifaa vinavyotumia kemikali zinazoharibu Tabaka la Ozoni.
Ndugu Wanahabari
Elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya bioanuai katika Taasisi za Elimu ilitolewa kupitia Shindano la Uandishi wa Insha kitaifa. Shindano hili lilihusisha wanafunzi wa Shule ya Msingi, Sekondari na Vyuo vya Elimu ya Juu. Lengo la mashindano haya lilikuwa kukuza na kupima uelewa, kuhamasisha ubunifu kwa wanafunzi na vijana kuhusu mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya bioanuai. Jumla ya wanafunzi 343 walishiriki, ambapo wa kike walikuwa 133 na wa kiume 202. Shule za msingi zilizoshiriki zilikuwa 58, shule za sekondari kidato cha I – IV zilikuwa 90, Shule za sekondari kidato cha V – VI zilikuwa 38 na vyuo 30 vilishiriki.
Mwongozo wa Tuzo ya Rais ya Hifadhi ya Mazingira umepitiwa kuboreshwa na kusambazwa kwa wadau ili waweze kushiriki kikamilifu katika mashindano ya Tuzo. Maboresho yamesaidia kupanua wigo na kujumuisha masuala ya uzalishaji endelevu viwandani; matumizi ya nishati mbadala ya kupikia; uchimbaji endelevu wa madini; kilimo endelevu; usimamizi wa taka; ufugaji endelevu, na Afya na Usafi wa Mazingira.
Mikakati ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira
Ndugu Wanahabari
Katika kuimarisha hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini Mikakati mbalimbali imeandaliwa na kutekelezwa. Mikakati hiyo nipamoja na:
- i) Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Kemikali na Taka Hatarishi wa mwaka (2020 – 2025);
- ii) Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa kukabiliana na Viumbe Vamizi wa mwaka (2019 – 2029);
- iii) Mpango- Kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji wadogo wa Dhahabu (2020 -2025);
- iv) Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa Hifadhi ya Bioanuai (2015 – 2020);
- v) Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa kudhibiti kuenea kwa Viumbe Vamizi (2019- 2029); na
- vi) Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa kuongoa Mfumo ikolijia ya mto Ruaha (2017-2022)
Aidha, Mikakati iliyofanyiwa mapitio katika kipindi hiki ni pamoja na:
- i) Mkakati wa Taifa wa kuhifadhi mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji wa mwaka 2019-2024;
- ii) Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Bahari, Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa wa mwaka 2019-2024; na
Changamoto za Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira
Ndugu Wanahabari,
- Pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanyika, uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira bado ni mdogo katika baadhi ya maeneo na juhudi zaidi zinahitajika katika kutoa elimu ya mazingira kwa umma;
- Baadhi ya mila na desturi bado zinarudisha nyuma juhudi za kuhifadhi mazingira. Kwa mfano, tatizo la uchomaji moto bado ni sugu katika maeneo mengi nchini na moja wapo ya sababu ni mila potofu, mfano; mtu akianzisha moto na ukawaka kwa muda mferu na kutekeleza eneo kubwa basi ana maisha marefu;
- Tatizo la mabadiliko ya tabianchi na athari zake ni changamoto kubwa kwa jumuiya ya kimataifa na nchi yetu. Tayari nchi yetu imeshaanza kuathirika na athari zinakadiriwa kuwa zitaongezeka zaidi kwa kuwa kwa mujibu wa taarifa za kisayansi, uzalishaji wa gesijoto katika nchi zilizoendelea unaongezeka badala ya kupungua;
- Juhudi za kimataifa za kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabianchi zinakuja na changamoto pamoja na fursa. Kwa upande wa changamoto, matumizi ya sekta ya misitu yanaweza kuathiri usalama na haki ya kujitawala (sovereignty) pamoja na haki za binadamu iwapo tahadhari hazitachukuliwa katika utekelezaji wake. Aidha, kilimo cha mazao kwa ajili ya kuzalisha nishati hususan biofueli inaleta changamoto kwa usalama wa chakula na mazingira nchini;
- Kutokuwepo kwa mfumo madhubuti wa utunzaji wa takwimu, taarifa na kumbukumbu za masuala ya mazingira na hivyo kusababisha ucheleweshaji wa maamuzi ya kisera na kimkakati;
- Kwa kiasi kikubwa Tanzania imeendelea kutekeleza shughuli za mazingira kwa kutegemea fedha za wafadhili jambo ambalo linasababisha kutekelezwa baadhi ya miradi ambayo siyo ya kipaumbele kwa taifa;
- Baadhi ya wawekezaji wanakwepa kufanya tahmini ya athari kwa Mazingira kwa miradi wanayoitekeleza jambo linalosababisha kutokuwepo kwa uzalishaji endelevu;
- Ufinyu wa bajeti ya Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mikakati na programu zinazoandaliwa umepelekea kuendelea kwa uharibifu wa mazingira nchini;
- Hali ya umasikini katika jamii inasababisha ongezeko la uharibifu wa mazingira nchini kutokana na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za misitu, maji, madini, bahari na maziwa;
- Hali ya ukame katika baadhi ya mikoa inasababisha kutofikiwa kwa malengo ya idadi ya miti inayotakiwa kupandwa na hivyo kurudisha nyuma juhudi za utunzaji wa mazingira hususan katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Manyara na Kilimanjaro; na
- Suala la uchomaji wa moto misitu na uharibifu wa mazingira kwa njia ya ukataji miti ovyo kwa ajili ya nishati na kilimo katika baadhi ya maeneo nchini unaendelea kwa kasi licha ya kuwepo kwa juhudi zinazofanywa na serikali. Ukataji miti kwa ajili ya nishati unaosababishwa na kuwepo kwa gharama kubwa za kununua nishati mbadala kama vile umeme na gesi ambapo jamii inashindwa kumudu. Aidha, ongezeko kubwa la watu nchini linasababisha kuongezeka kwa mahitaji ya ardhi kwa ajili ya kilimo na makazi.
Pamoja na changamoto hizi, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi imeendelea kutekeleza mipango, mikakati na programu mbalimbali kwa ajili ya kuhifadhi mazingira. Jamii inaendelea kuhamasishwa kuthamini mazingira na kuunga mkono juhudi mbalimbali za Serikali za kupambana na uharibifu wa mazingira ili tuweze kufikia maendeleo endelevu.
Ndugu Wanahabari,
Ofisi imeendelea kutekeleza mipango na miradi mbalimbali ya hifadhi na usimamizi wa mazingira ambayo ni pamoja na Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Uhakika na Usalama wa Chakula katika Maeneo Kame ya Tanzania, Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini, Mradi wa kujengea uwezo taasisi ili Kupunguza Hewa Ukaa inayosababishwa na ukataji miti na uharibifu wa misitu ifikapo mwaka 2022, Mradi wa kujenga uwezo wa Kitaifa kuwezesha utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Mradi wa Majaribio wa Kikanda wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Bonde la Ziwa Victoria.
Aidha, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuweka mfumo wa Usimamizi wa Mazingira nchini tangu Azimio la Rio na kuanzishwa kwa Idara ya Mazingira. Serikali imeendelea kuungana na Jumuiya ya Kimataifa katika kukuza juhudi za kuhifadhi Mazingira kupitia Mikataba mbalimbali ya Kimataifa. Serikali ya Tanzania imesaini na kuridhia jumla ya Mikataba 10 na Itifaki 8.
Ndugu Wanahabari,
Kwa kutambua na kuzingatia fursa na changamoto zilizopo, katika miaka ijayo, Serikali inatarajia kwamba Muungano utaimarika na mafanikio yaliyopatikana yataendelezwa kwa lengo la kuinua hali za maisha na ustawi wa wananchi wa pande mbili za Muungano. Kuimarika na kudumu kwa Muungano kutakuwa ni nguzo muhimu ya kuendeleza udugu na matarajio ya Waasisi wa Muungano ya kuwa na Tanzania yenye uchumi imara, Amani, utulivu, haki na usawa kwa kila Mtanzania.
Aidha, katika hifadhi na usimamizi wa Mazingira tunatarajia kuendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali katika shughuli za hifadhi mazingira ikiwemo: kuhamasisha upandaji miti na matumizi ya nishati mbadala kwa azma ya kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabia nchi; kulinda na kutunza vyanzo vya maji, udhibiti wa taka ngumu, kuendelea kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, na kutekeleza Kampeni Kabambe ya hifadhi na usafi wa mazingira. Kimsingi tunatarijia mazingira endelevu yatakayochochea ukuaji wa kiuchumi, ustawi ya jamii na Tanzania ya kijani.
Matarajio ya baadaye
Ndugu Wanahabari,
Kwa kutambua na kuzingatia fursa na changamoto zilizopo, katika miaka ijayo, Serikali inatarajia kwamba Muungano utaimarika na mafanikio yaliyopatikana yataendelezwa kwa lengo la kuinua hali za maisha na ustawi wa wananchi wa pande mbili za Muungano. Kuimarika na kudumu kwa Muungano kutakuwa ni nguzo muhimu ya kuendeleza udugu na matarajio ya Waasisi wa Muungano ya kuwa na Tanzania yenye uchumi imara, Amani, utulivu, haki na usawa kwa kila Mtanzania.
Aidha, katika hifadhi na usimamizi wa Mazingira tunatarajia kuendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali katika shughuli za hifadhi mazingira ikiwemo: kuhamasisha upandaji miti na matumizi ya nishati mbadala kwa azma ya kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabia nchi, kulinda na kutunza vyanzo vya maji.
Matarajio mengine ni udhibiti wa taka ngumu, kuendelea kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na kutekeleza Kampeni Kabambe ya hifadhi na usafi wa mazingira iliyozinduliwa Juni 5, 2021. Kimsingi tunatarijia mazingira endelevu yatakayochochea ukuaji wa kiuchumi, ustawi ya jamii na Tanzania ya kijani.
Hitimisho
Ndugu Wanahabari,
Mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka 60 ya Uhuru yametokana na jamii yenye umoja, mshikamano na isiyo na ubaguzi. Watu wa pande mbili za Muungano wanaishi na wanafanya kazi zao za kujiletea maendeleo katika sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kubughudhiwa. Aidha, Ofisi ya itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kutekeleza mipango, mikakati na programu mbalimbali za kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu.
Tunapoadhimisha Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, tuna kila sababu ya kuwakumbuka na kuwaenzi Waasisi wa Taifa letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume. Ni ukweli usiopingika kwamba, Muungano wetu ambao msingi wake ni historia ya karne nyingi ya ushirikiano wa watu wa pande hizo mbili na hatimaye kurasimishwa na Waasisi wetu mwaka 1964 umezidi kuimarika na kuenziwa. Mafanikio makubwa tuliyopata siyo ya kubezwa hata kidogo na yanapaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa kwa nguvu zote.
Ndugu Wanahabari,
Nawashukuru kwa ushirikiano wenu mnaotupa kila tunapowahitaji kwa ajili ya kuuhabarisha Umma kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira yanayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na niwaombe tena tuendelee kupeana ushirikiano.
Asanteni kwa kunisikiliza