Friday, March 14

 

c

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Novemba 21 mpaka Disemba 18, 2022 fainali za Kombe la dunia zitakuwa zikifanyika nchini Qatar, zikiwa za mwisho kushirikisha mataifa 32. Kuanzia fainali za mwaka 2026 zitakazofanyika katika nchi za Marekani, Mexico na Canada, idadi ya timu zitaongezeka na kuwa 48.

Toka mashindano haya yaanzishwe mwaka 1932, miaka 89 iliyopita, hakuna timu kutoka Afrika Mashariki iliyowahi kushiriki fainali zake. Si Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda wala Burundi iliyowahi kushiriki fainali hizo. Ukiachilia mbali DRC Congo mwanachama mpya mtarajiwa wa Afrika Mashariki, ambayo iliwahi kushiriki mara moja katika mashindano ya mwaka 1974.

Je mataifa haya yana mkosi? Ni swali tata lakini unaweza kusema hivyo, mataifa haya, labda yana mkosi kwenye soka kama utatazama kwa jicho hilo. Kenya inafanya vizuri kwenye riadha kama iivyo kwa Uganda, majina kama Joshua Chiptegei, Jacob Kiplimo na enzi hizo John Akii-Bua yakiiweka Uganda kwenye sura nyingine ya michezo. Kenya kama baba wa mbio ndefu ikijitambia kina Eliud Kipchoge, David Rudisha, Brigid Jepscheschir Kosgei na wengine wengi.

Tanzania enzi za kina Filbert Bayi, Suleiman Nyambui John Stephen Akhwari na Juma Ikangaa, ilifanya vyema pia kwenye riadha, ingawa kwa sasa kina Hassan Mwakinyo wanaipaisha nchi hiyo kwenye ndondi duiani. Lakini kwa jicho la mbali ziko sababu sugu za muda mrefu na muda mfupi zinazofanya mataifa ya Afrika Mashariki kuwa wasindikizaji wa michuano ya kombe la dunia kwa miaka mingi

Uongozi: Utawala mbovu na migogoro isiyo na kikomo

Soka la Afrika Mashariki, linakutana na mizozo ya kila leo ya kiutawala na uendeshaji. Imekuwa kawaida kwa miaka mingi kushuhudia mizozo, isiyo na mwisho kuanzia kwenye mashirikisho ama vyama vya soka vinavyosimamia mpira mpaka kwenye vilabu vya mataifa husika.

‘huu ni mwiba na mfupa wa muda mrefu unaosumbua soka letu, ukiona Yanga pametulia, ujue simba kunafukuta, au kinyume chake, na kwenye shirikisho, utawala huu ukitulia basi unaokuja unakuwa na vibweka,’ anasema Juma Shomvi, mfuatiliaji wa soka na kutoka Morogoro.

Kwa mujibu wa Shomvi, migogoro iliyoshuhudwa katika nchi za Tanzania, Kenya na hata Rwanda, iwe kwa ngazi ya vilabu ama ngazi ya mashirisho na vyama vya soka, yanarudisha jitihada za kusaidia soka lenyewe.

‘viongozi hawafikirii kuhusu mipango ya kuinua soka, wanafikiria nafasi zao, a muda mwigi unatumika kusuluhisha mizozo badala ya kusimamia soka na kufikiria kuboresha soka

Rushwa na matumizi mabaya ya fedha

Wiki hii, vigogo wa soka la Kenya, akiwemo Rais wa shirikisho la soka la nchi hiyo (FKF) Nick Mwendwa kukamatwa kwa sababu ya matumizi mabaya ya fedha.

H
Maelezo ya picha,Rais wa shirikisho la soka la nchi hiyo (FKF) Nick Mwendwa anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha

Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) lilimfungia miaka 10, rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi kwa matumizi mabaya ya fedha za shirikisho hilo. Fifa ilisema Malinzi alipokea dola 528,000 ukiwa ni mkopo kwa miaka minne aliyokuwa madarakani, lakini alishindwa kutoa taarifa sahihi ya matumizi ya fedha hizo.”

Malinzi na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Celestine Mwesigwa, aliyekuwa Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani Flora Rauya walifunguliwa kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 wakikabiliwa na mashitaka 20 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa Dola za Marekani 173,335.

Ismail Aaden Rage, aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha soka Tanzania(FAT), sasa ni shirikisho (TFF), aliwahi kuhukumiwa mika 3 jela kwa madai ya kuiba Sh milioni 1 kutoka Salvation Army ya jijini Dar es Salaam ambako timu ya Taifa iliweka kambi kwa ajili ya maandalizi na michezo ya kimataifa na Sh 400,000 alizodaiwa kuwalipa posho wachezaji. Baade alikata rufaa na kushinda kesi hiyo.

‘nchi zetu masikini, hazina fedha za kusimamia mpira na zilizoko chache, zinapigwa (zinaibiwa), na wajanja wachache, mpira ni pesa ni ngumu kufanikiwa kama wenzetu (Ulaya)’, alisema Shomvi

Ukiacha hilo, kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya upangaji wa matokeo kwa ligi za ndani unaochochewa na rushwa. Makelele haya sio bure, pengine kuna haja ya kutupiwa macho zaidi hasa kwa ligi za ndani zinazojenga soka la ushindani kwa timu za taifa.

Mipango isiyobebeka na soka la vijana

a

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Idrissa Gueye wa Everton wakati huo akiwana watoto wadogo wa shule ya Msingi Uhuru Dar es Salaam, Everton ilipokuwa Tanzania kujianda na msimu wa 2017/2018

Mipango ya muda mrefu na mipango ya muda mfupi, ni masuala yanayowekezwa kipaumbele kwenye soka la sasa duniani. Kuanzia, uwekezaji kwenye soka la vijana mpaka uwekezaji kwenye eneo la ufundi.

Maandalizi yanaanzia kwenye mipango, na mipango mizuri ni ile inayohusisha soka la soka la vijana

Sababu za muda mrefu na mfupi zinachangia, ikiweo kupuuza soka la vijana, amblo ndio singi wa mafanikifo ya wenzetu’, anasema Daniel Mlimuka, mchambuzi wa soka Tanzania

Angala kwa sasa nchi kama Tanzania, imeanzisha ligi za vijana kwa timu za ligi kuu, pia kumekuwa na shule kadhaa za soka la vijana zilizoanzishwa katika maeneo mbalimbali, lakini miundo mbinu ya viwanja, fedha za uendeshaji na usimamizi wa vijana hao kisoka kutokana na mazingira wanayotoka ya kimasikini, huenda ikawa changamoto kubwa.

Miundo mbinu ya viwanja

Sheria kuu ya soka ni uwanja, lakini kwa Afrika mashariki viwanja vyake viko hoi bin taaban. Leo pengine ni viwanja vichache ule wa Benjamin Mkapa Tanzania, Kasarani Kenya, Mandela Uganda na Amahoro Rwanda, inaweza kutumika kwneye michuano ya kimataifa ya kiwango fulani. Viwanja vingi ni vibovu visivyo na hadhi ya viwango.

‘unawezaje kushiriki kombe la dunia, ikiwa timu zako hazina viwanja, zinategemea viwanja vya umma, watoto wanacheza wapi leo, kila sehemu kuna nyumba?, anahoji Shomvi.

Ukitaja viwanja vizuri 10 vya soka Afrika, Afrika Kusini inaweza kuingiza viwanja 6 kama Soccer City, Moses Mabhida, Cape town, Pete Makaba, Nelson Mandela Bay na Mbombela, Kule Morocco viko vingi ukiwemo wa Stade Mohamed V, Algeria kuna Stade du 5 Juillet au El Djezair, Nigeria inao wa Sam Ogbemudia na Misri inao ule wa Borg Al Arab au Cairo. Ni ushahidi angalau viwanja vizuri vya mataifa haya makubwa Afrika vimekuwa msaada kutengeneza hamasa na soka la nchi hizo kusaidia kufanya vyema kimataifa.

Ligi za ndani na wachezaji wa kulipwa

Soka sasa ni ushindani, kuna na ligi bora ya ndani ni msaada wa kutengeneza kikosi bora cha timu ya taifa, ama kuwa na wachezaji wengi wanaocheza ligi zenye ushindani zikiwemo Ulaya unakuwa kwneye nafasi nzuri ya kufanya vyema, kutokana na viwango vikubwa vya mataifa yaliyoendelea kisoka na namna wanavyoubeba mpira wao.

Mbwana Samatta, nahodha wa Tanzania anayecheza Ubelgiji, unaweza kusema, ndiye mchezaji pekee angalau kutoka Tanzania kucheza ligi zenye Ushindani wa kueleweka Ulaya, Kenya imekuwa na wachezaji wakuhesabu kina Victor Wanyama kama ilivyo kwa Uganda.

a

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Nahodha wa Samatta akiwafunga Liverpool, kwenye ligi ya mabingwa Ulaya, wakati huo akiichezea Genk ya Ubelgiji

Leo mataifa mengi Afrika Magharibi, Kaskazini na hata Kusini, yamejaza wachezaji wenye majina makubwa kwneye soka la Ulaya kama Mohamed Salah, Mohamed Elneny (Misri) Sadio Mane na Edouard Mendy (Senegal), Partey (Ghana), Hakim Ziyech na Achraf Hakimi (Morocco), Riyah Mahrez (Algeria), Wilfred Ndidi, Kelechi Ihenacho na Victor Moses (Nigeria)

Ukiangalia mataifa ya Afrika yaliyofuzu hatua ya pili ya kombe la dunia kutoka Afrika ; Cameroon, Misri, Morocco, Nigeria,Tunisia, Algeria, Senegal, Mali, Ghana na DRC yana wachezaji wengi kwenye mataifa ya Ulaya na yanawapa faida kubwa yanapokutana na mataifa kama ya Afrika Mashariki yenye wachezaji wengi wa ligi za ndani.

Daniel Mlimuka, mchambuzi wa soka Tanzania anasema ‘kuwa na wachezaji waaocheza ligi zenye ushidani unakuwa na faida, mfano ni mechi ya Tanzania na DRC, DRC walinufaika na faida hiyo’.

‘Nigeria, Misri, Algeria, Cameroon, Senegal, Ghana yamekuwa yakifuzu mara kwa mara kweye fainali za Afrika na dunia kwa sababu ya kuwa na faida ya wachezaji wanaocheza Ulaya’, uwezo wao, uzoefu wao na utimamu wao ni mkubwa wa ligi kubwa unayapa faida mataifa haya’, alisema.

Mataifa ya Afrika yanaweza kufanya nini sasa?

‘hakuna uchawi kwenye soka la Afrika, tukubali kuwekeza kwenye soka la vijana, huu ni muarobaini pekee wa kututoa hapa, anasema Shomvi.

Shadrack Mwansasu, mwandishi wa habari za michezo wa BBC Tanzania anasema kuna kazi kubwa ya kufanya kufikia mafanikio kimataifa lakini yanawezekana kama mambo muhimu yatazingatiwa

f

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Ni kawaida kukuta watoto Afrika Mashariki, wakicheza kwenye viwanja vibovu, peku na mpira usiofaa

‘miundo mbinu ni muhimu kwa soka, viwanja vizuri vyenye hadhi ni muhimu, malazi kwa wachezaji, vifaa vya michezo,vyakula na walimu bora, mambo haya yanaweza kututoa shimoni’, alisema Mwansasu.

Kwenye hili la soka la vijana ambalo ni la muda mrefu, Mchambuzi Daniel Mlimuka anaongezea suluhisho la muda mfupi, ambalo linaweza kusaidia kwa sasa; ‘wenzetu wanafaida kubwa ya kuwa na wachezaji wengi wanaocheza nje, hata kama soka la vijana halijatengemaa kwa sasa’,

Mlimuka anatolea mfano wa mechi kati ya Tanzania na DRC, ambayo ilikuwa muhimu kwa taifa hilo la Afrika Mashariki kufuzu hatua ya pili.

‘Stars walipata nafasi nyingi lakini walishindwa kuua mechi, walikuwa wana papara….walikosa utulivu, DRC hawakuhitaji nafasi nyingi kupata magoli, kwa sababu tu walikuwa na watu wanaoweza kuamua mchezo, kwa uzoefu wao wa kimataifa’, alisema.

Ukiwasikiliza watu wanaofuatilia soka, wanataja miundo mbinu, soka la vijana na ufundi kama vitu muhimu kabisa, lakini yako mengine kama kuwa na ligi bora za ndani, kuwa na idadi kubwa ya wanaocheza soka kwenye ligi zenye ushindani Ulaya, Utawala bora na uwekezaji wa kifedha unaweza kusaidia mataifa ya Afrika Mashariki kujiuliza yanapojiandaa na harakati za kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2026