NA ABDI SULEIMAN.
ASASI zisizo za Kiserikali Kisiwani Pemba, zimesema kuwa mwaka mmoja wa Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi madarakani, umepelea asasi hizo kuwa huru kufanya kazi zao bila ya vikwazo vyovyote.
Kauli hiyo wameitoa katika kongamano la siku moja la kumpongeza Rais Dk.Hussein Mwinyi kutimiza mwaka mmoja madarakani, liliandaliwa na Ofisi ya Mrajis wa NGOs Pemba, kwa kushirikiana PACSO.
Mtaribu wa Jumuiya ya Tumaini Jipya Tatu Khamis Mselemu, alisema asasi hizo zimepata mafanikio makubwa ndani ya mwaka mmoja huo ikiwemo kufanya kazi zao bila ya kuingiliwa na taasisi yoyote.
Alisema ni wakati wao wa kujipanga ili kufanya kazi zao vizuri, kutokana na viongozi waliopo madarakani ambao wamekuwa bega kwa bega katika uwafanyaji wao wa kazi.
Omar Mjaka Ali alisema Dk. Mwinyi amefanya mambo makubwa ndani ya mwaka mmoja madarakani, kutokana na kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar kuwa wamoja, pamoja na kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Alisema jambo jengine kuwafanya wazanzibari kutumia bahari kwa asilimia kubwa katika shuhuli zao za uchumi, sera ambayo imeonekana kuwavutia vijana wengi.
Naye Rukia Ibrahim alisema vijana wamejenga imani kubwa na serikali ya awamu ya nane (8) katika sera ya uchumi wa buluu, ambao utaweza kuwaokoa vijana wengi nchini na kuachana na utegemezi.
Hidaya Majaka Ali mwakilishi kutoka watu wenye ulemavu, amemshukuru Rais wa Zanzibar kwa kuanzisha mahakama maalumu ya kushuhulikia kesi za udhalilishaji ambayo imepeleka faraja na matumaini kwa watu wenye ulemavu.
Aidha alishauri kuzingatiwa kwa miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, katika harakati za kuelekea kwenye uchumi wa buluuu ili uweze kuwanufaisha wote.
Afisa mdhamini Ofisi ya Rais tawala za mikoa serikali za mitaa na Idara maalumu za SMZ Thabit Othman Abdalla, alisema mwaka mmoja wa Dk. Mwinyi madarakani, umeonyesha nia nzuri kwa viongozi waliopo madarakani kuendana na kasi yake.
“Rais Mwinyi amekua akichukizwa na viongozi wasio kuwa waaminifu, wabadhilifu wa mali za umma, wizi, udanganyifu na kupelekea kuwaondosha madarakani”alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, alisema serikali inatambua mchango wa Asasi za Kiraia, katika kujenga mustakbali wa maisha, hivyo wanapaswa kuendelea kuijenga Zanzibar kuwa kitu kimoja.
Hata hivyo alizitaka NGOs kuhakikisha zainaendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini, kwani amani ndio kila kitu katika nchi yoyote ile duniani.
MWISHO