NA ABDI SULEIMAN.
KAMATI ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, imesikitishwa na kitendo cha kutokuwepo kwa Mkurugenzi au kaimu mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar katika ziara ya kamati hiyo Pemba.
Kamati hiyo imesema sababu ya kukosa ndege ya kuwasili Pemba kutoka Unguja haina mashiko yoyote, kwani ratiba ya ujio wa kamati hiyo na maeneo itakapokwenda inatambuliwa muda mrefu na sio ya kukurupuka.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Yahya Rashid Abdulla, mara baada ya kupokea taarifa ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Pemba kutoka kwa meneja wa ZAA Pemba Rajab Ali Mussa.
Alisema kamati haikuridhishwa na mwenendo wa mkurugenzi huo, kwani ratiba yao iko hata katika serikali kuu, kwani isifike pahali tukaanza kushtakiana wakati mambo yanapaswa kutatuliwa mapema.
“Sote tunatumikia watu kwa kazi, wananchi wanahitaji kujua na kupatiwa ufumbuzi wa masuala mbali mbali, sisi kazi yetu ni kuwasukuma nyinyi mukapata kutekeleza vizuri”alisema.
Aidha Mwenyekiti huyo alitaka kutambua kuwa Rais anaendelea kuzungumzia suala la uaminifu, uwadilifu katika miradi mikubw aya maendeleo, ambayo zaidi inawalenga wananchi moja kwa moja kwani wananchi bado wanaendelea kuwa na imani na serikali yao.
Akizungumzia ujenzi wa barabra ya Chake-Wete njia Kongwe, alisema wamekua wakishuhudia miradi mingi inafeli kutokana na mikataba inayotiwa saini kushindwa kutekelezwa, ipasavyo na kuonekana mwanzo na Mwisho wa mradi.
Kwa upande wa mnara wa kuongozea meli Kigomasha, alisema serikali imeelekeza suala la uwekezaji huku akitaka kujua imejipanga vipi katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Mjumbe wa kamati hiyo Mussa Fumu Mussa, alisema kwa kipindi kikubwa sana serikali inaandamwa na fedha nyingi sana za ulipaji wa fidia za nyumba na vipando vya wananchi, mara baada ya ujenzi kupita na nyumba kuharibika.
Naye mjumbe mwengine wa kamati hiyo Kombo Mwinyi Shehe, alisema zipo barabara zilizojengwa na kampuni ya MECCO, hivyo Wizara inapaswa kuwa makini katika barabara hiyo kwani inagusa maisha ya watu wengina na wakati mmoja.
Alisema ili kunusuru kujirudia kama yaliyotokea katika barabara ya Wete-Konde, lazima msimamizi wa ujenzi kuwa makini na ujenzi uwendane na mikataba na makubaliano yaliyosainiwa mwanzo.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara ya Wete-Chake Chake njia kongwe, afisa mdhamini wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Ibrahima Salehe Juma, alisema mradi huo umetengewa jumala ya USD 23 milioni, USD 10.0 milioni mchango wa BADEA, USD 11.4 Milioni ni mchango wa Saudi Fund na USD 1,6 Milioni mchango SMZ.
Alisema wizara tayari imeshafanya vikao vilivyowashirikisha wakuu wa mikoa miwili ya Pemba na taasisi mbali mbali amabzo kwa namna moja zitahusika katika utekelezaji wa mradi huo ili kuwez kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza.
Alisema tayari tathmini ya majengo ilishafanywa na sasa wanataka kupitia tena kutokana na tathmini ya awali gharama ni kubwa, ikilinganishwa na gharama ya mradi.
Aidha alifahamisha kuwa fidia ya kwanza ilikua ni Bilioni 14 na miti Milioni 500, huku wakiwashirikisha masheha na viongozi wengine wa serikali katika mradi huo.
Akitoa taarifa ya Mnara wa kuongozea Meli Kigomasha kwa wajumbe wa kamati hiyo, mkurugenzi wa bandari Tawi la Pemba Abdalla Salim Abdalla, alisema mnara wa kigomasha ni miongoni mwa minara minane ya shirika hilo, ambapo Pemba inaminara miwili inayotoa huduma za kimataifa.
Alisema minara hiyo hutumika kuongozea vyombo vinavyopita ama kuelekea India, Nchi za Falme za kiarabu (UAE), China na Ukanda wote wa kaskazini kuja Tanzania au kwenda Afrika ya Kusini.
Alifahamisha kuwa mnara wa Kigomasha ni miongoni mwa vyanzo vya mapato vinavyoingiza serikali fedha za kigeni, kwa mwezi unaingiza mapato wastani wa T.sh 17,666,666,67 sawa na T.sh 211,999,1000.00 kwa mwaka.
naye Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Pemba Rajab Ali Mussa, alisema Wizara kupitia bajeti ya 2021/2022 imetenga jumla ya Tsh Bilioni 2 kwa ajili ya ulipaji wa fidia ya watakaoathirika na ujenzi wa uwanja huo.
MWISHO