NA ABDI SULEIMAN.
SKULI ya Chasasa Secondari imefanikiwa kubuka mshindi wa kwanza, katika Kongamano la kupima uwelewa kwa wanafunzi, juu ya masuala ya Ukimwi na Elimu ya Afya ya Uzazi kwa vijana, baada ya kupata asilimia 73% ya majibu ya maswali walioulizwa.
Mashindi wa pili katika kongamano hilo la maswali na Majibu ni skuli ya Wete IslamiC Sekondari kwa kupata 65%, nafasi ya tatu ikachukuliwa na Uweleni Sekondari ilipata 64%, nafasi ya nne Tumbe Sekondari ilipata 60%, Dr.omar Sekondari 42% na Istiqama Secondari 41%.
Kongamano hilo la kupima uwelew kwa wanafunzi hao, juu ya kujibu maswali lilifanyika mjini Chake Chake, ikiwa ni shamra shamra kuelekea siku ya Ukimwi Duniani.
Akizungumza na wanafunzi hao Afisa Mdhamini Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Ahmed Aboubakar Mohamed, alisema vijana ndio viongozi wa sasa na ili kufikia huko lazima walinde afya zao, jambo la kusikitisha mpaka sasa 25% ya vijana Zanzibar ndio wenye uwelewa juu ya elimu inayohusiana na HIV.
“Kutokana na sensa ya 2012 wazanzibari wako Milioni 1.5, ukiigawa kwa thuluthi tatu vijana walioko skuli ni laki 5, kama wanafunzi hao wanaoelewa ni 25% kuna uwezekano wanafunzi laki 3.5 hawajuwi chochote kuhusiana na elimu ya HIV, ili kuwa raia bora, kiongozi bora na raia mwema upate elimu juu ya Ukimwi”alisema.
Aidha aliwataka vijana kutambua kuwa wanapaswa kuzingatia suala zima la elimu, pamoja na kutokukubali kushawishika au kurubuniwa, kwani wanapaswa kuishi katika maisha kama wanayoishi na familia zao.
Aliwaomba wanafunzi kuwa mabalozi kwa wenzao ambao hawakupata nafasi ya kufika hapo, kwa kutoa elimu inayohusiana na suala zima la Ukimwi na elimu ya afya ya uzazi, huku wakipaswa kuitumia vyema mitandao ya kijamii, ambao imekua ni changamoto kubwa kwa vijana.
Mkurugenzi wa Tume ya Ukimwi Zanzibar alisema lengo kuu ni kupeana elimu juu ya Maambukizo ya Virusi vya Ukimwi kwa wanafunzi, kwani utafiti uliofanywa mwaka 2016/2017 Tanzania nzima, unatathmini maambukizi ya ukimwi iko vipi kwa Tanzania ikiwemo Zanzibar na kuonyesha kuwa Zanzibar ina 0.4% ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.
Alisema utafiti huo uliangalia uwelewa wa jamii na watu wazima, umeonyesha vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 ni 25% tu wenye uwelewa sahihi juu ya Ugonjwa wa Ukimwi.
“Ili tuweze kujikinga na maradhi yoyote jambo la kwanza ni suala zima la elimu na ndio maana tumekutana na vijana hawa wa skuli za Sekondari na kuwapatia elimu ya afya ya uzazi”alisema.
Aidha alisema bado uwelewa kwa vijana nchini uko chini, licha ya kuwa ni miaka 36 tokea Ukimwi kuingia nchini, utafiti umeonyesha Mkoa wa Kusini uko chini sana, juu ya uwelewa maradhi hayo na 14% ya vijana katika Mkoa huo ndio wenyeuwelewa sahihi juu ya Ukimwi.
Naye mratibwa Tume ya Ukimwi Pemba Ali Mbarouk Omar, alisema lengo ni kujifunza ili kuweza kujikinga, kujilinda kwani umri wa vijana ni muhimu katika maisha ya watu.
Kwa upande wa wanafunzi ambao skuli zao zimeshika nafasi ya kwanza na Pili, waliwataka wanafunzi wenzao kuhakikisha wanajielewa na kujitambua kwani ugonjwa wa Ukimwi ni hatari na vijana ndio tegemeo la taifa.
MWISHO