Wednesday, October 30

ZAECA yakutana na waandishi wa habari kuelekea siku ya Rushwa Duniani

 

WAANDISHI wa Habari kutoka Vyombo mbali mbali vya habari Pemba, wakifuatilia kwa makini Ufunguzi wa mkutano wa siku moja juu ya kupambana na Rushwa, ikiwa ni shamrashamra ya kuadhimisha siku ya Rushwa Duniani, Mkutano uliofanyika mjini Chake Chake.
MKURUGENZI wa Mamlaka ya kuzuwia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ACP Ahmed Khamis Makarani, akizungumza na waandishi wa habari Pemba, ikiwa ni shamrashamra ya kuadhimisha siku ya Rushwa Duniani, Mkutano uliofanyika mjini Chake Chake
MWENYEKITI wa Klabu ya Waandishi wa Habrai Pemba Bakar Mussa Juma, akiongoza mkutano wa waandishi wa habari na ZAECA ikiwa ni shamrashamra ya kuadhimisha siku ya Rushwa Duniani, mkutano uliofanyika mjini Chake.

NA ABDI SULEIMAN.

Jamii nchini imetakiwa iondokane na jambo muhali ili kuisaidia Serikali katika kupiga vita rushwa na uhujumu uchumi kwa maslahi yao na  Taifa kwa ujumla.

Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya kuzuwia Ruswa Zanzibar,Ahmed Khamis Makarani   wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari juu ya kupambana na rushwa ikiwa ni shamrashamra ya kuadhimisha siku ya rushwa Duniani katika ukumbi wa Wizara ya fedha ulioko Gombani.

Mkurgenzi huyo alisema kuwa wahusika wa mamalaka hiyo Zanzibar wanafahamu kwamba kuna umuhimu mkubwa kuwakutanisha waandishi wa habari kuwapatia elimu ya kupambana na rushwa ili nao sasa wafanye kazi zao za kuandika habari mbali mbali za kuelimisha jamii juu ya kupambana na tatizo hilo kwa lengo la kuisaidia Serikali na Taifa .

“Sisi kama ZAECA tunafahamu kwamba waandishi wa habari muna umuhimu mkubwa  kwetu na jamii katika kutusaidia kuelimisha jamii juu ya kupambana na rushwa na uhujumu uchumi ili kuwa na jamii yenye maendeleo,” alisema mkurugenzi huyo.

Makarani alieleza kuwa mamlaka ya kuzuia rushwa Zanzibar ZAECA imekuwa ikishirikiana na wadau wengine nchini kuhakikisha kila Disemba 9 ya kila mwaka huazimisha siku hiyo, ikiwa na lengo la kuona kwamba wanapiga hatua ya kupinga rushwa na uhujumu uchumi kwa ambao hufanywa na baadhi ya wahalifu wasioitakia mafanikio nchi.

Aidha alifahamisha kuwa utafiti uliofanywa mwaka 2012 ulionyesha kwamba bado jamii inalo tatizo kubwa na zilitajwa aina tatu kubwa za rushwa ikiwemo rushwa muhali ambayo ndio inayoumiza.

“Rushwa muhali ndio iliyopewa kipaombele na ndio inayoumiza na hiyo inatokana na jamii kuwa hufanya kila kitu pamoja  na hii inatuumiza na sababu hii ya kukaa pamoja ndio imepelekea kuota kuwa ni tabia mbaya kwa jamii ya kuvumilia uhalifu na sio wa rushwa pekee ni aina zote za uhalifu tunazivumilia,” alisema Mkurugenzi.

Alieleza kuwa kitu muhali kwenye jamii imekuwa chanzo kikubwa  kupelekea kuwepo na kuongezeka kwa wahalifu,ambapo hata Rais kipindi alipoingia madarakani na hadi sasa bado anazungumza kwa sauti kubwa kuhusu jamii iondokane na muhali ili kuondosha vitendo mbali mbali vya uhalifu.

“Kauli mbiu inasema kataa rushwa ni wajibu wako, kukataa Rushwa  ni haki yako kukataa, hivyo chukueni kauli mbiu ili muiambie jamii kukataa rushwa muhali,hiyo ni silka mbovu ipo kwa kila mtu, hivyo sisi kama wapelelezi silka hiyo ndio inayotuumiza na kuona uvivu kutoa hukumu ama hatua kwa kuogopa tu muhali sivyo,”alisema.

Hivyo aliwataka waandishi kufanya kazi zao kwa uwazi, ili kuisaidia jamii katika kupambana na rushwa muhali na uhujumu uchumi ili kuisaidia Serikali na jamii katika kupiga vita  suala hilo kwa ajili ya  maendeleo.

Akiwasilisha mada juu ya vyombo vya habari katika mapambano ya rushwa Ali Mbarouk Omar alisema kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikifanya juhudi mbali mbali kuhakikisha wanatoa elimu kwa taasisi mbali mbali wakiwemo waaandishi wa habari lengo ni kuona kwamba wanapiga hatua na kufikia lengo walilolikusudia.

“Kazi yenu  waandishi wa habari ni kuhakikisha elimu munayopatiwa munaifanyia kazi ipasavyo kwa kuelimisha jamii kupitia kalamu zenu, kuona munawajibika kila pembe kupambana na rushwa muhali na aina nyengine ya rushwa ili kusaidia jamii,”alisisitiza .

Aidha alifahamisha kuwa suala la kupambana na rushwa ni jukumu la kila mmoja na sio la mtu mmoja pekee ama taasisi husika, hivyo kuwepo na uwazi ili kupiga vita mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi.

Nae Fat-hiya Mussa Saidi mratibu wa Chama cha Waaandishi wa habari wanawake TAMWA Zanzibar Ofisi ya Pemba, alisema wakati akiwasilisha mada iliyozungumzia kuhusu rushwa na haki kwa wanawake katika nafasi za uongozi alisema zipo sababu nyingi zinazopelekea wanawake kukosa nafasi mbali mbali za uongozi.

Alifahamisha moja ya sababu hizo nimfumo dume ulioshika kasi, mila na desturi, dini,uelewa mdogo kwa wanajamii na uwepo wa rushwa muhali ambayo inawakatisha tamaa wanawake waliowengi kugombea nafasi za uongozi na kukatisha ndoto zao.

Mratibu huyo aliwataka waandishi wahabari pamoja na jamii kuondokana na silka hiyo ya rushwa muhali ili lengo liweze kufikiwa kwa maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake  Ofisa dhamana ZAECA Pemba Suleiman Ame Juma akifunga mafunzo hayo alisema jamii ikiwa na rushwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana, hivyo jamii ikubali kutoa mashirikiano na badala yake iondokane na rushwa muhali kwa maslahi ya taifa, pia kutoa wito kwa waandishi kutumia kalamu zao zitakazosaidia kuelimisha jamii katika kupiga vita na kupambana na rushwa muhali na uhujumu uchumi kwa maslahi ya taifa.

MWISHO.