Wednesday, January 1

SERIKALI kuendelea kupambana na fedha haramu

 

NA HANIFA SALIM, PEMBA

NAIBU Katibu Mkuu ofisi ya Rais fedha na mipango Zanzibar Aboud Hassan Mwinyi amesema, kwa kuzingatia madhara yatokanayo na utakasishaji wa fedha haramu nchi nyingi duniani zinachukua hatua za kupambana na uhalifu huo.

Alisema, utakasishaji wa fedha haramu unatokana kwa kiasi kikubwa na vitendo vya uhalifu kama vile rushwa, ukwepaji wa kodi, biashara za dawa za kulevya, uvuvi haramu, kughushi bidhaa, ujambazi, uuzaji haramu wa silaha, uharamia na magendo.

Aliyasema, hayo alipokua akifungua warsha ya siku tatu kwa wadau wa taasisi mbali mbali za serikali Kisiwani Pemba iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Rais fedha na mipango Gombani Chake chake.

Alieleza, ufadhili wa ugaidi na silaha za maangamizi hushamiri mahali ambapo kuna udhaifu wa kudhibiti vitendo vya utakasishaji wa fedha haramu ambapo hupelekea madhara makubwa kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Alifahamisha, madhara hayo ni kupungua kwa nguvu kazi ya taifa kutokana na vitendo vya ugaidi, serikali kushindwa kukamilisha miradi ya maendeleo, kushuka hadhi ya nchi kimataifa, kupungua wawekezaji, makundi ya uhalifu kuwa na nguvu za kiuchumi, kuhatarisha utawala wa sheria na usalama.

“Ni matumaini yangu warsha hii inaendeleza na kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya taasisi hizi katika kudhibiti uhalifu ukiwemo utakasishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na silaha za maangamizi,” alisema.

Hata hivyo alisema, kupambana na uhalifu kutaweza kufanikiwa endapo kila mdau atatekeleza majukumu yake mwenyewe ipaswavyo hivyo, aliwataka wadau hao kutoa mashirikiano ili kupambana na uhalifu wowote.

Kamishna wa kitengo cha kudhibiti fedha haramu Tanzania Fatma Ayoub Simba alisema, taasisi zilizoshiriki kwenye mafunzo hayo ni muhimu katika kudhibiti uhalifu ikiwemo utakasisaji wa fedha haramu nchini.

Aidha alisema, ni matarajio yake kwa wadau hao watakua na imani kushirikiana, kupambana na utakasishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi pamoja na uhalifu mwengine.

Alieleza, kulingana na tathmini ya mifumo ya nchi kupambana na fedha haramu kwa tathmini ya mwisho iliyofanywa mwaka 2019 na umoja wa kupambana na fedha haramu wa nchi za mashariki na kusini mwa Afrika ambapo Tanzania ni mwanachama udhaifu mbali mbali umebainika.

“Udhaifu uliobainika ikiwa ni pamoja na vyombo vyetu vya uchunguzi kutozingatia kufanya uchunguzi wa fedha haramu sambamba na kutozingatia upelelezi na uwendeshaji wa mashitaka kulingana na viashiria hatarishi vya utakasishaji fedha na wahalifu kutokunyang’anywa mali zitokanazo na uhalifu ipaswavyo,” alisema.

Nao washiriki wa mafunzo hayo Khairat Said Soud kutoka bodi ya mapato Zanzibar ZRB ofisi ya Pemba alisema, mafunzo hayo ni ya awali ni muhimu kwao kwani yatawasaidia kuelewa utakasishaji wa fedha haramu utanavoathiri mtu, taasisi, jamii na taifa kwa ujumla.

Nae Mkuu wa upelelezi Wilaya ya Wete ACP Fakih Yussuf Mohamed alisema, mafunzo hayo yatawasaidia kuwajengea uwezo na kuwaengezea uzoefu juu ya masuala ya kupambana na vitendo hivyo vya uhalifu wa fedha haramu.

Warsha hiyo imejuisha washiriki kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka, jeshi la polisi, mamlaka ya kuzuia rushwa, idara ya uhamiaji, tume ya kitaifa ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya, kikosi maalumu cha kuzuia magendo, mamlaka ya mapato na bodi ya mapato Tanzania TRA.

                                         MWISHO.