Sunday, December 29

CHAKUWAZA yaingia Pemba.

NA ABDI SULEIMAN.

CHAMA cha Kuwaendeleza wasanii Zanzibar (CHAKUWAZA), kimekutana na wasanii Mashairi na Tenzi Kisiwani Pemba, kwa lengo la kujenga umoja upendo na mshikamano ili kuhakikisha chama hicho kinasonga mbele.

Mwenyekiti wa CHAKUWAZA Zanzibar Wanimo Bakari Wanimo alisema lengo ni kukutana na wasanii wa Pemba, ni kujuwana na kuutambulisha uongozi mpyta baada ya kumalizika kwa uchakuzi wa Chama hicho.

Alisema CHAKUWAZA kimekuja kuwaweka pamoja wasaani wa mashairi na Tenzi, ili kuona sanaa yao inathaminiwa kama zilivyo sanaa nyengine.

“Sina budi kuwashukuru wajumbe wote, mulionipigia kura sasa nipo kwa ajili ya kuendeleza sanaa zaetu, changamoto zipo nyingi ila tusikate tama tuendelee kuwa wamoja”alisema.

Mwenyekiti huyo aliyaeleza hayo katika uwanja wa michezo Gombani, wakati wa kikao cha kwanza cha watunga mashairi na tenzi Unguja na Pemba.

Aidha alisema tokea ukoloni hilo ndio kongamano la kwanza kufanyika lililowakutanisha watu wa mashairi na tenzi Zanzibar, ili kuona wanaendeleza vipi sanaa zao.

Massoud Mbarouk aliwataka wasanii wenzake kujiongeza kwa kujifunza kwa wasanii wenzao wakongwe waliopo ndani nan je ya nchi, ili kupata baadhi ya istilahi mbali mbali nzuri zinazoweza kuvutia wasikilizaji.

“Tunapaswa kufungua na kusoma vitabu mbali mbali kama kile cha Shaban Robat, kina mambo mengi ya kujifunza ili kufikia ndoto zetu katika utunzi na ushairi”alisema.

Hassan Hamad Othman alisema fani ya ushairi ni mali na tunu inayopaswa kuendelezwa, hivyo CHAKUWAZA na serikali kupitia Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, kuhakikisha wanawaendeleza wasanii wa shairi na tenzi.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar (BASSFU), Dk.Omar Abdalla Adam alisema sanaa ni kipaji katika nchi nyingi Duniani hakuna vipaji vya sanaa kama vilivyopo Zanzibar.

Aliwataka wasanii hao kuhakikisha wanalinda na kutunza vipaji vyao, kwani sanaa inalipa iwapo wasanii wenyewe watapendana, kuwa wamoja na kuvumiliana katika kuhakikisha wanafikia malengo yao.

“Kipaji ni muhimu sana zipo harusi, kampenzi za siasa, huhitaji waimbaji wan a watunzi wa tenzi au mashairi, chamsingi kuwa kitu kimoja sio huyu anachukuliwa kwa elfu hamsini wengine elfu ishirini lazima tuwe kitu kimoja”alisema.

Aidha katibu huyo aliwataka wasanii hao, kuhakikisha wanajiamini na kushirikiana ili kuweza kufika mbali, katika kazi zao za sanaa sambamba kuandaa ratiba ya wasanii wa Pemba kukutana na wenzao wa Unguja.

Hata hivyo aliwasihi kutambua kuwa sanaa ni ajira, sanaa ni kazi kama zilivyo kazi nyengine, kuhakikisha wanalinda vipaji vyao ili kufikia mbali, mashairi yanabembeleza, mashairi yanaondosha stresi hivyo wanapaswa kuendeleza, ili nafasi ziendelee kubakia Zanzibar.

Katika hatua nyengine aliwasihii wasanii wa Pemba wanapaswa kupendana kuondosha chokochoko, fitna katika chama chao ili kufikia mbali.

Akisoma risala ya Chakuwaza Omar Ali Faki, kutoka Pemba alisema wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ukosefu wa Ofisi na wizi wa kazi zao .

Hata hivyo alisema katika kisiwa cha Pemba hakuna mtu wala taasisi wanyoweza kupeleka ombi la kuchapishiwa kitabu wakasikilizwa hivyo wamemuomba katibu mtendaji kuzipatia ufumbuzi changamoto zao.