Wednesday, January 1

Vijiji 409 Kisiwani Pemba vimeshapata huduma ya umeme.

NA ABDI SULEIMAN.

SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO) Tawi la Pemba, limesema kuwa jumala ya vijiji 409 sawa na 96.5%, tayari vimeshapatiwa huduma ya umeme wa uhakika Kisiwani Pemba.

Hayo yameelezwa na Afisa Uhusiano wa shirika hilo tawi la Pemba Amour Salum Massoud, wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha pamoja baina ya ZECO na masheha wa wilaya ya Chake Chake.

Alisema ni vijiji 15 sawa na 3.5% ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo kwa sasa, tayari mikakati mbali mbali imeshapangwa kuhakikisha vijiji hivyo vinapatiwa huduma hiyo ili suala la umeme liwe histori ndani ya kipindi hiki cha serikali ya awamu ya nane madarakani.

Alisema kwamujibu wa taakuwimu kutoka kwa Mtakuwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, ili kijiji kiweze kuitwa kijiji kinapaswa kuwa na kaya zisizopungua 80 hadi 120, hivyo ipo haja kwa masheha kuhakikisha wanavitafuta vijiji au vitongoji ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo.

“Kwa kiasi kikubwa hali ya usambazaji wa huduma ya umeme katika kisiwa cha Pemba, imefikia 96.5% jambo ambalo linatia moyo mkubwa katika huduma za umeme”alisema.

Akizungumzia suala la Changamoto, alisema ni hujuma zinazofanywa katika miundombinu ya umeme, ikiwemo kutiwa moto, kuchimbwa mchanga, nyaya za umeme kuangukiwa na miti, hali inayopelekea kulitia hasara shirika hilo.

Naye Afisa Mipango na utafiti ZECO Pemba Ali Faki Ali, alisema kwa mujibu wa Mtakuwimu Mkuu wa Serikali chake chake juma ya Vijiji 96 vimeshapatiwa umeme, huku mikakati wakiendelea katika maeneo madogo madogo ili kuendelea na mipango kwa ajili ya mwakani.

Alisema serikali imeingiza Bilioni 11 kwa ajili ya usambazaji wa Umeme, pamoja na shirika kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya huduma hizo.

Katibu Tawala Wilaya ya Chake Chake Omar Juma Ali, alisema adhama ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane (8), ni kusogeza huduma bora na muhimu kwa wananchi wake ikiwemo Maji, ELimu, Afya na Umeme ambayo ndio muhimu, huku Wilaya ya Chake Chake huduma ya umeme ikiwa inapatikana katika vijiji vyote.

Naye sheha wa shehia ya Ndagoni Massoud Ali Mohamed, alilitaka shirika la umeme Zanzibar ZECO Tawi la Pemba, kutokuwafumbia macho wanaoharibu miundombinu ya umeme, badala yake kuwachukulia hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

Alisema serikali imekua ikitumia fedha nyingi sana katika ukarabati wa huduma hizo pale zinapokosekana, hivyo ZECO inapaswa kuonyesha mfano kwa wale wanaoharibu miundombinu hiyo.