Wednesday, October 30

“Tutawadhibiti baadhi ya watu wakorofi wanaozitumia vibaya boda boda” RC Mattar

NA MWANDISHI WETU, PEMBA

MKUU wa Mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Masoud amesema, haridhishwi na matendo yanayofanywa na baadhi ya waendesha bodaboda ikiwemo ajali zitokanazo na uzembe.

Alisema kuwa, kuna baadhi yawandesha  boda boda hawafuati sheria za barabarani zilizowekwa jambo ambalo hupelekea kupoteza maisha ya watu kutokana na uzembe wao.

Aliyaeleza hayo katika hafla ya makabidhiano ya pikipiki zilizotolewa na bank ya CRDB kwa ajili ya jumuiya ya waendesha bodaboda Mkoani humo  iliyofanyika ukumbi wa baraza la Mji Chake chake.

“Mara kadhaa nimekuwa nikiwaambia jeshi la Polisi kama hawatoshi waseme tutaengeza vikosi vya SMZ vipo tayari kufanya kazi tushirikiane kuhakikisha tunawadhibiti baadhi ya watu wakorofi wanaozitumia vibaya boda boda,” alisema.

Alieleza inawezekana kwa Mkoa wa kusini kubaki salama bila ya ajali zinazopelekea kupoteza maisha ya watu endapo kila mmoja akifuata sheria, wajibu na taratibu zilizoekwa na nchi.

Aidha alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kwa dhati kabisa kuweza kuunga mkono na kuwasaidia wananchi hivyo aliwataka waendesha bodaboda kuamini kazi hiyo ni kama kazi nyengine ambayo inahitaji kuwekewa misingi na kusaidiwa kuendelea kwake.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya waendesha boda boda Mkoa wa kusini Pemba (PESBOA) Kassim Juma Khamis alisema, jumuiya yao ni ya mfano kwa Zanzibar hivyo, aliishauri mikoa mengine kuiga mfano wa jumuiya hiyo ili kulinda maisha ya wanachama wao na kuweza kujiletea maendeleo.

Kwa upande wake Meneja uhusiano na masuala ya Bima kutoka CRDB Bank Zanzibar Hamida Juma, alisema Bima ya bodaboda inaweza kumsaidia katika chombo ambacho amekichukulia mkopo baadae ikatokeza ajali Bima itamrudishia kwa kumpatia fedha kwa ajili ya kununua nyengine.

“Badala ya kuwa chombo umekikatia bima ndogo sasa itakuwa umerudishwa katika sehemu ile ile ambayo kabla hukupata ajali baada ya kufuata masharti unayotakiwa ikiwemo kuvaa kofia ngumu, abiria anatakiwa awe mmoja pia inapoungua utalipwa gharama za kununua nyengine hizi ni faida za bima,” alisema.

Mkuu wa usalama barabarani wa jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Shawwal Abdalla alisema, mkoa huo unaongoza kwa ajali nyingi na vifo Zanzibar zilizosababishwa na bodaboda ambapo mwezi Januari hadi Novemba jumla ya ajali 22 zimejitokeza ndani ya mwaka huu.

Akitoa nasaha kwa waendesha bodaboda hao Sheikh Khamis Salum alisema, Allah (S.W) katika kulinda maisha ya mwanadamu ameingiza kisasi kwa mtu atakaepoteza maisha ya mwenzake hivyo aliwataka waendesha bodaboda waitumie neema hiyo kwa kuzingatia sheria ili kuepusha vifo vya watu.

                                           MWISHO.