Wednesday, October 30

Benki ya Dunia yaunga mkono hatua ya serikali ya Tanzania kuwarejesha wasichana shuleni

Benki ya Dunia imeunga mkono tangazo la Serikali ya Tanzania la kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa elimu, vikiwemo vile ambavyo vimewazuia wasichana wajawazito au kina mama wachanga kuhudhuria shule katika mfumo rasmi.

Uamuzi huu muhimu unasisitiza dhamira ya nchi ya kusaidia wasichana na wanawake vijana na kuboresha nafasi zao za kupata elimu bora, ilisema taarifa ya benki hiyo.

Benki ya dunia imesema zaidi ya wasichana 120,000 huacha shule kila mwaka nchini Tanzania. 6,500 kati yao kwa sababu ni wajawazito au wana watoto.

”Benki ya Dunia inaunga mkono kwa dhati sera zinazohimiza elimu ya wasichana na zinazowezesha wanafunzi wote kusalia shuleni.

”Benki inatarajia kutoa miongozo itakayowawezesha wasichana wajawazito na kina mama vijana kuendelea na masomo na itasaidia utekelezaji wake kupitia ushirikiano wetu na Serikali ya Tanzania katika sekta ya elimu. Kuifanya elimu kuwa bora, salama, na kupatikana zaidi ni muhimu ili kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania.” ilisema taarifa hiyo.

Hapo jana Tanzania ilitangaza rasmi kuwaruhusu wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa kwasababu ya kupata ujauzito wakiwa shuleni kurejea masomoni kupitia mfumo rasmi.

Uamuzi huo umetangazwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia , Profesa Joyce Ndalichako alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kuhusu mafanikio ya wizara hiyo katika miaka 60 ya uhuru wa Taifa hilo.

Mbali na wanafunzi waliopata mimba, wanafunzi wengine waliokatiza masomo ya kwa sababu mbalimbali nao wataruhusiwa kurejea katika mfumo huo rasmi.

Mimba

CHANZO CHA PICHA,BROOKE FASANI AUCHINCLOSS

‘Takwimu za elimu zinaonesha kwamba wanafunzi wanaacha shule kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utoro, ujauzito, vifo pamoja na nidhamu, lakini sababu kubwa katika takwimu za utoro shuleni ambapo kwenye shule za msingi ni 100,008 ambapo wanafunzi watoro ni asilimia 93%, mimba ni asilimia ndogo tu, takribani asilimia 5% ya wanafunzi wanaoacha shule, alisema waziri Ndalichako.

Kwa mujibu wa Waziri Ndalichako wanafunzi watakaotaka kurejea shule wataruhusiwa kufanya hivyo ndani ya miaka miwili baada ya kuwa nje ya mfumo rasmi kwa utoro ama kukatiza masomo.

‘Yule ambaye matatizo yaliyomsababisha atoke shuleni yatakuwa yamekwisha na anataka kurudi shuleni serikali itampa nafasi na itakuwa ndani ya miaka miwili tangu alipoacha shule’, alisemaKwa mujibu wa Waziri Ndalichako wanafunzi watakaotaka kurejea shule wataruhusiwa kufanya hivyo ndani ya miaka miwili baada ya kuwa nje ya mfumo rasmi kwa utoro ama kukatiza masomo.

Tamko jipya la sasa la Serikali ya Tazanzania kuruhusu wanafunzi waliopata mimba na changamoto zingine kurejea masomoni linahitimisha marufuku iliyodumu kwa zaidi ya miaka minne iliyowekwa na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, hayati John Pombe Magufuli.

Juni 2017 Hayati Magufuli alipiga marufuku wanafunzi wanaopata mimba mashuleni kuendelea na masomo ya shule ya msingi na sekondari akisema ndani ya utawala wake hakuna mwanafunzi atakayepata mimba na kuruhusiwa kurudi shuleni.

Akazitaka taasisi zinazotetea utaratibu wa wanafunzi waliopata mimba kurudi shuleni, kufungua shule zao za wazazi lakini si kuilazimisha Serikali kufanya hivyo.

Kauli ya Magufuli ikazua mijadala na upinzani kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu nchini na nje ya nchi hiyo, wakiona hatua hiyo ni kumnyika haki ya kupata elimu mtoto wa kike.

Benki ya dunia ilipotangaza kuinyima mkopo Tanzania

Mwaka 2018 Benki ya dunia ilitangaza kuinyima mkopo wa dola milioni 500 nchi ya Tanzania, mkopo uliokuwa ukilenga kuboresha elimu nchini humo.

Moja ya sababu kuu za kuzuiliwa kwa mkopo huo ni uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuzuia wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua.

Katika taarifa rasmi iliyotumwa kwa barua pepe na moja ya wasemaji wakuu wa benki hiyo aliyopo jijini London, Benki hiyo ilisema inaendelea na majadiliano na serikali ya Tanzania kushusu suala hilo.

Hata hivyo benki hiyo baadaye iliahirisha mpango huo kutokana na mgawanyiko mkubwa wa maoni juu ya benki hiyo iidhinishe mkopo huo kwa Tanzania ama la.

Kwa mujibu wa nyaraka za Benki ya Dunia, pamoja na mambo mengine, mkopo huu ulikusudiwa kwenda kusaidia upatikanaji wa elimu bora na kwa urahisi kwa wanafunzi waliokuwa wanarudi shule baada ya kuwa wamepata ujauzito.

Kipengele hicho ndicho kilichozua utata kiliwasukuma wanaharakati wa Tanzania kuiandikia bodi ya utendaji ya Benki ya Dunia ikiwa benki hiyo itaipa Tanzania mkopo huo, kabla ya nchi hiyo haijaahidi kuondoa sera na kipengele cha sheria kinachowakataza wanafunzi wa kike kurudi shuleni baada ya kujifungua, basi benki itakuwa imekubaliana na sera na sheria hiyo ambayo wanaharakati waliita ya kibaguzi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la CNN la nchini Marekani, hakuna sababu rasmi iliyotolewa kuhusu kuahirishwa kwa kura hiyo japo inaripotiwa kuwa uongozi wa benki hiyo ulifanya kikao cha dharura na wanaharakati wa haki za binaadamu kutoka Tanzania na mashirika ya kimataifa.

Hatua ya sasa ya Tanzania imepokelewa vipi?

Kumekuwa na hisia mbalimbali kuhusu hatua ya sasa ya serikali ya Tanzania, wengi wakiunga mkono huku wengine wakieleza umuhimu wa suala hili kuwepo sheria.

Wasichana wenyewe wameipokea kwa furaha hatua hii kama huyu aliyewahi kukatisha masomo yake ambaye sasa amefikia elimu ya chuo kikuu.

Ngayo, ni jina la kubuni alipita kwenye changamoto hiyo alipoolewa akiwa na umri mdogo wa miaka 13 na kuacha shule ingawa alifaulu kwenda kidato cha kwanza.

Ngayo amefurahi kwa hatua aliyoifikia baada ya kupata elimu na kuweza kutimiza ndoto zake.

kwa hisani ya BBC.