Siku mojo baada ya Mahakama ya juu zaidi nchini India kupitisha hukumu ambayo ilimuondolea hatia mtu aliyemnyanyasa kingono mtoto wa kike wa miaka kwa sababu “hakukuwa na mgusano wa ngozi kwa ngozi” na mwathiriwa, hukumu nyingine iliyopunguza kifungo cha jela kwa mwanamume aliyepatikana na hatia ya kumdhalilisha kingono mvulana wa miaka 10 imesababisha hasira.
Amri hiyo, ambayo ilitangulia uamuzi wa kihistoria wa Mahakama ya Juu kwa siku moja lakini sasa imeripotiwa, ilitangazwa na mahakama kuu ya Allahabad katika jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh.
Uhalifu huo ambao ulifanyika mwaka wa 2016 wakati mwanamume huyo alipotembelea nyumba ya mtoto huyo na kumpeleka katika hekalu la eneo hilo ambako alimdhalilisha kingono.
Alikuwa amempatia mtoto huyo rupi 20 sawa na ( senti 27) ili kumnyamazisha asizungumzie unyanyasaji huona kumtishia endapo atatoa taarifa ya kile kilichotokea.
Kesi iliyowasilishwa mahakamani mnamo Agosti 2018 ilimpata mwanamume huyo na hatia ya “unyanyasaji wa kingono uliokithiri” chini ya Sheria kali ya Pocso (Ulinzi wa Watoto dhidi ya Makosa ya Kujamiiana) na kumhukumu kifungo cha miaka 10 jela.
Mwanamume huyo alikata rufaa na wiki iliyopita, jaji wa mahakama kuu alipunguza kifungo chake hadi miaka saba, akisema kuwa chini ya sheria, shambulio hilo “halikuwa mbaya zaidi” – ikimaanisha kuwa uhalifu haukuwa mkubwa kuliko vile mahakama ya kesi ilivyofikiria kuwa.
Wataalamu wa sheria wametilia shaka hukumu hiyo, wakisema kuna mambo kadhaa katika Sheria ya Pocso ambayo yanafanya shambulio “kuwa mbaya zaidi”, mojawapo ikiwa ni kama mwathiriwa ana umri wa chini ya miaka 12.
Lakini agizo hilo limezua ghadhabu nchini India huku wengi wakijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kuikosoa.
Wengi walidokeza kuwa ni wiki jana tu ambapo Mahakama ya Juu, ilitupilia mbali amri ya mahakama kuu ya Mumbai ya ”ngozi kwa ngozi kutogusana”, ikiisema kwamba majaji wanapaswa kuzingatia “nia ya ngono” na sio maelezo ya kitendo hicho.
Mtumiaji mmoja wa Twitter alielezea agizo hilo kuwa la “kuudhi na la ajabu”; mwingine aliandika kwamba “hakuna kiasi cha adhabu kinachoweza kufuta kiwewe cha mvulana huyo mdogo”; na baadhi ya wengine walijiuliza “hakimu alikuwa na shida gani?”
Mbunge Mahua Moitra alikuwa miongoni mwa waliotuma ujumbe kwenye Twitter akionyesha hasira yake kutokana na agizo hilo:
“Mahakama Kuu Amkani- Pocso ilikusudiwa kuwaokoa watoto kutokana na makosa mabaya zaidi. Usiipunguze,” aliandika.
India ina idadi kubwa zaidi ya watoto wanaonyanyaswa kingono duniani huku maelfu ya visa vikiripotiwa kila mwaka.
Mwaka jana, Ofisi ya Kitaifa ya Rekodi za Uhalifu ilisajili makosa 43,000 chini ya Sheria ya Pocso – hiyo ni wastani wa kesi moja kila baada ya dakika 12.
Mwaka 2007, utafiti wa wizara ya wanawake na ustawi wa watoto uligundua kuwa zaidi ya 53% ya karibu watoto 12,300 waliohojiwa waliripoti aina moja au zaidi ya unyanyasaji wa kijinsia.
Utafiti huo umebaini kuwa kinyume na imani ya jumla kwamba wasichana pekee ndio walinyanyaswa, wavulana walikuwa katika hatari sawa – labda zaidi ya 53% ya wale waliosema kuwa wahasiriwa walikuwa wanaume.
Na polisi wanasema kuwa katika zaidi ya 90% ya kesi, wanyanyasaji wanajulikana na mhasiriwa – sawa na kesi ya mvulana wa miaka 10.
Anuja Gupta, ambaye amekuwa akishughulikia suala la unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, haswa unyanyasaji wa kingono, kwa robo karne, anasema idadi rasmi hajulikani kwani kesi nyingi hata haziripotiwi.
“Unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto unaitwa janga la kimya. Liko kila mahali. Inatokea katika kila nyumba ya pili na vizazi,” anasema.
“Lakini kuna unyanyapaa na kusitasita kwa ujumla kuzungumzia mada hiyo kwa kuwa wengi wa wanaonyanyasa ni watu wa karibu wa familia, watu wakiwemo walionusurika wanasema watasuluhisha ndani ya familia hivyo kwa kila kesi inayofika mahakamani, mamia hawafanyi hivyo.
CHANZO CHA HABARI BBC