NA ABDI SULEIMAN.
KAMATI ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, imewataka wataalamu wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar, kutokuendelea kuianguza Serikali pale wanapoamua kupitia utaalamu wao katika ujenzi wa barabara nchini.
Kamati hiyo imesema Wizara hiyo imekua na wataalamu wengi, lakini wanashindwa kuisaidia serikali pale wanapofanya tafiti zao, ili kuepuka kuingia hasara mara mbili zaidi inapoanza miradi ya maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Yahya Rashid Abdulla, mara baada ya kukagua barabara ya Kipapo-Mgelema-Wambaa yenye urefu wa KM 9.3, wakati wa ziara ya kamati hiyo Kisiwani Pemba.
Alisema chakusikitisha wataalamu wanashindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu, katika kuishauri serikali ili isiweze kuingia hasara mara mbili pale mradi unapotaka kufelishwa.
“Hebu angalieni wataalamu wa sera na utafiti mulikuwa wapi muda wote barabara inaanza mpaka inafika hapa, leo ndio munatupa ushari kwamba munataka kuipitisha upande mwengine, hii harasa marambili isingetokea”alisema.
“Serikali ina waamini ndio ikatoa mawazo hayo, lakini vitu vinaonekana vinabadilika na haviko sawa, ila mutambuwe kuwa wananchi bado wanaimani na serikali yao hii ya awamu ya nane”alisema.
Aidha Mwenyekiti huyo aliushauri uongozi wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, kusimamia miradi ipasavyo kasi iliyopo hairidhishi, hivyo kila mtu kwa nafasi yake anapaswa kujituma na kujitambua.
Mjumbe wa kamati hiyo Mussa Fumu Mussa alisema suala la kuchelewa kutokukamilika kwa barabara hiyo sio la hivi sasa, ni lakipindi kirefu kwani awamu waliokuja barabara ilikuwa sehemu hiyo hiyo imeishia.
Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa barabara Zanzibar Injinia Mbarouk Juma Mbarouk, alisema utekelezaji wa barabara ya Kipapo hadi Mgelema awamu ya kwanza 5.5KM umefikia 70% na awamu ya pili Mgelema hadi Wambaa 3.8KM umefikia 10%.
Alisema mradi huo umetengewa kutumia shilingi Bilion 5,523,454,420/=, hadi kufikia Julai 30 Jumla ya shilingi 900 zimershaingiwa.
Akizungumzia mtambo wa Lami Kwareni, injia Mbarouk alisema kwa sasa mtambo huo umekua mkongwe sana na kutokana na mabadiliko ya Teknolojia, ipo haja ya kupatikana kwa mtambo wa kisasa ambao utawezesha kwenda na wakati huo.
Afisa Mdhamini wa Wizara hiyo Ibrahim Saleh Juma, aliishukuru kamati hiyo kwa ushauri wake katika kuhakikisha wizara hiyo inakuwa bora nchini, pamoja na kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yato yaliotolewa kwa lengo la kuleta ufanisi katika kazi.