Sunday, November 24

Ralf Rangnick: Mfahamu raia wa Ujerumani anayetarajiwa kuchukua mikoba ya ukufunzi Manchester United

Maelezo ya picha,Ralf Rangnick:

Manchester United inakaribia kumteua Ralf Rangnick kuwa meneja wao wa muda mfupi kwa mkataba wa miezi sita.

Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 63 anatarajiwa kujiunga na United lakini hataiongoza timu hiyo katika mchezo wa mwishoni mwa wiki dhidi ya Chelsea, wakati huu akisubiri kibali chake cha kazi.

United wameshamalizana na Rangnick, lakini hawajamalizana na Lokomotiv Moscow, ambako Mjerumani huyo anafanya kazi kama Mkuu wa masuala ya michezo na maendeleo.

 

Rangnick anatua baada ya United kumfukuza kazi Ole Gunnar Solskjaer Jumapili iliyopita kufuatia kuiongoza timu hiyo miaka mitatu bila kombe.

Rangnick alishinda kombe la Ujerumani akiwa na Schalke mwaka 2011 na kuipeleka RB Leipzig katika fainali ya kombe hilo mwaka 2019.

Katika msimu wa 2010-11 aliiongoza Schalke kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo walipoteza kwa jumla ya mabao 6-1 didi ya united, ambao na wao walikuja kuchapwa na Barcelona katika fainali.

United kwa sasa ni ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu ya England na Solskjaer, ambaye aliifungia bao la ushindi Man United katika fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1999, alifukuzwa baada ya kipigo cha aibu cha 4-1 kutoka kwa Watford Siku ya Jumamosi.

Michael Carrick, msaidizi wa Solskjaer, anaiongoza timu hiyo kwa muda, huku United ikisema atakuwa katika nafasi hiyo wakati ikijaribu kusaka meneja wa mpito hadi mwisho wa msimu huu.

Carrick aliiongoza United siku ya Jumanne kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Villarreal, matokeo ambayo yameihakikisha United kumaliza kileleni mwa kundi lao la Ligi ya Mabingwa.

Rangnick amejijengea heshima kwenye ukocha wakati wake akiviongoza vilabu vya Ujerumani hasa akiwa na Stuttgart, Hannover, Hoffenheim, Schalke na RB Leipzig.

Baadaye alikuwa meneja wa vilabu vya Red Bull na klabu yake ya sasa ya Lokomotiv ina mchezo wa Europa League dhidi ya Lazio Alhamisi jioni na isingependa United kvuruga maandalizi yao.

Rangnick alivutiwa na mazungumzo ya awali na maafisa wa United mapema wiki hii. Hata hivyo, amekuwa na majadiliano zaidi kuhusu jukumu lake zaidi baada ya msimu kumalizika.

Viongozi waandamizi wa United wanaamini utaalamu wa Rangnick utakuwa muhimu sana kutokana na mtazamo wa kiufundi na mfumo.

Hatua hiyo ya Old Trafford kumleta meneja wa mpito hadi mwisho wa msimu itawapa nafasi ya kufanya tathmini ya kutosha kuhusu meneja mpya wa kudumu anayefaa.

Mauricio Pochettino anajulikana kuvutiwa na kazi ya United lakini klabu hiyo ya Ligi Kuu England ina wasiwasi wa kuingia katika majadiliano ya muda mrefu na PSG ambayo yanaweza kuchukua muda mrefu kuliko wanavyotaka.

Inafahamika kuwa Carrick atakuwa kwenye behci kuiongoza United Jumapili dhidi ya Chelsea katika uwanja wa Stamford Bridge.

Mlinzi wa zamani wa Ujerumani Lutz Pfannenstiel alifanya kazi kwa muda mfupi na Rangnick huko Hoffenheim na anaamini kuwasili kwake Old Trafford kutakuwa na manufaa kwa United.

“Ralf Rangnick ni mtaalamu mkubwa, kwa kweli ni mmoja wa makocha bora au mameneja waliozalishwa Ujerumani katika miaka 15-20 iliyopita,” alisema Pfannenstiel, ambaye ni mkurugenzi wa michezo wa St Louis City SC.

Ole Gunnar Solksjaer

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Ole Gunnar Solksjaer

“Kila kitu alichofanya hadi sasa kilikuwa na mafanikio na kila wakati alikuwa wazi kwamba kama atapata fursa ya kufanya kazi katika klabu kubwa nchini Uingereza, anataka kufanya hivyo.

“Kwa hivyo ukiangalia kocha huyu wa mpito, nadhani yeye ndiye anayeweza kuweka mambo sawa ili kuirudisha Manchester United kwenye njia yake. Nadhani alikuwa mtu bora kwenye soko.

“Tunapenda kumwita nchini Ujerumani, profesa wa mpira wa miguu, kila kitu anachokifanya kinatazamwa vizuri, jinsi anavyoweka mifumo ya klabu katika kila klabu ni jambo la kushangaza.”

CHANZO CHA HABARI BBC