Wednesday, October 30

Sera na Sheria zinazotungwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu zinapaswa kutekelezwa kwa vitendo.

 

Na, Hassan Msellem, Pemba.

Wadau wa watu wenye ulemavu kisiwani Pemba wameomb Sera na Sheria zinazotungwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu zinapaswa kutekelezwa kwa vitendo ili watu wenye ulemavu waweze kupata haki zao za msingi ikiwemo Matibabu, Elimu pamoja na ajira.

Ombi hilo limetolewa na wadau mbali mbali wakati wakichangia mada juu ya rasimu ya Sera kwa watu wenye ulemavu mkutano uliofanyika Wawi Ukumbi wa Makonyo Kisiwani Pemba, wamesema baadhi ya Sera na Sheria zimeshapitwa na wakati sambamba na kutokutekelezeka, hivyo basi wameombwa kutunga Sera na Sheria kutunga Sera na Shehia zitakazoweza kuwasaidia watu wenye ulemavu pamoja na kutekelezwa kwa vitendo.

Akiwasilisha mada juu ya rasimu hiyo afisa Sera kutoka ofisi ya makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Bi. Sabra Ali Mohammed amesema Sheria ya watu wenye ulemavu ya namba 9 ya mwaka 2006 imefanikiwa kwa kiasi kikukbwa katika utekelezaji wake licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza ambapo zikirekebishwa zitaongeza ufanisi juu ya masuala ya watu wenye ulemavu.

‘’moja ya Sera ambayo imeibuka inasema kwamba uratibu usiotosheleza wa taasisi juu ya masuala ya watu wenye ulemavu, utekelezaji dhaifu pamoja na kupoitwa na wakati kwa Sheria ya watu wenye ulemavu namba 9 mwaka 2006’’ alisema

Aidha amesema matokeo ya Sheria ya mwaka 2006 yamebainisha kuwepo kwa mapungufu kadhaa katika Sheria Kisera, mikataba ya kimataifa pamoja na muundo na mamlaka.

Kwa upande wake mwanasheria kutoka ofisi ya makamu wa kwanza wa rais Hajra Idrissa Haji amesema kutungwa kwa Sheria mpya ya watu wenye ulemavu inadhamiria kufuta Sheria namba 9 ya mwaka 2006 kwa lengo la kuimarisha mfumo  wa kisheria utakaowezesha kufikia lengo la kuwa na dira ya kuwa na jamii jumuishi ambayo inahusisha watu wenye ulemavu katika kuimarisha haki na ustawi wa watu wenye ulemavu nchini.

Nae mkurugenzi wa baraza la watu wenye ulemavu Zanzibar Ussy Khamis Debe amesema miongoni mwa changamoto zinazoikabili Sheria za watu wenye ulemavu ni Utekalezaji wa Sera na Sheria jambo ambalo linapelekea watu wenye ulemavu kukosa haki zao za msingi licha ya uwepo wa Sheria hizo.

        ‘’watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi na tukiangalia historia ya watu wenye ulemavu tulikotokea mpaka hapa ambapo tumefikia sasa hivi ni mafanikio ispokuwa changamoto ambayo tunakumbana nayo ni kwenye utekelezaji’’ alisema

Ali Khamis Kombo ni afisa wa elimu mjumuisho kutoka kitengo cha elimu mjumuisho Zanzibar, amesema suala la ajira kwa watu wenye ulemavu bado halijatekelezwa kwa vitendo kwani amesema tafiti zilizofanyika katika taasisi kadhaa za Serikali zinaonesha hakuna watu wenye ulemavu ambao wameajiriwa katika taasisi hizo licha ya kuwa na vigezo vya kuweza kuajiriwa.

        ‘’Mimi mwenyewe nimefanya research kwenye Wizara tatu ya makamu wa kwanza wa rais, makamu wa pili wa rais pamoja na Wizara ya elimu lakini sikukuta hata mtu mmoja mwenye ulemavu ambaye amajiriwa kwa upande wa Pemba’’ alisema

Mussa Seif Mussa ni afisa wa watu wenye ulemavu Mkoa wa Kusini Pemba amependekeza kutungwa kwa Sheria itakayobaisha kutengwa kwa kiwango cha fedha kwa ajili ya matibabu kwa watu wenye ulemavu ili waweze kupata haki yao ya msingi ya matibabu.

        ‘’moja miongoni mwa changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu ni ukosefu wa matibabu kwahivyo tunataka kuwepo kwa sheria ya fedha za matibabu kwa watu wenye ulemavu maana kwakweli watu wenye ulemavu wanahangaika sana kutafuta matibabu’’ alisisitiza

Said Rashid Hassan ni mwanasheria kutoka kituo cha huduma za Sheria Pemba ameziomba mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa watakaokutwa na hatia ya kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji watu wenye ulemavu kwani kuongezeka kwa vitendo hivyo kunazidi kuwadhalilisha watu wenye ulemavu nchini.

Mkutano huo umejumuisha makundi mbali mbali ikiwemo watu wenye ulemavu, watendaji wa Serikali pamoja na watendaji kutoka taasisi binafsi ukiwa na lengo la kujadili rasimu ya Sera mpya ya watu wenye ul\mavu visiwani Zanzibar umeandaliwa na baraza la taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar ikiwa ni sehemu ya shamra shamra kuelekea siku ya watu wenye ulemavu duniani Decemba 3 ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema “uongozi na
Ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu, kuelekea ujumuishwaji na ufikiwaji endelevu baada ya Uviko-19 Duniani.”