Sunday, November 24

JET yatoa elimu ya uhifadhi , maliasili kwa waandishi wa habari Tanzania

NA ABDI SULEIMAN.

MWENYEKITI wa Chama cha Waandishi wa habari za Mazingira Tanzania, (JET) Dr.Ellen Otaru, amesema kazi kubwa iliyopo ni kutoa elimu na ushirikishwaji wa vijana na wanawake, katika ulinzi na uhifadhi wa mazingira na maliasili kwa maendeleo endelevu.

Alisema matumizi mabaya ya mazingira hupelekea wanyama na viumbe mbali mbali kupotea na baadhi yao kufariki, hayo yanatokana na matumizi mabaya ya mazingira yanayofanywa na binaadamu.

Akizungumza katika mkutano uliowashirikisha waandishi wa habari za uhifadhi, uwindaji haramu wa wanyamapori na usafirishaji, kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET).

Alisema asilimia 40% ya watanzania ni Vijana ndio tegemeo la taifa, huku miundombinu ya makaazi, barabara yakiongezeka, lakini ardhi bado inaendelea kubakia vile vile hali inayopelekea kugusa maeneo ya uhifadhi maliasili, hivyo ipo haja ya kuangaliwa kwa mipango miji na kuwepo kwa maeneo maalumu ya uhifadhi.

Hata hivyo Dr.Ellen aliwataka waandishi wa habari katika kuandika habari zao kutumia takwimu, kwani habari hizo ndizo zinazoendana na wakati uliopo hivi sasa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa JET John Chikomo, alisema Waandishi wananafasi ya kutumia makundi maalumu, wakati wa kuandika habari zao, ili kuona yanapotokea matukio ya uwindaji haramu wanaepukana nayo.

Alisema lengo la mafunzo ni kuwajengea Uwezo wanahabari wa kusimamia na kuandika habari za Uhifadhi, uwindaji haramu na usafirishaji wa wanyamapori, ili jamii iweze kufahamu changamoto kubwa inayoikumba sekta ya uhifadhi wa malia asili.

Kwa upande wake mtaalamu kutoka mradi wa USAID Tihifadhi Maliasili, hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alisema suala la uhifadhi linachukua njia nyengine kutokana na mabadiliko ya tabianchi nchini.

Alisema mradi umejikita zaidi katika kulinda shuruba za wanamapori, pampoja na misitu na viumbe vya baharini na kujengea uwezo sekta binafsi ili kufikia malengo yake.

Kwa upande wake afisa mwengine kutoka mradi huo wa Tuhifadhi Maliasili, ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema dunia inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi, vizuri kufanywa mipango mizuri ya ardhi, ili kupunguza migogoro inayotokea baina ya binaadamu na wanyama katika maeneo ya jamii.

“Ipo haja tukaamua kuendeleza kupanda miti kwa wingi, ili kuweza kurudisha uoto wa asili ambao umepotea kutokana na matumizi mabaya ya ardhi yanayofanywa na binaadamu”alisema.

Hata hivyo alisema zipo sehemu ambazo ukame unatokea na wanyama kufariki kutokanana maji kuchukuliwa na kutumiwa katika shuhuli nyengine, kama vile kilimo hali inayopelekea kupoteza hata viumbe hai.

Nao waandishi wa habari za uhifadhi, uwindaji haramu wa wanyamapori na usafirishaji, wameushukuru mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, pamoja na Chama Cha waandishi wa habari za mazingira Tanzania kwa kupatia mafunzo hayo, ambayo yameweza kuwaongezea uwelewa juu ya suala la uhifadhi wa nyamapori.

MWISHO