Sunday, November 24

NMB yakabidhi bima ya mkono wa pole kwa vikundi Pemba

 

NA ABDI SULEIMAN.

BENK ya NMB kwa kushirikiana na Metropolitan Life Tanzania, kwa mara ya kwanza imekabidhi bima ya mkono wa pole kwa vikundi, kufuatia kifo cha mmoja ya wanachama wa kikundi cha Umoja ni Nguvu kilichoko Mvumoni Wilaya ya Chake Chake.

Bima hiyo ya mkono wa pole ambayo hukatwa kwa vikundi, na pale mwanachama wa kikundi anapofariki Benk hiyo hukabidhi ubani, kwa wanakikundi ili kufidia shuhuli za mazishi.

Hayo yameelezwa na meneja wa Benk ya NMB Tawi la Pemba Hamad Mussa Msafiri, wakati wa hafla ya kukabidhi ubani wa shilingi Milioni tatu kwa kikundi cha Umoja ni Nguvu kukata bima ya Silver, hafla iliyofanyika mjini Chake Chake.

Alisema kikundi hicho kimekua cha mfano baada ya kukata bila ya Silver, huku akiwapongeza kwa kukubali kwao kukata bima hiyo na kuwa mfano kwa vikundi vyengine.

“Umoja ni Nguvu kimekua ni kikundi cha kwanza katika kuwapatia bima ya mkono wa pole kwa vikundi, hili linapelekea kuwaaminisha wananchi kama bima zetu zipo sahihi na sio utani”alisema.

Kwa upande wake afisa Mahusiano Mohamed Abdalla, bima ya mkono wa pole zipo aina tatu ambazo kikundi hupaswa kuchagua bima ipi inaweza kukata, ikiwemo bima ya Bronze, bima ya Silver na Bima ya Gold.

Aidha alitaja bima hizo kuwa hazina mashart ispokua kikundi kinapaswa kuwa na watu watano, bronze akifariki mwanachama hukabidhi kikundi Milioni moja, Silver hukabidhi kikundi Milioni tatu na Gold hukabidhiwa kikundi Milioni tano.

“bronze mwanachama huweka shilingi 500 kwa mwaka hulipa elfu 6000 na kwatu watano wa kikundi wanalipa elfu 30,000 kikundi, upande wa Silver mwanakikundi analipa 1200 kwa miezi mwaka hulipa 14400 kwa watu watano hulipa 72000, nayo bima Gold mwanakikundi huchangia 2000 kwa mwaka 24000 kwa watu watano 120,000.”alisema.

aidha akishuhudia makabidhiano ya fedha hizo kwa kikundi cha Umoja ni Nguvu, sheha wa shehia ya Mvumoni Ali Khamis Massoud, aliishukuru benk ya NMB kwa kutekeleza ahadi yake kwa vitendo kwa kikundi hicho baada ya kuondokewa na mmoja wa wanachama wao.

Hata hivyo aliwataka wanavikundi wengine kujitokeza kukata bima ya vikundi, ili kuweza kunufaika na bima hiyo pale mmoja wa wanakikundi anapoondoka duniani.

MWISHO