Sunday, November 24

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Baraza la Wazee wa CCM.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui  Zanzibar Bi. Khadija Jabir,akiwa na Ujumbe wake walipofika Ikulu kwa mazungumzo na kumpongeza, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 1-12-2021

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akifuatilia taarifa wa Baraza la Wazee wa CCM Afisi Kuu Kisiwandui Zanzibar,ikiwasilishwa na Katibu wa Wazee wa CCM.Bw.Haji Machano, wakati wa mkutano wao uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi Afisi Kuu Kisiwandui Zanzibar, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo Bi. Khadija Jabir (kulia kwa Rais) walipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi Afisi Kuu Kisiwandui Zanzibar, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo Bi. Khadija Jabir (kulia kwa Rais) walipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Mjumbe wa Baraza la Wazee wa CCM Bw.Khatib Ramadhan Iddi, baada ya kumalizika kwa mazungumzo na Ujumbe wa Baraza la Wazee wa CCM Afisi Kuu Kisiwandui Zanzibar,yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapindsuzi Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, baada ya kumaliza kwa mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 1-12-2021

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kwamba Serikali anayoiongoza  ina lengo la kuhakikisha inajenga uchumi imara utakaoleta maendeleo kwa wananchi wote.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Viongozi pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar,waliofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kumpongeza.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba siasa ni uchumi na siasa ikiwa nzuri na uchumi nao huimarika, hivyo juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kuhakikisha kunajengwa uchumi ulio imara na madhubuti.

Aidha, Rais Dk. Miwnyi aliwaeleza wazee hao mipango na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Nane katika kuimarisha sekta za maendeleo ili kuhakikisha uchumi unazidi kuimarika pamoja na vijana kupata ajira  na Serikali nayo kupata mapato.

Alisema kuwa jambo kubwa na la msingi katika kuhakikisha Zanzibar inaendelea kupata maendeleo na kuujenga uchumi wake kuwa imara ni kuwepo kwa amani na utulivu, juhudi ambazo zimechukuliwa katika kuhakikisha hilo linafanyika.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kulipongeza Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar, kwa kuendeleza utamaduni wao wa kukutanan na kiongozi aliyoko madarakani kwa azma ile ile ya kuzungumza na kubadilishana mawazo.

Alitoa shukurani kwa dua wanazozifanya wazee hao mara kwa mara kwa viongozi wao na kwa nchi yao na kuwasisitiza haja ya kuendelezwa kwa utaratibu huo.

Dk. Mwinyi pia, aliwaeleza wazee hao juhudi zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza za kuhakikisha jengo la kihistoria la Beit al Jaib linajengwa upya na kurudi katika hadhi yake ya asili ujenzi ambao unatarajiwa kuanza rasmi hapo Febuari mwakani.

Pia, Rais alieleza hatua za Serikali katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika ikiwa ni pamoja na kuanzisha huduma za Bima ya Afya ili iwe rahisi kupatikana kwa huduma za afya.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja na umuhimu wa kuijenga upya nyumba ya Kijangwani iliyokuwa Afisi ya ASP ambayo kwa sasa imebomoka kwa azma ya kuhakikisha historia haipotei.

Mapema akisoma Tamko la  Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar, Mzee Haji Machano alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2020 pamoja na ushiriki kabambe wa kampeni alizozifanya za uchaguzi huo.

Baraza hilo lilieleza kufarajika na kazi aliyoanza kuifanya wakati alipoingia madarakani kwani uongozi wake wameifurahia ikiwa ni pamoja na kuzunguka katika Wilaya zote za Unguja na Pemba na kukagua maendeleo pamoja na kukutana na wananchi ambao walipata fursa ya kueleza matatizo wanayoyakabili.

Pamoja na hayo, Baraza hilo lilimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake anazozichukua katika kuiongoza Zanzibar na kuiweka katika hali ya usalama, amani na utulivu.

“Umekemea  rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, umerekebisha mfumo mzima wa elimu na kukarabati utawala, umekemea ubakaji, udhalilishaji wa watoto na wanawake, umechukizwa sana na uingizaji na utumiaji dawa za kulevya nchini na umeunda chombo cha udhibiti na ufuatiliaji, umepanua uchumi wa buluu na kuiweka Wizara maalum ya shughuli hizo, umewaita wawekezaji”,alisema sehemu ya Tamko hilo.

Aidha, Baraza hilo lilitoa ushauri kwa Rais Dk. Mwinyi ikiwa ni pamoja na kushauri kwa kujengwa nyumba ya ASP, iliyopo kijangwani ambayo ina historia kubwa pia, walishauri  kujengwa kwa jengo la Bait el Jaib, kuongeza kasi ya kupiga vita vitendo vya ukatili, ubakaji, udhalilishaji wa watoto na wanawake, uingizwaji wa dawa za kulevya pamoja na kupambana na maradhi ya miripuko.