Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa katika juhudi za kupambana na UKIMWI, bado janga hilo linabaki kuwa tishio kwa ustawi wa maisha ya watu na maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, iliyofanyika katika Kijiji cha Kidimni Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema kuwa ingawa Zanzibar imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kufikia malengo ya kudhibiti UKIMWI, ikiwemo kiwango cha chini ya asilimia moja (1%) ya maambukizi hapa visiwani, uchambuzi wa takwimu mbali mbali unaonyesha kwamba bado kuna baadhi ya makundi hayajaweza kufikiwa ipasavyo na huduma zinazotolewa.
Mheshimiwa Othman amebainisha kuwa wanawake katika visiwa vya Unguja na Pemba wanaonekana kufanya vyema katika kuzifikia na kuzitumia huduma zikiwemo za ushauri nasaha, upimaji wa Virusi vya UKIMWI (VVU) na kuvipunguza mwilini, na pia matumizi ya dawa za kupunguza makali ya virusi (ARV).
Akifafanua baadhi ya takwimu, Mheshimiwa Othman amesema, “katika watu 166,566 waliopatiwa huduma za ushauri nasaha na uchunguzi wa VVU kati ya Januari hadi Septemba mwaka huu hapa Zanzibar, wengi wao walikuwa ni wanawake ambao ni idadi ya 86,947 ukilinganisha na 79,619 idadi ya wanaume, aidha kati ya watu 7,481 wanaotumia dawa za ARVs hadi kufikia Septemba mwaka huu, 5,170 ni wanawake ukilinganisha na idadi ya wanaume 2,427 ambapo tofauti hizi zina athari kubwa katika kudhibiti maambukizi ya VVU na kulimaliza janga la UKIMWI”.
Akieleza changamoto mbali mbali katika kukabiliana na janga hilo, zikiwemo za unyanyapaa na kushindwa kujielewa kwa baadhi ya makundi-athirika, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dokta Saada Salum Mkuya, amesema kuwa kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI ya Zanzibar, Serikali itahakikisha inaandaa mbinu mbadala ili ifikapo mwaka 2030, yasiwepo maambukizi mapya hapa Visiwani.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Bw. Rashid Hadid, amesema kuwa hadi kufikia maadhimisho ya mwaka huu, bado idadi ya maambukizi ya UKIMWI katika mkoa wake inabaki kuwa kubwa, kulinganisha na mikoa mingine ya Zanzibar, kutokana na kukithiri kwa vituo vya ulevi, mabaa, kumbi za starehe na uwepo wa kiasi kikubwa cha vitendo vya ngono-zembe.
Harakati za maadhimisho ya siku hii hulenga zaidi katika kuongeza uelewa kwa jamii juu ya maradhi ya UKIMWI, kuishajihisha jamii kujiepusha na mambo ambayo yanachangia maambukizo ya VVU, kueleza mafanikio, changamoto na mikakati itakayosaidia katika kulidhibiti janga hili, kuwafariji, kuonyesha mshikamano kwa watu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI, na kuwakumbuka wale waliopoteza maisha yao kutokana na balaa hilo.
Maadhimimisho ya mwaka huu ya Siku ya UKIMWI Duniani, inayoadhimishwa kila ifikapo Disemba 1, yamechukua kauli mbiu inayosema “TUWEKE USAWA KUMALIZA UKIMWI NA MAJANGA MENGINE”, ikiwa ni msisitizo katika kuweka usawa wa upatikanaji wa huduma za kinga na tiba kwa watu wote.
Viongozi mbali mbali wa Serikali na Kijamii, Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, Wadau wa Maendeleo na Asasi za Kiraia, wamejumuika katika hafla hiyo, ambao ni pamoja na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Khamis Hamza Chilo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dokta Omar Dadi Shajak, Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja, Bi Marina Joel Thomas na Mwakilishi kutoka Umoja wa Mataifa (UN), Dr. George Loy.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar