Wednesday, October 30

Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na watoto yasaini mkataba wa kupatiwa matibabu na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete

Katibu Mkuu Wizara ya Afya ,Ustawi wa Jamii,  Wazee , Jinsia na Wato Fatma Mrisho akisaini mkataba wakupatiwa matibabu ya  Moyo wagonjwa kutoka Zanzibar, katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo  Tanzania Bara, mara uongozi wa Taasisi hiyo ulipofika Ofisini kwake kwa ajili ya kufunga mkataba huo wa  miaka mitatu.

PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya ,Ustawi wa Jamii,  Wazee , Jinsia na Wato Fatma Mrisho akisaini mkataba wa kupatiwa matibabu ya  Moyo wagonjwa kutoka Zanzibar, katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo  Tanzania Bara, mara uongozi wa Taasisi hiyo ulipofika Ofisini kwake kwa ajili ya kufunga mkataba huo wa  miaka mitatu.

PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR.

Issa Mzee  – Maelezo 

Wazara wa Afya, Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto imetia saini Mkataba wa Makubaliano  na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete,  yanayohusisha upelekaji wa wagonjwa wa moyo wanaotoka Zanzibar  kupatiwa matibabu katika Taasisi hiyo.

Mkataba huo ulisainiwa na Katibu Mkuu wa  Wazara wa Afya, Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Zanzibar na Kiongozi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Pr.Mohammed Janabi, katika ukumbi wa Wizara hiyo Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya utiaji saini Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Fatma Mrisho amesema mkataba huo una manufaa makubwa kwa wanachi kwani utawasaidia katika kupatiwa matibabu kwa gharama nafuu.

Alisema uwepo wa taasisi hiyo nchini umeiwezesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutumia gharama nafuu katika matibabu ya moyo ikilinganishwa na kupeleka wagonjwa nje ya nchi jambo ambalo husababisha gharama kubwa kwa serikali.

Aidha alisema Serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha gharama zinazohitajika zinalipwa ili wananchi waweze kupatiwa matibabu katika taasisi hiyo.

Kwa upande wake Kiongozi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Pr.Mohammed Janabi, amesema  jumla ya wagonjwa 200 kutoka Zanzibar walipelekwa katika taasisi hiyo kwa ajili ya matibabu ambapo wagonjwa 31 walifanyiwa upasuaji na kupatiwa matibabu na hakuna aliepoteza maisha.

Alisema uamuzi wa Serikali ya Zanzibar wa kupeleka wagonjwa katika Taasisi hiyo, umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za kifedha ikilinganishwa na kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

Alieleza kuwa, Taasisi hiyo inamapango wa kuwaleta wataalamu wake Zanzibar ili kuweza kuwafanyia uchunguzi wa awali wagonjwa wa moyo kabla ya kusafirishwa kwa ajili ya matibabu.

Aidha alisema Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ipo tayari kuendeleza ushirikiano na Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ili kuhakisha wananchi wanapata matibabu nchini.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dkt, Marijani Msafiri, amesema ipo haja ya kuweka miundombinu ya kuwa na Taasisi ya Moyo Zanzibar ili wagonjwa waweze kupata matibabu visiwani hapa.

Hata hivyo, alisema bado ushirikiano wa karibu unahitajika baina ya Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ili wagonjwa wa moyo waweze kupata matibabu kwa wepesi.

Aidha aliwataka wananchi wa Zanzibar kufuata utaratibu ulioekwa katika Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja, na kuacha tabia ya kwenda moja kwa moja katika matibabu bila ya kupatiwa rufaa kutoka hospitalini hapo.