Wednesday, October 30

WATOTO kusoma ni haki yao na sio kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji “Siti Habib kutoka ZLSC

 

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

WAZAZI na walimu wameshauriwa kuwalinda watoto dhidi ya udhalilishaji na kuepuka kuwa miongoni mwa watendaji wa matendo hayo.

Akizungumza na wanafunzi katika skuli ya Maandalizi Madungu Chake Chake, mwanasheria kutoka Kituo cha Huduma za Sheria (ZLSC) Pemba Siti Habib Mohamed alisema, ipo haja ya kuwasaidia watoto wasifanyiwe udhalilishaji wanapokuwa skuli, madrasa na nyumbani.

Alisema kuwa, ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha watoto wanakuwa salama muda wote, huku wazazi na walimu wakiepuka kuwafanyia watoto hao udhalilishaji, kwani inaaminika kwamba wanakuwa kwenye mikono salama.

“Utasikia mwalimu au mzazi anambaka mtoto, kwa kweli inahuzunisha sana, kwa sababu hatujui sasa watoto waelekee wapi, zile sehemu ambazo tunaona ni salama kwao ndizo ambazo hufanyiwa ukatili huo”, alisema mwanasheria huyo.

Aliishauri jamii kwa ujumla waendelee kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbali mbali katika kupambana na janga hilo, ili kumlinda mtoto na kuhakikisha anapatiwa zile haki zote za msingi.

Aidha alielezea lengo la mkutano huo kuwa ni katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto, kwani kumekuwa na matendo mengi wanayofanyiwa watoto na kuona kwamba, kuna haja ya kuwaelimisha ili wajue namna ya kujilinda na kuripoti ikiwa wamedhalilishwa.

“Kwa vile tunapambana tumeona kwamba ipo haja ya kufika hapa skuli, kwani ukatili unaweza kufanyika sehemu yeyote, hivyo tunataka wajue kujinda na kujua viashiria vya udhalilishaji ili waviepuke”, alisema.

Kwa upande wao wanafunzi walipokuwa wakiulizwa athari za udhalilishaji walijibu kuwa, inaweza kusababishia mtoto maradhi, kifo, kuathirika kimwili, kisaikolojia na hata kuweza kukosa elimu na kupelekea kushindwa kutimiza ndoto zake za baadae.

Nao walimu wa skuli hiyo wamekishukuru kituo hicho kwa kuona umuhimu wa kuwapa elimu wanafunzi wao, wanaamini itazidi kuwasaidia kujikinga na kuripoti pale wanapofikwa na majanga hayo.

“Watoto wanaelewa maana ya udhalilishaji na athari zake, lakini wanashindwa kusema kutokana na kuwa na hofu, ila kupitia elimu hii tunatarajia hofu zitawatoka”, walieleza walimu hao.

Mkutano huo ulifanyika katika skuli ya Madungu Chake Chake ambao umeandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Pemba ikiwa wanaadhimisha siku 16 za kupinga ukatili na Udhalilishaji kwa wanawake na watoto.