Sunday, November 24

Uwandani wanataka elimu ya kisheria.

NA ABDI SULEIMAN.

WANANCHI wa Uwandani Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, wamesema kuwa bado elimu ya kisheria haijawafikia na wanahitaji kupatiwa elimu hiyo ili waweze kujuwa wapi wafuate haki zao za kisheria pale wanapozikosa.

Walisema wamekuwa wakikosa haki zao mbali mbali muda mrefu sasa, hivyo watakapopatiwa elimu hiyo wajuwa wapi wafikishe malalamiko yao ili kudai haki zao.

Waliyaeleza hayo katika mkutano wa wazi ulioandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, katika siku 16 za kupoga vita vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto nchini.

Salum Juma Hamadi mkaazi wa Uwandani, alisema masuala ya udhalilishaji uwandani yapo na yameshakuwa mzingo, huku wananchi wakishidwa kujuwa wapi pakupata haki zao baada ya kukosa elimu.

“Tumekuwa tuykishuhudia wananchi kusuluhishana wenyewe kwa wenye kwa kuogopa aibu, wengine kudai fidia ya fedha lakini kama ingekua wanajua sheria zinasema vipi yote yasingetokea”alisema.

Naye Sada Yahya Hamad alisema akinamama wanapaswa kukaa pamoja katika suala zima la ulezi wa watoto wa kike, kwani akinababa hawajuwi mazingira ya mtoto wakike yanavyokuwa.

Kwa upande wake Siti Hamad Massoud alisema suala la udhalilishaji katika visiwa vya Unguja na Pemba limekuwa ni kubwa, hivyo aliitaka idara ya Katiba na msaada wa kisheria kuangalia upya sheria ili kupunguzika kwa matendo yao.

Afisa Sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Yussra Abdalla Said, aliwasihi wazazi kuangalia nguo za watoto wao wanazowavisha, kwani zimekuwa zikiwatega sana wanaume kutokana na nguo hizo zilivyo.

Alisema jambo jengine matukio ya udhalilishaji yamekua ni biashara kwa sasa, kwani mtu anadai hata shilingi Milioni 20 ili kesi isiweze kupelekwa mahakani na anaweza kulipa.

Naye Mwanasheria Safia Saleh Sultani, aliwataka wananchi kufahamu sherai mbali mbali za nchi yao, kwani kutokujuwa sheria sio sababu ya kuvuja sheria, huku akiahidi kufika kuwapatia elimu ya sheria.

Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Pemba Asiya Ibrahim Mohamed, aliwasihi wananchi wa uwandani kutokuyakalia chini matendo hayo kwa kusuluhishana, kwani kutoa pesa sio suluhisho la tatizo hilo.