Sunday, December 29

VIDEO:”MUHALI ni moja kati ya sababu zinazorudisha nyuma mapambano juu ya Vitendo vya Ukatili na udhalilishaji wa kijinsia “RC SALAMA.

NA KHADIJA KOMBO- PEMBA               

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Muheshimiwa Salama Mbarouk Khatib amewataka wanajamii pamoja na wadau wa mapambano juu ya Vitendo vya Ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kuto vifumbia  macho vitendo hivyo kwa kuhakikisha vinachukuliwa hatua ili kukomesha kabisa vitendo hivyo nchini.

Akizungumza katika kilele  cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji wa kijinsia huko katika ukumbi wa chuo cha elimu Mbadala Vitongoji Pemba Mh. Salama amesema muhali ni moja kati ya sababu zinazorudisha nyuma mapambano hayo hivyo ni vyema jamii kuacha kabisa tabia hiyo ili kuhakikisha janga hili linaondoka.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali pamoja na Afisa Mdhamini Wizara ya Afya ustawi wa jamii jinsia na watoto Yakoub Mohammed Shoka wamewataka wazazi kuwa karibu na watoto wao kwa kufuatilia mienendo yao ili kuhakikisha usalama wao na kuwanusuru na  vitendo hivyo.

Kwa Upande wake Muwasilishaji mada juu ya usafirishaji haramu wa binaadamu pamoja na athari za ukatili na udhalilishaji Mohammed Jabir amesema kuna uwezekano mkubwa unaposafirishwa kinyume na utaratibu kukumbwa na vitendo hivyo kwani mara nyingi unapofika huko hufanyishwa kazi ambazo hazimo katika makubaliano hivyo amewataka wanajamii kuondokana na safari hizo.

Afisa Miradi Msaidizi Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamaji Tanzania (IOM) Sarah Ali Abdalla ameahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar katika kupiga vita vitendo hivyo.

Siku kumi na sita (16) za kupinga ukatili na udhalilishaji wa kijinsia hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 25 /11/hadi tarehe 10/12  ambapo kwa mwaka huu Kitaifa zimeandhimishwa Kisiwani Pemba.

 

KUANGALIA VIDEO HII YA MAADHIMISHO BOFYA HAPO CHINI.