AMINA AHMED MOH’D,PEMBA.
JITIHADA zilizofanywa na Gazeti la Zanzibar leo juu ya kumtangaza mama mjane ambae hali ya maisha yake ni duni kutokana na ulezi wa familia yenye watoto wanne pekee yake na kujiingiza katika udhalilishaji imeanza kuzaa matunda.
Kazi ya gazeti la Zanzibarleo ya kuuhabarisha umma juu ya hilo tayari kume jitokeza Wasamaria wema na kuanza kumsaidia mama huyo ambapo tayari hatua za awali za kuanza ujenzi zimeanza.
Akizungumza habari hizi mama huyo alisema anamshukuru muandishi wa habari hizo pamoja na gazeti la Zanzibar la tarehe 28 Octoba 2021 ambalo lilitangaza taarifa zake kwa kumtoa katika mateso ambayo yalikuwa yakimuandama kwa muda mrefu.
Alieleza kuwa mateso , shida na dhiki ambazo zilikuwa zinasababisha maisha magumu kwa watoto wake kutokana na malezi ya familia peke yake, na kugubikwa na umasikini na ugonjwa liliwafanya watoto wake kukumbwa na kadhia za udhalilishaji.
Bi maryam ambae ni mkaazi wa Chake Chake alitoa ya moyoni mara baada ya kuona harakati za ujenzi wa nyumba yake zikianza .
“Sijui niseme kitu gani lakini nimefurahi sana na nawashukuru nyote ambao mumesababisha mpka leo hii na mimi nimeanza kusaidiwa ili nipate sehemu salama ya kukaa na familia yangu”, alieleza kwa furaha mama huyo.
Akizungumza mmoja kati ya watoto wa mama huyo wa Bimaryam (jina
linahifadhiwa) aliwaomba wasamaria wengine kuiga mfano huo mara
watakapoyaona ama kuyasikia matatizo ya wanajamii tafauti wenye
masuala kama yao.
Oktoba 28 mwaka huu 2021 gazeti hilo lilitoa makala maalum juu ya malezi ya mama pekee yanavyochangia vitendo vya udhalilishaji ambapo kupitia makala hiyo wasamaria wema walimtafuta mwandishi wa habari hizi kwa lengo la kutaka kuwafikisha nyumbani kwa mama huyo.
Lengo la kufika kwa mama huyo ni kuangalia na kujionea hali halisi na kuahidi kumsaidia ambapo tayari wameanza kutekeleza ahadi zao kwa kuanza harakati za ujenzi huku wakiahidi mara utakapokamilika ujenzi huo watasaidia mtaji wabiashara kwa familia yake.
Hata hivyo wasamaria hao ambao hawakutaka kutajwa majina yao
walivipongeza Vyombo vya habari hususan Gazeti hilo la Zanzibar leo kwa kufanya wajibu wao kwa weledi unaotakiwa na kuondosha matatizo kama hayo jambo ambalo linaweza kuondosha changamoto ambazo zinaweza kuifanya jamii kujiingiza katika udhalilishaji.