Mkutano ulioitishwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa na wadau wa siasa unaendelea jijini Dodoma, Tanzania. Ulianza Jumatano, Desemba 15 na ulitarajiwa kudumu kwa siku tatu hadi Ijumaa Desemba 17, 2021.
Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mkutano, imepokelewa kwa hisia huku mijadala na mabishano ikiendelea nje , hasa katika mitandao ya kijamii.
Mkutano huo uliwakutanisha washindani wa kisiasa, upande wa chama tawala na vyama vya upinzani na wadau wa siasa. Ulilenga kujadili demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini humo. Ndiyo mkutano wa kwanza wa aina hiyo tangu kumalizika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2020.
Tangu awali, uhusiano wa utawala na chama tawala kwa upande mmoja na vyama vya upinzani kwa upande mwingne, haikuwa wa kuridhisha. Ajabu ya mambo, mkutano huo umeibua mvutano mpya unaovihusisha vyama vikuu vya upinzani, ACT Wazalendo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kipi kiini cha mvutano wa upinzani?
Msingi wa mvutano wa sasa na majibizano makali ni kutofautiana kati ya chama kikuu cha upinzani bara, Chadema na kile kikuu cha upinzani Zanzibar, ACT Wazalendo, juu ya njia bora ya kuondoa mkwamo wa kisiasa uliopo kwa kushirikiana na upande wa serikali.
ACT Wazalendo wamelitumia jukwaa la mkutano wa wadau wa siasa kutafuta maridhiano na kumuomba Rais Samia, kutafuta njia inayofaa ili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anayeshikiliwa kwa tuhuma za ugaidi aachiwe huru.
“Tunakuomba sana kwa mujibu wa sheria na kufuata taratibu zote za kisheria tusaidie mwenzetu tuwe naye ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja, tuunganishe nchi yetu, tufanye siasa kwa tija kwa masilahi ya nchi yetu.” Alisema Zitto Kabwe, kiongozi wa ACT Wazalendo, wakati akihutubia mkutano huo.
Kwa upande wa Chama cha Chadema na NCCR Mageuzi vimesusia mkutano huo, hawakuona ni jukwaa sahihi kwao kushiriki majadiliano ya kisiasa. Mkutano haukukidhi haja ya mjadala wa kisiasa wautakao. Wakautafsiri ni mkutano wa kupiga picha na Rais Samia.
Maamuzi ya kuhudhuria au kutohudhuria ndiyo yamezalisha zogo kati ya viongozi na wafuasi wa vyama vikuu vya upinzani. Kila chama kimechukua uamuzi tofauti kufikia lengo moja la kisiasa, ambalo ni utawala wa sasa kuachana na baadhin ya sera za ba ni misimamo inayotafsiriwa na baadhi ya watu kuwa kutokuwa ya haki hususan kwa vyama vya upinzani.
Wapi mambo yamekwenda kombo?
Ripoti ya taasisi ya Human Rights Watch ya Januari, 2019 juu ya Tanzania, ilieleza kuporomoka katika uzingatiaji wa uhuru wa kujieleza, kujumuika na kukusanyika tangu kuingia madarakani Rais wa awamu ya tano Rais John Magufuli, ambaye sasa ni marehemu, pamoja na ukiukwaji wa haki zingine za binadamu.
Itakumbukwa hayati Magufuli aliingia na sera zilizoondosha kabisa uhuru wa kisiasa, ikiwemo mikutano na maandamano. Wakati wa uongozi wa Magufuli palishuhudiwa kamatakamata ya mara kwa mara ya viongozi wa upinzani na wafuasi wao na kufunguliwa kesi mbali mbali mahakamani.
Hata baada ya Rais Magufuli kufariki Machi 17, 2021, bado sera zake na misimamo yake ipo hai. Rais wa sasa pamoja na kusisitiza kusamehe na kuwaacha watu kusema ya moyoni, bado hali haijabadilika sana kwa misimamo ya awali ndiyo inazochagiza patashika ya muda mrefu kati ya upinzani na utawala.https://www.bbc.com/ws/av-embeds/cps/swahili/michezo-59693880/p09rrg9m/swMaelezo ya video,
Rais Samia: Mashtaka dhidi ya Mbowe hayajachochewa kisiasa
Je, Rais Samia katimiza ahadi yake?
Aprili 22, 2021 akitoa hutuba yake ya kwanza iliyotoa mwelekeo wa serikali yake ndani ya Bunge jijini Dodoma, Rais Samia alieleza nia yake ya kutaka kukutana na kuzungumza na vyama vya kisiasa nchini.
Katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, mwezi Agosti mwaka huu, Rais Samia alieleza azma yake ya kuonana na upinzani bado ipo. Ingawa hakuweka wazi siku rasmi ya mkutano huo.
Mkutano unaoendelea Dodoma haukuitishwa na Rais Samia. Kauli yake ya kutaka kuonana na vyama vya kisiasa, kwa wengi ilimaanisha yeye mwenyewe ndiye ataitisha mkutano huo, kujadiliana na vyama juu ya hali ya siasa nchini.
Kwa hakika haieleweki bayana kusema katimiza ahadi. Ila ni rahisi kusema baadhi ya mijadala ya kisiasa ambayo ingezuka katika mkutano aliouahidi yeye, yameibuliwa na yanajadiliwa katika mkutano unaoendelea Dodoma.
Mkutano huu utaleta tija?
Mkutano huu umeonesha ishara njema katika mambo kadhaa. Moja, Rais Samia ametoa nafasi kwa vyama vya kisiasa kukaa na kujadili namna ya kufanya mikutano. Akitambua ni haki yao ya msingi.
“Naomba leo hapa mjadili pamoja na mambo mengine namna ya kufanya mikutano ya siasa ya hadhara kwa mujibu wa sheria, nafahamu ni haki yenu.”
Kauli hii inaashiria uwezekano wa serikali kuondoa katazo hilo ambalo linakwenda kinyume na katiba ya nchi inayoruhusu shughuli za amani za kisiasa, bila upendeleo wala kuingiliwa na kuvunjwa na Jeshi la Polisi.
Pili, Rais Samia amesikiliza ombi la Zitto Kabwe la kutaka Mbowe aachiwe huru. Kauli yake juu ya ombi hilo inaashiria uwezekano wa kesi inayomkabili kigogo huyo wa Chadema kupatiwa ufumbuzi wa kisiasa.
Kwa hakika bado kuna mengi ya kuyasubiri na kuona. Ikiwa mkutano huu utakuwa ndio mwanzo wa kufunguka dirisha la maelewano kati ya upinzani na utawala ama ni dirisha litalofungua malumbano makali zaidi ya kisiasa.
CHANZO CHA HABARI BBC SWAHILI NEWS.