Thursday, January 16

Maafisa wa Serikali Wilaya ya Chake Chake wametakiwa kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika mipango ya maendeleo.

Na, Hassan Mselle, Pemba.

Maafisa wa Serikali kutoka Wilaya ya Chake waliyopatiwa mafunzo ya ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika mipango ya kimaendeleo wameombwa kuyafanyia kazi mafunzo hayo ili kuboresha mustakbali wa wenye ulemavu nchini.

Ombi hilo limetolewa na mratibu wa Baraza la taifa la watu wenye ulemavu Kisiwani Pemba Bi. Mashavu Juma Mabrouk wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo ya siku tisa ya ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika mipango ya maendeleo yaliyotolewa kwa maafisa kutoka  taasisi mbali mbali  za Serikali huko katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Chake Chake amesema lengo la mafunzo ni kutoa elimu kwa maafisa hao juu ya umuhimu wa ujumuishwaji wa mipango ya maendeleo kwa watu wenye ulemavu nchini.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamejikita katika haki kuu za watu wenye ulemavu ikiwemo elimu, afya, kazi, kujikimu pamoja na uwezweshaji.

        ‘’Tumeamua kutoa mafunzo haya kwa maafisa wa taasisi mbali mbali kwasababu wao ndio watendaji wakuu wa mipango ya maendeleo ya watu wenye ulemavu ili waone basi kuwa mipango yote wanayopanga wanahakikisha kuwa wanaweka ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu’’ alisema Mratibu huyo

Kwa upande wake afisa jinsia na maendeleo kutoka baraza la taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar Munira Abdulhalim Mohammed amesema  tafiti ambazo hazikushirikisha kikamilifu watu wenye ulemavu zimetoa ushahidi mdogo kuhusu changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu katika jamii, hivyo basi amewaomba maafisa hao kushirikiana idara pamoja na jumuiya za watu wenye ulemavu pindi wanapohitaji kufanya utafiti.

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo Mwenyekiti wa jumuiya ya Wanawake wenye ulemavu Zanzibar Salma Haji Saadat amesema watu wenye ulemavu wanakabiliwa na vikwazo mbali mbali ambavyo huwazuia kufikia lengo la ujumuishwaji kama vile okosefu wa vifaa vya marekebisho, vikwazo vya miundombinu pampja na vikwazo vya kimtazamo.

        ‘’Watu wenye ulemavu mara nyingi huzuiwa kufikia upeo wa uwezo wao si kwa sababu ya ulemavu wao tu bali ni kutokana na vikwazo vya kimazingira, kimtazamo na kitaasisi wanavyokabiliana navyo’’ alifafanua

Riziki Hamad Ali ni mwalimu kutoka kitengo cha elimu mjumuisho amesema ripoti ya dunia iliyochapishwa mwaka 2011 imeeleza kuwa watu wenye ulemavu hukabiliwa na gharama za ziada zinazotokana na ulemavu wao ambapo 15% ya matumizi ya kaya kwa ajili ya matibabu ukilinganisha na 11% kwa watu wasio na ulemavu.

                ‘’Hii inaonesha dhahiri kuwa watu wenye ulemavu wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa huduma za matibabu kwa kiasi kikub ilinganishwa na watu wasio na ulemavu hivyo basi maafisa wa afya munapaswa kuliangalia kwa umakini sana hili’’ alisema

Kombo Ali Hamad ni mtu mwenye ulemavu wa viungo ambaye na mshiriki wa mafunzo hayo amewataka maafisa hao kufahamu changamoto zinazo wakabili watu wenye ulemavu pamoja na kushirikiana na idara na jumuiya za watu wenye ulemavu ili watu wenye ulemavu waweze kupata haki zao za msingi.

        ‘’Wengi walioshiriki katika haya mafunzo ni watendaji wa Serikali kwahivyo nawaomba waelewe changamoto za watu wenye ulemavu kwakushirikiana na jumuiya za watu wenye ulemavu ili watu wenye ulemavu wapate haki zao za msingi isionekane kama watu wenye ulemavu ni watuwakufanyia huruma nakuwapendelea tu’’ alieleza

Aidha amesema watu wenye ulemavu wanakabiliwa na Changamoto kadhaa ikiwemo Changamoto ya ufikiaji wa huduma za msingi ikiwemo huduma ya elimu, afya, stadi za maisha pamoja na kazi kutokana na miundombinu ya majengo isio rafiki kwa watu wenye ulemavu sambamba na ukosefu wa visaidizi kama vile Vitimwendo, fimbo za kutembele, magongo ya kutembelea nakdhalika.

        ‘’Wengi waliohudhuria mafunzo haya ni watendaji wa Serikali kwahivyo tunawaomba waelewe namna ya kuwajumuisha watu wenye ulemavu waelewe changamoto za watu wenye ulemavu ili watu wenye ulemavu wapate haki zao za msingi na isionekane kuwa watu wenye ulemavu ni kuwafanyia huruma au kuwapendelea tu’’ alisema

Nae Dau Silima Ali kutoka jumuiya ya wakalimani wa lugha za alama Zanzibar (JUWALAZA) amewashauri wananchi kusomea lugha za alama kwani idadi ya wakalimani Kisiwani Pemba ni ndogo ukilinganishwa na uhitaji.

        ‘’Kwakweli changmoto ya ukosefu wa wakalimani ni kubwa sana kwasababu hata ukiangalia mahakamani wakalimani hakuna kwahivyo mtu mwenye ulemavu wa usikivu au kuongea anaweza kukosa haki yake ya kwasababu tu ya kukosa mkalimani kwahivyo nawaomba sana wananchi kujitoa zaidi kwenda kusomea lugha ya ukalimani wala sio ngumu kama wanavyodhani’’ alisema

Nao maafisa hao wameahidi kuyafanyia kazi ipaswavyo mafunzo hayo ili kuhakikisha mipango na mikakati ya kimaendeleo ya Serikali inaboreshwa zaidi sambamba na kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu nchini.

Mafunzo hayo ya siku tisa yenye lengo la kujenga uelewa kwa maafisa wa Serikali juu ya ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika mipango ya maendeleo yamejumuisha maafisa kutoka taasisi mbali mbali za Serikali Wilaya ya Chake Chake.