NA ABDI SULEIMAN.
KAMISHENI ya Utalii Pemba imewataka wamiliki wa mahoteli, nyumba za kulala wageni ndani ya kisiwa hicho, kuhakikisha wanakata leseni za mwaka mpya, ili kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Kamisheni imesema ukataji wa leseni unamuwezesha mliki wa hoteli na nyumba ya kulala wageni, kufanya biashara yake kikamilifu bila ya kupata vizingiti vyoyote vile.
Akizungumza na Zanzibarleo katika ziara ya uhamasishaji ukataji wa leseni, ukaguzi wa vyumba, sehemu za utupaji takataka, vifaa vya huduma ya dharura na hali ya usafi wa jikoni, katika hoteli mbali mbali Kisiwani Pemba.
Afisa uhusiano na Tathmini kutoka Kamisheni ya Utalii Pemba Haitham Suleiman Khamis, alisema lengo la ziara hiyo ni uhamasishaji juu ya ukataji wa leseni mpya za kazi, kutambua changamoto zilizojitokeza msimu uliopita na kuzifanyia kazi ipaswavyo.
Alisema wamelazimika kufanya ukaguzi huo, ili kujiridhisha kuwa vyumba vilivyopo ndio hivyoi hivyo au kuna vilivyoongezeka, pamoja na utoaji wa huduma kwa lengo la kuepuka udanganyifu unaoweza kujitokeza.
“Unajua udanganyifu upo katika maeneo yote, mtu anaweza kukwambia anavyumba hivi kumbe kuna na vyengine hajavisema, sasa hapa serikali inakosa mapato”alisema.
Aidha aliwataka wamiliki hao wa mahoteli na nyumba za kulala wageni, kuhakikisha wanavitangaza vivutio vya utalii vilivyopo Pemba kwa wageni wao wa naokuja kwenye hoteli zao, sambamba na kuwa na mazingira mazuri ya uhifadhi wa takataka zao
Kwa upande wake Mdhamini wa Kamisheni hiyo Hamad Amini, aliwataka wamiliki hao wa mahoteli na nyumba za kulala wageni, kueleza ukweli katika kazi zao hususana kwneye suala la utoaji wa huduma kwa wateja.
Alisema haipendezi kuona mmiliki huyo anatoa taarifa isiyo sahihi kwenye mikataba yake ya leseni, wakati anajua kwama kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Naye Mkuu wa Huduma katika hoteli ya The Manta Resort iliyopo Makangale Shaban Abdalla, alisema utubaji wa takataka ni aibu kubwa kwa wageni, hali inayolekea kila siku kusafisha maeneo ya hoteli na kila wiki husafisha fukwe kwa ajili ya wageni.
“Tatizo lipo kwa wananchi wanakwenda pikiniki katika maeneo ya fuke zilizpo karibu na hoteli hiyo, pamoja na pango la hatoro kutembea, huwacha mataka yao baada ya matembezi na kushindwa kusafisha hali inayokuwa kero kubwa kwa wageni wao”alisema.
Aidha alisema suala la usafi kwao ni kitu muhimu na chakwanza katika sekta ya utalii, huku akiiyomba kamisheni ya Utalii kuweka watu maalumu katika maeneo ya fukwe kwa ajili ya kuwatia hatiani watakao chafua.