Friday, January 17

WHO yataka baadhi ya matukio ya msimu wa sikukuu kusitishwa kwa kuhofia Omicron

 

m

Shirika la Afya Duniani WHO limewasihi watu kufuta baadhi ya mipango yao katika kipindi hiki cha mapumziko ili kupunguza kasi ya maambukizi ya aina mpya ya virusi vya Corona vya Omicron vinavyoendelea kusambaa duniani kote.

Mkurugenzi wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kufutwa kwa baadhi ya matukio yaliyopangwa ni bora, kuliko kuondoa uhai na kuongeza kuwa maamuzi magumu ni lazima yakachukuliwa.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Tedros Ghebreyesus amesema kwa sasa kuna ushahidi tosha kwamba aina ya virusi vya Omicron vinasambaa kwa kasi kushinda vya Delta. Na kuwataka watu kuahirisha kwa muda mipangilio yao.

” Sote tumechoka na hili janga. Wote tunataka kutumia muda wetu kuwa pamoja na marafiki pamoja na familia zetu. Sote tunataka hali irudi kawaida.

” Njia ya haraka kuweza kufanikisha hili ni kwa sisi sote viongozi na kila mmoja kuchukua maamuzi magumu kuweza kujilinda wenyewe na kulinda wengine.

Ni bora kufuta matukio tuliyopanga kufanya, kuliko kuyaondoa maisha… Ni bora kuacha kufanya sasa na kusherehekea baadaye kuliko kusherehekea sasa hivi na kuja kupatwa na huzuni baadaye.”

Kauli hiyo ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya imekuja wakati baadhi ya nchi ikiwemo Ufaransa na Ujerumani kuweka masharti makali na vikwazo vya safari katika jitihada za kujaribu kuzuia kusambaa kwa aina hii mpya ya virusi vya Corona. Uholanzi tayari imetangaza zuio la kutoka nje katika kipindi hiki cha msimu wa Krismas.

Marekani nako Ikulu ya nchi hiyo imesema Rais Joe Biden hana mpango wa kuweka zuio, hapo awali mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza nchini humo Dokta Anthony Fauci alionya kuwa safari katika kipindi hiki cha Krismasi zitaongeza kusambaa kwa Omicron hata kwa watu ambao wamepata chanjo kamili.

Wizara ya Mambo ya nchi za nje ya Marekani na Taasisi ya kudhibiti na kujikinga na magonjwa nchini humo CDC zimewashauri raia wa nchi hiyo, kutosafiri katika nchi nane zikiwemo Hispania, Finland, Chad na Lebanon.

Nchini Uingereza nako sherehe za mwaka mpya katika baadhi ya maeneo maarufu zimefutwa , ikiwa ni hatua zilizochukuliwa kwa ajili ya usalama wa afya.

Aina hiyo ya virusi vya Omicron iligunduliwa nchini Afrika Kusini Novemba mwaka huu.

Dokta Tedros amesisitiza pia janga hili linaweza kumalizika mwakani iwapo asilimia 70 ya watu katika kila nchi duniani watakuwa wamechanjwa ifikapo katikati ya mwaka huo 2022.

Aidha amesema China nchi ambayo janga hili la mlipuko wa Corona lilipoanzia mwaka 2019, ni kazima iweke wazi taarifa. Ili kuweza kujulikana kwa chanzo.

CHANZO CHA HABARI BBC SWAHILI NEWS.