NA ABDI SULEIMAN.
MAHAKIMU na Mkadhi Kisiwani Pemba, wamesema kuwa wapo tayari kujitoa katika kuhakikisha upatikanaji wa haki, kwa watu wasiokuwa na uwezo na wenye mahitaji maalumu unafanikiwa kwenye mahakama mbali mbali kisiwani hapo.
Walisema upatikanaji huo wa haki kwa watu wasiokuwa na uwezo na wenye majitaji maalumu, ulikuwepo tokea awali lakini sasa watahakikisha wanalipa kipaombele jambo hilo.
Wakizungumza na Zanzibar leo mjini Chake Chake, katika mafunzo ya Mahakimu juu ya upatikanaji wa haki kwa watu wasiokua na uwezo na wenye mahitaji maalumu katika mahakama.
Hakimu wa mahakama ya Mkoa wa Chake Chake Lusiano Makoye Nyango, alisema mafunzo hayo yalikuwa muhimu kwao yataweza kuimarisha utendaji kazi wao, kwani jukumu lao ni kusaidia wananchi wasiokuwa na uwezo katika suala la upatikanaji wa haki.
“Tupo tayari kujitolea ili kuona haki inapatikana kwa wasio kuwa na uwezo na wenye mahitaji maalumu, chamsingi ni kufuata sheria na taratibu kama zilivyo”alisema.
Naye kadhi wa Wilaya ya Chake Chake Omar Juma Othamana, alisema watakahakikisha wanafanya kazi kwa pamoja na wasaidizi wa sheria, baada ya kujuwa majukumu yao na kuona wananchi wanapata haki zao zinazostahiki.
Hakimu wa Wilaya ya Chake Chake Nema Juma, alisema mafunzo hayo yamewaongezea ujuzi katika kuwasaidia watu wasio kuwa na uwezo kisheria ili kuona wanapata haki zao za kisheria.
Aliwataka wananchi kuendelea kujenga imani na Mahakama, mahakimu na makadhi pale wanapopeleka malalamiko au wanapokuwa na kesi zao, ili kuona jinsi gani mahakama hizo zinavyowapatia haki.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, alisema ipo haja ya kubadilika kwa mahakimu na majaji, kutokana na mafunzo hayo waliopatiwa jambo ambalo litaweza kuleta ufanisi mzuri katika kazi zao.
Alisema wanawajibu mkubwa kwa sasa kwenda kufanyia kazi, yale ambayo yatapunguza malalamiko kwa wananchi juu ya upatikanaji wa haki katika mahakama kwa kuzingatia sheria na kanuni.
“sio jambo jema kuona tunalalamikiwa katika mahaka zetu, nena rudi nenda rudi wengine ndio kama hao wanasema wanamuachia mungu, baada ya kukosa haki zao kwa muda mrefu”alisema.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Saidizi wa Mahakama Mkuu Pemba Thuweba Amour Haji, aliiyomba Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar, kuendelea kuwapatia mafunzo mahakimu na majani, pamoja na kuwaangalia makarani wa mahakama katika mafunzo yanayokuja ili kuona haki inapatikana kwa urahisi.
MWISHO