Monday, November 25

MSWADA WA SHERIA YA KUANZISHWA KWA MAMLAKA YA UDHIBITI DAWA ZA KULEVYA WAPITA

KUPITISHWA  kwa sheria ya kuanzishwa kwa mamlaka ya udhibiti ya madawa ya kulevya itaipa nguvu mamlaka hiyo katika mapambano dhidi ya waingizaji, wasambazaji na watumiaji wa madawa hayo Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo wakati akiaghirisha Mkutano wa Tano wa Baraza la Kumi la wawakilishi uliofanyika katika ukumbi wa baraza hilo Chukwani Jijini Zanzibar.
Alisema tatizo la dawa za kulevya limekuwa janga Duniani kote hali inayosababisha kupoteza nguvu kazi ya taifa, hivyo uamuzi uliofanywa na wajumbe wa baraza hilo ni wa kupongezwa kutokana na kuzamiria kutatua na kuondosha kabisa kadhia hiyo.
Mhe. Hemed alieleza ni jukumu la kila mwananchi kushiriki kwa namna moja au nyengine katika mapambano ya madawa ya kulevya huku akiwahidi wajumbe wa baraza hilo kuwa serikali itahakikisha inasimamia na kutekeleza sheria hiyo ili kutokomeza madawa ya kulevya Zanzibar.
Akizungumzia juu ya dhana ya utawala bora Makamu wa Pili wa Rais alitumia fursa hiyo kuiagiza Tume ya Maadili ya Umma kuendelea kutoa taaluma kwa viongozi wa ngazi mbali mbali wakiwemo masheha na madiwani ili kujua umuhimu wa ujazaji wa Fomu ya tamko la mali na madeni ambazo zipo kwa mujibu wa sheria.
Aidha, aliwapongeza wajumbe wa baraza hilo kutokana na ukomavu na uweledi wao kisiasa kwa kuwasilisha hoja tatu (3) za msingi katika mkutano huo wa tano wa baraza la kumi la wawakilishi ikiwemo hoja ya kuanzishwa kwa mtandao wa wabunge wa Afrika Mashariki wa kupambana na rushwa kanda ya Zanzibar hoja ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa miradi mikubwa ya kimaendeleo inayotarajiwa kutumia fedha nyingi.
Kuhusu kufanikisha utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo Makamu wa Pili wa Rais aliziagiza taasisi zote zinazotekeleza miradi hiyo kushirikiana na wakuu wa Wilaya na Mikoa samba na kuwapa taarifa wananchi waliokaribu na maeneo ambayo miradi hiyo inatekelezwa kwa lengo la kuondoa kasoro ndogondogo zinazoweza kujitokeza.
“Ni matumaini yangu kuwa miradi hiyo itasimamiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa pamoja na kuzingatia Value for Money kwa sekta zote ikiwemo Elimu, Afya na uwezeshaji wananchi kiuchumi kama ilivyoelezwa na Mhe. Rais” Aliesma Makamu wa Pili wa Rais
Akigusia juu ya wahanga wa Maste Life Mhe. Hemed alisema serikali imeanza mchakato wa kuwalipa wananchi fedha zao na zoezi hilo linaendelea vizuri ambapo aliwaomba wananchi kuendelea kuwa wastahamilivu wakati serikali inaendelea na juhudi za kuwarejeshea amana zao.
Alieleza kuwa kuanza kwa utaratibu huo ni kutimiza ahadi ya Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alioitoa wakati akilihutubia taifa katika sherehe ya kutimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani.
Akielezea kuhusiana na kutimia kwa miaka 58 ya Mapinduzi matukufu ya 1964 Mhe. Hemed aliesema sherehe hizo zitajumuisha uzinduzi na uwekaji a mawe ya msingi katika miradi mbali mbali Unguja na Pemba ambapo harakati zinatarajiwa kuanza rasmi Januari 01, 2022 kwa kuadhimisha tamasha la mazoezi ya kitaifa.
Alifafanua kwamba, kutokana na jamii kukubwa na maradhi mingi yasiombukiza ikiwmo kisukari, presha, shindikizo la damu, kiharusi na saratani aliwaasa wananchi kuchkua tahadhari mapema kwa kushuhulisha mwili na mazoezi ambapo serikali zote mbili zimeandaa muongozo wa kuushuhulisha mwili kwa kufanya mazoezi muongozo ambao unasimamia chini ya uongozi wa Wizara ya Afya.
Pamoja na mambo mengine, Mhe. Hemed amewakumbusha wajumbe wa baraza hilo kushirikiana na serikali kwa kuielimisha jamii katika majimbo wanayoyaongoza juu ya umuhimu wa kushiriki kuhesabiwa kupitia zoezi la sensa ya watu na makaazi linalotarajiwa kuanza mwakani kwani zoezi hilo litaisidia Nchi kupanga vizuri mipango yake ya maendeleo kwa kipindi cha miaka kumi (10) ijayo kwa kupata takwimu halisi na sahihi ya idadi ya watu na makaazi.
Akigusia juu ya suala la mazingira Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza serikali itashirikiana na Jumuiya ya wawakilishi inayohusiana na mabadiliko ya Tabia Nchi kwa lengo la kuhakikisha inalinda mazingira na kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuyatunza mazingira, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni katika kuelekea uchumi wa Buluu.
“Ukweli usiofichika mazingira yetu hivi sasa yapo katika hali mbaya kiasi kwamba maeneo ya kilimo yanaingia maji chumvi, kiwango cha maji ya bahari kimepandaa juu, viumbe vya baharini vimepotea na hata mvua hazinyeshi kwa miongo kama kawaida yake” Alisema Makamu wa Pili
Mkutano wa Baraza la wawkilishi umeaghirishwa hadi siku ya Jumatano ya Febuari 16, 2022 Saa Tatu kamili Asubuhi.
MWISHO