NA ABDI SULEIMAN.
ASASI za Kiraia zinazofanya kazi na vijana zimetakiwa kuwasilisha taarifa zao za kazi katika taasisi ya Vijana ili serikali ifahamu kazi wanazozifanya katika kuwainua vijana katika harakati za kiuchumi.
Hayo yameelezwa na afisa Mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Salum Ubwa Nassor, wakati akifungua mkutano wa uratibu wa shughuli za wadau wa maendeleo ya Vijana uliowashirikisha wadau kutoka taasisi za kiraia na serikali na kufanyika mjini Chake Chake.
Alisema asasi hizo zinafanya kazi kubwa sana lakini hazionekani, hivyo wanapaswa kushirikiana na serikali ili zinapotokezea changamoto ziweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Aidha aliwataka wadau wa maendeleo ya vijana Pemba, kuzidisha mashirikiano kwa wizara na jumuiya za vijana ili kuwasaidia kama lilivo lengo la Rais wa Zanzibar dk, Hussein Ali Mwinyi la kuhakikisha wanajikwamua kimaisha.
“kikao hichi kitasaidia namna ya upatikanaji wa taarifa kwa serikali na kwa jamii ili serikali itambue kazi wanazozifanya kwa ajili ya vijana ambao wamekusudiwa kuendelezwa na kusaidiwa kujikwamua kiuchumi,”alisema.
Alifahamisha kuwa, wasimamizi wakubwa wa kuwaendeleza vijana ni wadau hao na ndio maana wizara imeona kuna haja ya kufanya kikao hicho chenye lengo la kujadili ambayo wamekua wakiyafanya kwa maslahi ya vijana.
“Tunaelewa kuna mambo mengi ambayo munayafanya lakini kwa bahati mbaya taarifa zenu hazifiki sehemu zinazohusika jambo ambalo wengi wasioelewa hawafahamu kitu gani munakifanya kwa vijana na badala yake kunaletwa tafsiri zisizofaa kwenye taasisi na asasi zenu”, alisema.
Hata hivyo aliwataka wadau hao licha ya kuwa wanakumana na vikwazo vingi katika kuwasaidia vijana lakini wasivunjike moyo sambamba na kuwataka wasogee katika wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo kwani alisema ipo kwa ajili ya kutoa mashirikiano kwao ili kulisaidia taifa lao.
Akielezea lengo la mkutano huo mratib wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Pemba Ali Mussa Bakar, amesema ni kuona wanashirikiana na asasi za kiraia kuangalia ni miradi gani haijawafikia vijana.
Mratib huyo alisema, wadau wengi wa vijana wamekua wakifanya shughuli ambazo zina lengo la kuwaendeleza vijana na kila mdau hufanya kwa upande wake ambao unafaa.
Alisema kuwa, kikao hicho kina lengo la kuratibu shughuli za wadau ambazo wamekua wakizifanya ili kuona kwa asilimia kubwa ya vijana wananufaika katika maeneo yote na rika zote.
Aidha alisema, katika utekelezaji wa sera ya maendeleo ya vijana imetakiwa kuwafikia vijana kwa kuwahudumia kupitia maendeleo yao ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.
Akiwasilisha taarifa ya mradi wa kijana hai foundatiom Suleiman Mujoni Baitani alisema, mradi wao kwa sasa wanachokifanya ni kutoa mafunzo ya stadi za maisha, ujasiriamali na matumizi ya fedha.
“Mradi wetu ambao tunaufanya Pemba unaitwa miliki uwezo unalenga kuimarisha ujasiriamali wanawake, kuwawezesha kujenga biashara endelevu zenye faida za kukua ili waweze kuingia katika uchumi rasmi kwa Kisiwa cha Pemba”,alisema.
Alisema, wanufaikaji wa mradi huo ni wanawake 60 ambao wamegaiwa kwenye makundi matatu ikiwemo wanawake wenye umri wa miaka 25-40, wanawake vijana wenye umri 18-35, na wanawake wenye ulemavu wenyeumri 18-35.
Akiwasilisha taarifa ya uwezeshaji mratibu wa mfuko wa uwezeshaji Pemba Farid Hamuni Juma alisema, mkopo unaweza kupatiwa kupitia mfuko huo ni kuanzia shilingi 500,000/= hadi 1,000,000/= na kurejesha ni miezi sita hadi mwaka mmoja.
Alisema, walengwa wakuu wa mfuko huo ni vijana na akina mama ambao wanajishuhulisha na mradi wa mboga mboga na matunda ambapo mwezi Julai-Disemba mwaka huu wametoa mikopo 113 yenye thamani ya shilingi milioni 90,500,000 na kati ya waliopatiwa mkopo huo vijana 29 walibahatika kupata milioni 21,800,000.
MWISHO.