Hassan Msellem, Pemba
Jumuiya ya watu wasioona Zanzibar (ZANAB) imesema watu wenye Ulemavu wa Macho hawapewi kipaumbele katika nafasi za ajira licha ya kuwepo baadhi ya watu wenye Ulemavu wa Macho ambao Wana vigezo stahiki vyakupatiwa nafasi ya ajira kwa mujibu wa fani walizosoma.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa jumuiya hiyo kisiwani Pemba Suleiman Mansour Suleiman amesema Kuna watu wenye Ulemavu wa Macho ambao wamehitimu fani mbali mbali Kwa ngazi za shahada na astashada pamoja Cheti lakini wananyimwa haki yao ya msingi ya kufanya kazi katika taasisi za Serikali.
‘’Ukweli ni kwamba Kuna idadi kubwa ya watu wenye Ulemavu wa Macho ambao wamehitimu fani mbali mbali Kama vile ualimu, ufundi, watunza Kumbu Kumbu nakadhalika lakini Kama utafanya uchunguzi Chake mzima hii hawazidi hata watu watano ambao Wana Ulemavu wa Macho ambao wameajiriwa’’ alisema
Ili kupata takwimu sahihi ya watu wenye Ulemavu wa Macho ambao wameajiriwa katika taasisi za Serikali kwa upande wa Wilaya ya Chake Chake nilifika katika ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora nakufanikiwa kukutana Afisa Mdhamin Wizara hiyo ambaye ni Bi. Halima Khamis Ali ambapo amesema katika wizara tisa ambazo wamefanya utafiti ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali pekee ambayo imeajiri mtu wenye Ulemavu wa Macho.
“Tumefanya utafiti Kwa wizara tisa za Serikali lakini katika wizara zote hizo ni wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali pekee ndio ambayo imeajiri mtu mmoja mwenye Ulemavu wa Macho ambaye ni mwanamke, kwahivyo inanosha ni jinsi ambayo watu wenye Ulemavu wa Macho wanavyokabaliana na changamoto ya ukosefu wa ajira licha ya baadhi yao kuwa na vigezo vya kuweza kuajiriwa Kwa mujibu wa taaluma zao” Alisema
Sambamba na hilo Mwenyekiti huyo amesema jumuiya hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ya ukosefu wa fedha pamoja ufinyu wa ofisi jambo ambalo linasababisha kushindwa kufanya shughuli zao ipaswavyo.
Ili kupata ufumbuzi juu ya changamoto zinazoikabili jumuiya hiyo Pemba Press Club nilizungumza na Mratibu wa baraza la taifa la watu wenye ulemavu Kisiwani Pemba Mashavu Juma Mabrouk amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatenga kiasi cha fedha kila mwaka kwa ajili ya kuiwezesha jumuiya hiyo ingawa kiasi kinachotengwa kinakuwa kidogo kutokana wingi wa jumuiya hizo pamoja na mahitaji ya Baraza.
‘’Kila bajeti ya mwaka inaposomwa basi kuna kiwango chao cha fedha wanachotengewa ingawa kiasi hicho kinaweza kuwa ni kidogo kutoakana wingi wa jumuiya hizo pamoja na majukumu ya baraza huwezi kuwaahidi kuwa mwaka huu tutatoa kila jumuiya millioni 20 wakati bajeti yetu ni millioni mia moja’’ alieleza
Akiendelea kuelezea changamoto hizo mwenyekiti wa jumuiya hiyo amewalalamikia viongozi wa mfuko wa kunusuru kaya masikini Tanzania (TASAF) kutokana na ubaguzi wanaoufanya kwa watu wenye ulemavu pindi wanapofika mitaani kwa lengo la kuwasaidia wananchi ambao waishi katika mazingira magumu nakuwaomba viongozi hao kuachana na tabia kwani inawaumiza sana watu wenye ulemavu.
Akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo mratibu wa mfuko wa kunusuru kaya masikini Tanzania (TASAF) Mussa Said Kisenge amesema hakuna ubaguzi wowote katika utoaji wa misaada hiyo bali wanaangalia hali na uhitaji wa mtu.
“Sisi tunafata utaratibu unavyoturlekeza hatufanyi kazi kiupendeleo Kama mtu ana vigezo vyote vyakuingizwa kwenye system basi tunamuingiza tu na jukumu Hilo linamfanya na Sheha wa Shehia husika kwakushirikia na wananchi sisi kazi yetu ni kumuingiza muhusika katika orodha” alifafanu
Jumuiya ya watu wasioona Zanzibar (ZANAB) ilianzishwa Rasmi January 1 mwaka 1993 Kwa lengo la kuwaunganisha pamoja watu wenye Ulemavu wa Macho, kuwa na Sauti mmoja ili kuweza kutambuliwa na kupatiwa haki zao Msingi Visiwani Zanzibar.