NA HASSAN MSELLEM-PEMBA.
Jumuiya ya watu wenye ulemavu wasioona ZANAB wameiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani ili kulinda usalama wa watu wasio ona.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya mwaka kuanzia Januari hadi Disemba huko ofisini kwao Chake Chake katibu wa Zanab Bi. Rehema Vuai Ali amesema baadhi ya madereva wanadharau fimbo nyeupe zinazotumiwa na watu wasiona wakiwa barabarani na kuwasababishia usumbufu mkubwa ikiwemo kuwagonga.
Amesema watu wenye ulemavu wanahaki sawa na watu wengine hivyo ni vyema kuheshimu sheria za usalama barabarani zinazowalinda watu hao.
‘’Tathmini inaonesha watu wenye ulemavu wa macho 22 Wamekutwa na kadhia mbali mbali wakati wakiwa barabarani katika mkoa wa Kusini Pemba kuanzia Mwezi January hadi Disemba na wanaosababisha kadhia hizi kwa kiasi kikubwa ni madereva wa daladala na bodaboda’’ alisema
Nae mwenyekiti wa Zanab Kisiwani Pemba Suleiman Mansour Suleiman amesema jumuiya hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ufinyu wa ofisi pamoja na ukosefu wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zake, hivyo basi ameiomba Serikali kutenga fungu maalum kwa ajili ya kuisaidia jumuiya hiyo.
‘’Mheshimiwa katibu ZANAB tunakabiliwa na changamoto nyingi sana lakini changamoto kuu ni ukosefu wa eneo la kutosha kwa ajili ya ofisi tuna kijichumba kimoja kisichozidi futi sita tunakwekwenezana humo humo kike kiume, kitu chengine pesa hatuna muda mwengine hata nauli ya kuja kazini zinatushinda sueze za kuendesha shughuli nyengine kwahivyo tunaiomba Serikali itenge fungu maalum kwa ajili yetu’’ alieleza
Akifungua kikao hicho katibu tawala wilaya ya chakechake Bw. Omar Juma Ali ameitaka jumuiya ya zanab kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali ikiwemo mikopo kwa ajili ya wanachama wao.