MARYAM SALIM HABIB,PEMBA.
Waziri wa utalii na mambo ya kale Zanzibar Leila Mohammed Mussa
amewataka wananchi wa kijiji cha Mleteni na vitongoji vyake
kuhakikisha wanaitumia vyema na kulinda miundombinu ya umeme kwa
maendeleo.
Wito huo ulitolewa na Waziri huyo kwa niaba ya Waziri wa ujenzi
mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Rahma Kassim Ali wakati
akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mleteni na vijiji vyengine
jirani katika uzinduzi miundombinu hiyo ukiwa ni shamrashamra za
kuadhimisha Mapinduzi matukufu ya Januari 1964.
Leila alisema kuwa Mapinduzi matukufu ya Januari 1964 wananchi wajue
kwamba ndio yalioanzisha chachu na mwanga juu ya mapambano ya haki za
msingi kwa wazanzibar wote.
“Katika kuhakikisha kwamba wananchi wanafaidika na Mapinduzi hayo
matukufu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejiwekea mikakati imara
yakuona wanawapatia wananchi wake huduma mbali mbali muhimu za kijamii
karibu na maeneo yao bila ubaguzi” alisema Waziri Leila.
Alifahamisha kuwa Serikali imehakikisha huduma zote muhimu
anazostahiki mwanadamu anazipata zinawafikia karibu na maeneo yao
wanayoishi bila yakuwepo na chembe yoyote ya ubaguzi wa
kisiasa,dini,kabila na itikadi nyengine.
Alieleza kuwa Mapinduzi matukufu ya 1964 ni vyema wananchi kuelewa
kuwa ndio msingi wa uliowafanya wananchi wa nchi husika wanaondokana
na ubaguzi wa shuhuli za kimaendeleo.
“Kama tunavyoelewa kabla ya Mapinduzi jamii zetu huduma zote muhimu
zilizokuwa zikitolewa zilikuwa zilitoka kwa ubaguzi,” alisema Waziri
huyo.
Alisema kuwa Serikali ipo katika shamra shamra za kuadhimisha siku ya
Mapinduzi matukufu kwa Unguja na Pemba, kwa kuzindua miradi mbali
mbali ya kimaendeleo ikiwa ni ishara ya juhudi ya mafanikio makubwa za
ukombozi ambazo zilipelekea kufanyika kwa Mapinduzi hayo.
Hivyo waziri Leila alieleza kutokana na juhudi za makusudi
zilizofanywa na waasisi waliopita juu ya kuwapatia maendeleo wananchi
wake, ipo haja kwenu wananchi wa Mleteni na vijiji vyengine kuitumia
vyema fursa mtakazopatiwa kwa maendeleo.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatibu,
katika shamrashamra za ufunguzi wa huduma ya umeme kijijini hapo
alisema lengo la waasisi wa Mapinduzi matukufu ya 1964 walikubaliana
kwamba nchi ya Zanzibar iendelezwe kwa kuthamini matunda na dhamira
ya Mapinduzi ,hivyo suala la umeme ni miongoni mwa matunda yenyewe.
“Katika Kijiji cha Mleteni ni miongoni mwa vijiji ambavyo vilibahatika
kufikiwa na ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi na hapo ndipo Rais kutoa tamko kwamba kijiji hicho kiweze
kufikishiwa huduma zote muhimu kama wanavyopatiwa wengine na hayo ndio
matumizi mazuri ya Mapinduzi,” alisema Salama.
Alieleza thamani ya Mapinduzi ni kuona kila mmoja anatumia matunda
hayo bila ubaguzi wowote, kwa maendeleo endelevu ndani ya nchi.
Salama aliwataka wananchi hao kuhakikisha miundombinu hiyo wanaitumia
na kulinda ipasavyo kuhakikisha lile lengo lilokusudiwa linafikiwa.
Mapema Katimu mkuu Wizara ya maji, Nishati na Madini Dk, Mngereza Mzee
Miraji katika uzinduzi huo alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
katika kutekeleza majukumu yake mnamo September mwaka 2020 Rais
Mwinyi alifika katika kijiji hicho akiwa na ziara yake ya mikoa
miwili ya Pemba kutoa neno la shukran baada ya kuchuguliwa na
kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi
“Katika kusikiliza changamoto za wanakijiji hao na vijiji vyengine
jirani miongoni mwa changamoto aliopatiwa ilikua ni Umeme, Skuli na
Barabara ambapo kwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu tatizo la umeme
limeondoka,” alisema.
Alieleza katika lengo la Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ni
kumkomboa mwananchi katika suala la maendeleo na sio vyengine na ndio
Serikali ya Mapinduzi ikaendeleza hayo.
Alifahamisha kuwa kutokana na tamko la Serikali juu ya kufikisha kwa
huduma ya umeme kijijini hapo,ndipo Wizara ya Maji, Madini Nishati na
umeme kwa kuungana na Serikali imehakikisha inatekeleza ahadi ya Rais
kuona ndani ya kipindi kichaçhe linafanyiwa kazi kwa maendeleo.
“Ikizingatiwa shuhuli kuu zinazofanywa kijijini hapa na vitongoji
vyake vyengine imechukua juhudi za makusudi kukamilisha kwa haraka
huduma hiyo, ili kwenda sambamba na malengo ya Serikali ya awamu ya
nane katika kuboreshwa uchumi endelevu,” alieleza.
Akitowa taarifa ya kitaalamu Dk, Mngereza alisema kuwa huduma ya umeme
na usambazaji katika Kijiji cha Mleteni umegharamiwa na Serikali ya
Mapinduzi kupitia shirika la Umeme (ZECO)Zanzibar,ili kuondosha
usumbufu wakufuata huduma hiyo muhimu kwenye maeneo mengine mbali na
kijiji chao.
“Kazi ya usambazaji umeme katika Kijiji cha Mleteni chenye nyumba 39
imegharimu shilingi milioni 123.45 ambapo ni kwa kazi ya usambazaji
ya miundombinu hiyo kijijini hapo iliojumuisha jumla ya maeneo
mbalimbali, ambapo jumla ya nyumba 6 kati ya hizo tayari zimeshaungiwa
huduma hiyo kwa maendeleo endelevu,” alifahamisha.
Hata hivyo kwa upande wa wananchi wa kijiji hicho waliipongeza
Serikali ya Mapinduzi chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Mwinyi kwa utekelezaji wa ahadi yake
kwa vitendo na kuahidi kwamba watatumia miundo mbinu hiyo kwa malemgo
yaliokusudiwa.