PEMBAWAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Dk, Soud Nahoda Hassan Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , kwenye Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk, Hussein Ali Mwinyi inaendelea kuthamini kulinda matunda ya Mapinduzi ya Januari 1964 kwa kuwapatia wananchi wake huduma muhimu ikiwemo huduma ya elimu karibu na maeneo yao.Kauli hiyo ilitolewa na Waziri huyo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Skuli ya maandalizi ya Matangatuani Wilaya ya Micheweni Mkoa wa kaskazini, ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 58 ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.Alisema kuwa Serikali ya awamu ya nane inafanya juhudi za makusudi ili kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa kuwapatia wananchi huduma mbali mbali muhimu karibu na maeneo yao wanayoishi ili kuondosha usumbufu wanaopata.“Miongoni mwa huduma zinazotolewa kwa jamii ni pamoja na miundombinu ya maji, barabara, umeme, Elimu ,Afya na nyengine muhimu ambazo zinahitaji kupatiwa mwanadamu katika maisha ikiwa ni matunda ya Mapinduzi hayo,” alisema Waziri huyo.Alieleza kuwa lengo la Mapinduzi matukufu ni kuhakikisha inawawekea wananchi wake katika mazingira mazuri ambayo yatawaletea maendeleo ya taifa kwa ujumla.“Serikali yenu imefuta michango yote kuanzia maandalizi hadi Sekondari kama ilivyo azma ya Mapinduzi hayo ya kila mtoto aweze kupata haki zake za msingi za kielimu kwa maendeleo, yote hayo ni kutahmini na kuenzi matunda ya Mapinduzi,” alieleza.Alisema kuwa Serikali imeimarisha miundombinu ya Elimu kwa kujenga skuli za kisasa kwa Unguja na Pemba,na kuzipatia vifaa vyote muhimu ili wanafunzi waweze kujifunza vizuri kwa maendeleo.Alifahmisha kuwa sera ya elimu ya mwaka 2006 inaelekeza kuwapatia elimu ya maandalizi watoto wote kuanzia miaka 4, lengo ni kuona kila mtoto anapata haki yake ya msingi ya elimu kwa wakati maalum.“Ingawa Serikali inafanya jitihada juu ya kuboresha elimu mijini na Vijijini, bado kumekuwa na changamoto ya kufeli kikubwa kwa masomo ya sayansi na hesabati na uhaba wa skuli za maandalizi na madrsa hasa vijijini, jambo ambalo hupelekea watoto kufuata huduma hiyo masafa makubwa kutoka maeneo wanayoishi,” alisema.Alisema kutokana na changamoto hiyo ya muda mrefu ya wananchi wa Matangatuani kukosa Skuli ya maandalizi karibu na makaazi yao, Serikali imeliona hilo kwa kuwajengea Skuli hiyo ya karibu na eneo lao ili kuondosha usumbufu wanaopata watoto.Hivyo alitoa wito kwa wananchi hao kuwataka wananchi wa Shehia hiyo kuienzi na kuithamini miundombinu hiyo, ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa maendeleo na kuwa chanzo cha kutoa wataalamu zaidi kwa maendeleo, hilo ndio lengo la Mapinduzi matukufu.Nae Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mgeni Yahya Khatib kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo Salama Mbarouk Khatib alisema kuwa miongoni mwa malengo ya matunda ya Mapinduzi ni kuondoa adui ujinga kupitia elimu.“Uwepo wa Skuli ya maandalizi Matangatuani itakuwa chachu kwa watoto wa shehia hiyo na vitongoji vyake ya kujipatia elimu karibu na eneo lao, ili kuondokana na usumbufu wanaopata wakufuata huduma hiyo mbali na mazingira yao,” alisema mkuu wa Wilaya.Mkuu huyo aliwataka wananchi kuendelea kutoa mashirikiano na uongozi wa walimu wa skuli hiyo ili kufikia lengo lililokusudiwa.Mapema Katibu mkuu Wizara ya Elimu Zanzibar Ali Khamis Juma, wakati akisoma ratiba ya kitaalamu katika shamra shamra ya ufunguzi wa skuli hiyo alisema kuwa ujenzi wa skuli hiyo ulitokana na mwamko wa wananchi wa eneo husika na kuomba uongozi wa Wizara kuwajengea Skuli kutokana usumbufu wanaopata watoto wao.“Kutokana changamoto wanaopata watoto wa shehia ya Kifundi kufuata huduma ya elimu Konde ambapo ni kutoka kwenye shehia hiyo hadi Konde ni kilomita 4, jambo ambalo lilikuwa ni hatarishi kwa watoto kutokana vitendo vya udhalilishaji vilivyoshamiri,” alisema katibu huyo.Wizara ilikubaliana na ombi na ndipo kujenga skuli ya maandalizi yenye madarasa mawili, Ofisi moja na vyoo, ili watoto waondokane na usumbufu wanaopata.Aidha alisema kuwa Skuli hiyo inatarajiwa kuanza na watoto 120 wakiwemo watoto wa kike 54 na wakiume 66,ujenzi wa skuli hiyo hadi kukamilika kwake uligharimu jumla ya shilingi 56 Milioni zote hizo zilitolewa na wizara ya elimu kwa msaada wa wahisani wa maendeleo.Alieleza kukamilika kwa ujenzi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya hatari kwa watoto wadogo kwa kufuata elimu masafa marefu.Katibu huyo alisema kuwa kutokana na watoto kila siku kuongezeka kwa madarasa mawili hayatoshi, hivyo kuwa na mpango wa kuongeza madarasa mengine manne, ili watoto wapate elimu katika shehia yao bila usumbufu.Kwa upande wake Zakia Omar Khamis mwalimu mkuu wa Skuli hiyo aliwataka wazazi kutoa mashirikiano ya kutosha ili kufikia lengo lililokusudiwa na Serikali ya Mapinduzi hayo.Hata hivyo , aliomba Serikali pamoja na wizara husikaiweze kuwaendeleza kielimu, kuwapatia vifaa vya kisasa vyakusomeshea. Share