NA ZUHURA JUMA, PEMBA.
SHEHIA tano za Wilaya ya Wete Pemba zimekabidhiwa boti kwa ajili ya uimarishaji wa doria, ili kuhakikisha matumizi endelevu na usalama wa rasilimali za bahari ambazo ni tegemezi katika kunufaisha maisha ya jamii.
Akizungumza katika mkutano wa kukabidhi boti hizo kwa wananchi katika bandari ya Ukunjwi, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Abdalla Hussein Kombo alisema, hatua hiyo inaendana sambamba na dhana ya uchumi wa Buluu katika kuimarisha usalama wa chakula na upatikanaji wa lishe bora kupitia usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari.
Alisema kuwa, kuwepo kwa boti hiyo kutasaidia kuziwezesha jamii hasa wanawake na vijana kutumia fursa zinazotokana na uchumi wa Buluu katika kujiendeleza kiuchumi.
“Mambo yote haya hayatawezekana pasi na kuwepo mazingira salama ya bahari, ikiwemo kujiepusha na Uvuvi unaoathiri uwepo wa rasilimali kama samaki, matumbawe, majani ya bahari, viumbe waliohatarini kitoweka, misitu ya mikoko na mikandaa”, alisema Waziri huyo.
Alizitaka Shehia hizo kushirikiana pamoja ili kujenga mazingira Bora ya uchumi wa Buluu kupitia sekta mbali mbali ikiwemo utalii, kukuza kipato cha mvuvi mmoja mmoja na maendeleo ya jamii za wavuvi kwa ujumla.
“Nimeambiwa kuwa awali kumeshafanyika mafunzo ya doria ya nadharia na vitendo, ili kujenga utimamu kwa wajumbe wa kamati za Uvuvi za shehia ya Mtambwe, Selem, Gando, Fundo na Ukunjwi zilizounda eneo la usimamizi wa pamoja”, alisema.
Mapema akizungumza katika mkutano huo Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya kutuma na kisimamia rasilimali za bahari kwa Jamii (MCCC) Ali Khamis Thani alisema, Kampuni yao kwa kushirikiana na Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na mazao ya Baharini, ilianza kuwajengea uwezo wavuvi tangu mwaka 2014 na kuishajihisha jamii katika uhifadhi.
“Tunawawezesha wanajamii kuandaa mipango midogo ya usimamizi wa rasilimali kwenye maeneo yao, kufanya tathmini na ufuatiliaji wa ndani ya maji, ufuatiliaji wa mwenendo wa upatikanaji wa pweza na samaki kupitia ukusanyaji wa taarifa za mapato ya mazao hayo”, alisema Afisa huyo.
Alieleza kuwa, matarajio yao ni kwamba boti hiyo itawasaidia wanajamii kuweka usalama mzuri wa rasilimali zao zinazoendelea kitishiwa na suala la uvuvi haramu wa zana mbali mbali zinazokatazwa na sheria ya Uvuvi, ili kufika usimamizi endelevu.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati Tendaji Hifadhi ya Bahari Khamis Sharif Haji aliwataka wanashehia hizo kushirikiana pamoja katika kuhakikisha wanayalinda mazingira sambamba na kuitunza boti hiyo ili idumu kwa muda mrefu.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Uvuvi Shehia ya Fundo Said Omar Ali alisema, ni faraja kwao kupata boti hiyo kwani itawasaidia kudhibiti uharibifu katika maeneo ya baharini ambao unafanywa na baadhi ya wavuvi wanaotumia bunduki na nyavu za kukokota.
Sheha wa shehia ya Ukunjwi Mkongwe Kasanje Khamis alieleza kuwa, atatoa ushirikiano na kisimamia katika kuhakikisha lengo lililokusudiwa linafanikiwa.
Boti hiyo pamoja na vifaa vya doria vimetolewa na Kampuni ya MCCC pamoja na Shirika la Wild Aid.