NA ZUHURA JUMA, PEMBA
JUMLA ya watu 4,396 kisiwani Pemba wameripotiwa kuugua ugonjwa wa sukari kwa mwaka 2020 na mwaka 2021.
Kati ya wagonjwa hao, wanaume ni 1,452 na wanawake ni 2,944 ambapo mwaka 2020 wagonjwa walioripotiwa ni 1,883 na mwaka 2021 ni wagonjwa 2,513.
Akizungunza na mwandishi wa habari hizi Mratibu wa maradhi yasioambukiza Pemba dk, Yussuf Hamad Iddi alisema, mwaka 2020 katika mkoa wa Kaskazini Pemba wamepokea wagonjwa wa kisukari 1,193 na Kusini wamepokea wagonjwa 696.
Alisema kuwa, mwaka 2021 Mkoa wa kaskazini Pemba walipokea wagonjwa wa kisukari 1,343 ambapo mkoa wa Kusini walipokea wagonjwa 1,170.
Dk. Yussuf alisema kuwa, mwaka 2021 idadi ya wagonjwa imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2020 kutokana na wananchi kupima afya zao kwa wingi.
“Mwaka 2020 wananchi walikuwa hawaendi hospitali kupima afya zao, kwani walikuwa wanahofia kuambiwa wana ugonjwa wa Corona, lakini mwaka 2021 walikuwa wanakuja kwa wingi na ndipo tukagundua wagonjwa wengi”, alisema Mratibu huyo.
Aidha alifafanua kuwa, kati ya wagonjwa hao walioripotiwa, idadi ya wanawake imekuwa kubwa ikilinganishwa na wanaume kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo kutokufanya mazoezi.
“Kati ya wagonjwa hao 4,396, wanawake ni 2,944 na wanaume 1,452, ambapo mwaka 2020 wanawake ni 1,883 na wanaume ni 650 na mwaka 2021 wanawake ni 1,711 na wanaume 802”, alisema dk Yussuf.
Aliwataka wanajamii wafanye mazoezi kila siku kwa muda wa nusu saa, kwani yanajenga afya na huepusha magonjwa mbali mbali yakiwemo ya kisukari.
“Jamii ielewe kwamba mazoezi na kufanya kazi ni vitu viwili tofauti, kwa sababu wengine wakimaliza kufanya kazi wanasema wameshafanya mazoezi, waache dhana hiyo”, alisema.
Watu wanaougua magonjwa yasioambukiza wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku, huku Serikali igipigania kuondosha magonjwa hayo, ili kuwa na Taifa lenye afya bora.