Thursday, January 16

Mhe Hemed azungumza na Mabalozi walioteuliwa karibuni

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika mataifa mbali mbali waliofika Ofisini kwake Vuga kwa ajili ya kumuaga.

Na Kassim Abdi, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewahakikishia mabalozi walioteuliwa na kupangiwa kazi katika mataifa mbali mbali kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano katika kufanikisha vyema majukumu yao.

Mhe. Hemed alieleza hayo wakati mabalozi hao walipofika Ofisini  kwake Vuga kumuaga  kwa ajili ya kwenda kuiwakilisha Tanzania katika Nchi zao walizopangiwa.

Aliwaeleza Mabalozi hao kuwa, tumaini la watanzania lipo juu yao hivyo, hawana budi kufanya kazi zao kwa kuimarisha ustawi wa uchumi wa Taifa la Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais alisema ana Imani kubwa na uwezo walionao mabalozi hao jambo ambalo litatoa tija katika suala zima la kuwavutia wawekezaji kuja kekeza nchini kwa lengo la kujenga uchumi imara wa Nchi yetu.

Alieleza kuwa, Watanzania wataendelea kuwaombea huku akiwahakikishia ushirikiano wa karibu kutoka serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kufanikisha kazi zao za kila siku.

Nae, Kiongozi wa msafara huo Balozi Perera Ame Silima anaekwenda kuiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Visiwa vya Comoro alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais kuwa, watayafanyia kazi maelekezo na maagizo alioyatoa kwa maslahimapana ya ustawi wa Tanzania.

Mabalozi waliofika kumuaga Makamu wa Pili wa Rais wanakwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Brazili, Congo, Israil, Urusi, Quwait na Umoja wa Visiwa vya Comoro.