Thursday, January 16

SUALA la kudumisha amani linapaswa litawale katika mfumo wa maisha ya kila siku ya mwanadamu-Msaidizi wa katibu wa Mufti Pemba .

 

  NA ABDI SULEIMAN.

 

SUALA la kudumisha amani linapaswa litawale katika mfumo wa maisha ya kila siku ya mwanadamu, ili waweze kujizuia pale wanapokumbana na viashira ambavyo vinaweza kusababisha migogoro.

 

Hayo yameelezwa na Msaidizi wa katibu wa Mufti Pemba shekhe Said Ahmad Mohamed, mjini Chake Chake wakati akiwasilisha mada ya njia sahihi zinazofaa kutumiwa katika kutatua migogoro na ujenzi wa amani, kwenye kongamano la siku mbili la vijana, wanawake na viongozi wa dini wa mkoa wa kusini Pemba.

 

Alisema katika maisha yapo makundi tofauti yenye misimamo tofauti, lakini yanapaswa kuwa na misingi ambayo inafuata dini zao ili kuondosha hitilafu zao katika mambo ya kidunia.

 

Alifahamisha kuwa suala la utunzaji wa amani ni jambo la muhimu kwa wananchi, ili kuondokana na jamii iliyopandikizwa itikadi na mitazamo tafauti yao.

 

“Katika jamii tunayoishi tunakuwa na migongano na migogoro, ambaypo haiwezi kuepukika, dini ni mfumo na utaratibu wa maisha uliowekwa na muumba ili kuweza kufahamu maisha ya mwanadamu, vizuri kufuata matakwa hayo ya muumba ili tuishi salama”alisema.

 

Akielezea lengo la kongamano hilo mratibu wa mradi wa dumisha amani na katibu wa jumuiya ya PECEO Juma Said Ali, alisema lengo ni kuijengea jamii misingi imara ya kutatua migogoro pale inapotokea katika maeneo yao.

 

Juma alisema katika jamii kumekua kukijitokeza migogoro mingi ambayo mwisho wake inapelekea uvunjifu wa amani, hivyo ujio wa mradi huo utaweza kuwasaidia wanajamii, kujua njia sahihi za utatuzi wa migogoro pale inapotekea.

 

Hata hivyo aliwataka viongozi wadini kuwa mabalozi wakubwa kwa jamii na vijana, katika kuhakikisha amani ya nchi inaendele kudumishwa.

 

Kwa upande wa washiriki wa kongamano hilo wamesema kupotea kwa malezi ya zamani, sambamba na kukosekana kwa mashirikiano na upendo yanasababisha migogoro miongoni mwa jamii.

 

Msimamizi wa vijana Wilaya ya Chake Chake Stara Khamis Salim, alisema mchango wa vijana katika kupunguza uvunjifu wa amani, ni kuendelea kutoa elimu kwa vijana licha ya kuwa ni changamoto kubwa kwao.

 

Aliyomba serikali na wadau wa maendeleo kuwa na muda au wakati maalumu kuwapatia vijana elimu juu ya suala hilo, katika kipindi chote na sio kipindi cha uchaguzi pekee.

 

Said Omar Saidi alisema vijana ndio chanzo cha uvunjifu wa amani kutokana na kukosa elimu ya kutosha jambo ambalo linapaswa kupigiwa kelele na wadau wote.

 

Naye Abdalla Ali Mohamed alisema malezi yaliyopo sasa kwa watoto ni tatizo, jamii imesahau malezi ya pamoja kwa watoto lazima vijana watabadilika na kutokufuata malezi ya wazazi wao.

 

Kwa upande wake Mkadamu Makame alisema suala la utandazi wa kidunia, linachangia katika uvunjifu wa wamani vijana wamekuwa ni watumiaji wakubwa wa simu za kisasa na utumiaji wa vileo, mwisho wake wanaingia katika vitendo ambavyo haviendani na maadili yao.

 

Kongamano hilo limeandaliwa na jumiya ya PECEO kupitia utekelezaji wa mradi wa dumisha amani Zanzibar, wakishirikiana na Foundation for civil society na Search for common groud, kwa ufadhili wa umoja wa nchi za ulaya.