RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ufunguzi wa madarasa katika Skuli ya msingi Sebleni, ni kielelezo cha dhamira ya Serikali katika kukabiliana na changamoto ya miundombinu inayozikabili skuli mbali mbali hapa nchini.
Dk. Mwinyi amesema hayo katika hafla ya Ufunguzi wa Madarasa sita ya Skuli ya Msingi Sebleni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema ujenzi wa madarasa hayo uliofanyika kwa mashirikiano kati ya Serikali, Viongozi wa Jimbo na wananchi ni miongoni mwa juhudi za kuzifanyia kazi changamoto mbali mbali zinazokabili skuli hapa nchini.
Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha watoto wote nchini; Mjini na vijijini wanatumia haki yao ya kupata elimu katika mazingira bora.
Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi na walezi kusimamia na kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao ili kuhakikisha wanatumia vyema fursa ya kupata elimu.
Dk. Mwinyi alisema ana imani ujenzi wa madarasa hayo utapunguza tatizo la msongamano wa wananfunzi katika madarasa na kuwapatia mazingira bora ya kujifunzia.
Alieleza kuwa ongezeko la idadi ya watu nchini sambamba na kukuwa kwa makaazi, kumeongeza mahitaji ya majengo ya skuli pamoja na mahitaji zaidi ya madarasa, hivyo kuilazimu Serikali kwa kushirikiana na wananchi na Viongozi wa Jimbo la Kwahani kujenga Skuli za Amani na Sebleni ambazo kabla hazikuwepo.
Alisema katika kipindi cha miaka 58, Serikali imefanya juhudi kubwa ya kuongeza idadi ya skuli ili kutoa fursa kwa wanafunzi wengi zaidi mjini na vijijini ili kupata haki yao ya msingi ya elimu.
Akizungumzia Historia ya sekta ya Elimu hapa nchini, Dk. Mwinyi alieleza kuwa kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Zanzibar ilikuwa na jumla ya skuli 69 pekee katika ngazi mbali mbali; na kubainisha kuwa skuli mbili zilikuwa za ngazi ya maandalizi zilizoandikisha wanafunzi 60 , skuli 62 za msingi pamoja na skuli tano za Sekondari.
Alisema hadi kufikia Disemba mwaka 2021, Zanzibar ilikuwa na skuli za maandalizi 774, skuli za msingi 545 pamoja na skuli za Sekondari 302 zikiwa na jumla ya wanafunzi 552,328; ikilinganishwa na wanafunzi 25,432 waliokuwepo kabla ya Mapinduzi ya 1964.
Alisema katika mazingira ya namna hiyo, ni dhahiri kuwa mahitaji katika utopaji wa elimu yataongezeka, na hivyo akabainisha dhamira ya serikali katika kukabiliana na changamoto mbali mbali ikiwemo ya miundombinu, uhaba wa walimu, vitabu na ukosefu wa vikalio.
Alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto (UNICEF) pamoja na Taasisi ya “Education above all” ya kutoka nchini Qatar imesaini mkataba wa mradi unaogharimu Dola za Kimarekani Milioni tatu, ukiwa na lengo la kusaidia kuwarejesha skuli watoto wenye umri kati ya miaka 7-14 walio nje ya skuli rasmi.
Aidha, alisema Serikali itaendeleza kuunga mkono juhudi zinazoanzishwa na Viongozi na Wananchi za ujenzi wa miundombinu mbali mbali ya elimu ili kufikia dhamira hiyo ya Serikali.
Rais Dk. mwinyi alieleza kuwa Serikali kupitia Fedha za Mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) imedhamiria kutumia sehemu ya fedha hizo kwa ajili kupunguza changamoto za upungufu wa madarasa, kwa kujenga madarasa mapya 1,131, yakiwemo yale yalioanzishwa kwa nguvu za wananchi pamoja na kujenga madarasa mengine mapya.
Alisema Serikali itazifanyia ukarabati skuli za msingi na Sekondari na kujenga Vyoo 1963 katika skuli mbali mbali Unguja na Pemba, sambamba na kujenga Nyumba kumi za Walimu katika visiwa vidogo vidogo, pamoja na kununua madawati 8,000 kwa ajili ya wanafunzi 24,000 wa skuli za msingi.
Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Simai Mohamed Said, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusema pamoja na kupitia changamoto ya Kilimwengu ya kuwepo kwa Ugonjwa wa Uviko -19, Serikali ilifanikiwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wote wa sekta ya elimu, ambapo asilimia 20 ya Fedha za Bajeti huelekezwa katika sekta hiyo.
Alisema maendeleo makubwa yanayoonekana kupitia sekta hiyo yanatokana na umoja na amani iliopo hapa nchini.
Aidha, Mbunge wa Jimbo la Kwahani CCM Ahmada Yahya Abdul-wakil (Shaa) alisema madarasa yaliofunguliwa ni juhudi na maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduiz DK. Hussein Ali Mwinyi, ambapo alikuwa Mbunge wa Jimbo hilo katika kipindi cha mwaka 2015-2020.
Alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha jengo la Ghorofa skulini hapo ikiwa ni hatua ya kupanua wigo kwa wanafunzi wengi zaidi kusoma na kuondokana na changamoto ya uhaba wa madarsa unaoikabili Zanzibar.
Vile vile, Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani, Yahya Rashid Abdalla aliishukuru Serikali, Viongozi na wananchi wote waliochangia na kufanikisha ujenzi huo, akibainisha hatua hiyo inadhihirisha matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.
Rashid, aliwataka wananchi wa Jimbo hilo kujiandaa na kushiriki kikamilifu katika uandikishaji wa zoezi la Sensa, pale wakati utakapowadia ili kupata takwimu sahihi na kuchochea maendeleo.
Katika hatua nyengine, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , chini ya Uongozi wa Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake za kuendelea n ujenzi wa majengo ya madarasa.
Aidha, Risala ya Uongozi wa Jimbo hilo ilibainisha Ujenzi wa madarsa hayo sita katika Skuli ya Msingi Sebleni, uliotokana na wazo la Rais Dk. Mwinyi, umegharimu shilingi Milioni 158 zinatokana na michango ya Serikali, Viongozi wa Jimbo pamoja na nguvu za Wananchi.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari, Ikulu Zanzibar.