NA ABDI SULEIMAN.
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi Taifa na ,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi na walezi nchini kusimama na kuendelea kuwalea Vijana wa Kitanzania katika maadili mema kwani ndio tegemeo kubwa na nguvu kazi ya Taifa lolote Duniani.
Alisema Serikali imekuwa ikiwathamini sana vijana kutokana na umuhimu wao kwa maendeleo ya Taifa na inafanya mbinu mbali mbali ya kuwafanya vijana kupata ajira zikiwemo za kujiajiri wenyewe kwa kuwanzishia miradi na kuwapatia mikopo mbali mbali.
Aliyaeleza hayo huko katika kiwanja cha mpira cha Makombeni Wilaya ya Mkoani Pemba, wakati akiwahutubia vijana wa Tanzania walitembea kilo mita 129.1 kwa ajili ya kuyaenzi Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 sambamba na kuyafunga matembezi hayo.
Mama Samia alitowa pole kwa wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba kutokana na msiba wa kupoteza jamaa zao waliozama na boti wakiwa katika harakati za kuvuka ng’ambu moja kwenda nyengine kwa kufuata huduma .
Aliwaomba wananchi hao kuwa na subra katika kipindi hicho kigumu na Serikali imeguswa na msiba huo ambao ni mkubwa na iko pamoja nao.
“Nawaomba kila mmoja asimame na wawaombee kila mtu kwa imani ili wale majeruhi kama wapo waliolazwa Haspitali wawaombee wapone haraka,”alieleza.
Alifahamisha kuwa taifa linategemea sana Vijana katika usalama na maendeleo ya nchi hivyo lazima wafuate malezi mema wanayopewa na walezi wao ili kupambana na changamoto mbali mbali zinazowakwaza.
Rais Samia ambae pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa, aliwataka vijana hao kutumia fursa mbali mbali zinazojitokeza ikiwemo zile za uchumi wa buluu ili waweze kujipatia vipato vyao vya halali na kukuza uchumi wa nchi yao.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetenga fedha nyingi billion 85.4 kwa ajili ya vijana hivyo ni wajibu wao kuzitumia fedha hizo katika maeneo hayo kwani bidhaa za baharini zinasoko kubwa katika masoko ya kimataifa.
“ Tumieni fursa ya Uchumi wa Buluu kama ilivyo kauli mbiu ya Sherehe za miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuekeza katika mazao ya baharini kama vile ufugaji wa kaa na samaki na kuwapeleka katika nchi mbali mbali ili muweze kuendesha maisha yenu na kujipatia ajira,”alisema.
Alitowa vito kwa Vijana na wazee kutumia fursa zinajitokeza za kuomba mikopo mbali mbali kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia suala la mabadiliko ya tabia nchi Rais Samia aliwataka Vijana hao kutumia fursa hizo za kimazingira kwa kuzaa mbinu mbali mbali za uhifadhi kwa kujiimarisha kiuchumi na kuepusha maji ya bahari kupanda juu.
Alisema sasa hivi maeneo mengi yameshaathiriwa na mabadiliko hayo ikiwemo Unguja , Pemba na Tanga kutokana na uharibifu wa mazingira jambo linasababisha maeneo baadhi ya maeneo maji ya bahari kupanda katika maeneo ya makaazi au ya Kilimo.
“ Tayari Serikali imeshachukuwa juhudi mbali mbali za kuzuwia maji hayo kupanda juu ikiwemo kupiga matuta ya kuzuwia maji hayo kwa unguja na Pemba lakini endeleeni kuchukuwa tahadhari ili kuweza kukabiliana na hali hiyo,”alieleza.
Hata hivyo mama Samia, aliwaomba Vijana kujitokeza katika kuchanja chanjo ya Uviko 19 kwani inakinga kubwa ya ugunjwa huo na haina madhara kama inavyoelezwa.
Alifahamisha kuwa sio kuwa mtu anapochanja hawezi kupata maradhi ya Uviko 19 lakini chanjo hizo zinapunguza makali ya maambukizo .
Alisema vijana wamesifu sana Rais Samia kwa kusimamia Chanjo hiyo kwa kujitokeza kuchanja hadharani , lakini jee na wao wamechanja au wanasifu tu.
Aliwahimiza vijana hao kuwa na ushiriki mkubwa wa zoezi la Sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika hapo baadae kwani ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Alisema Serikali ili inaweze kutekeleza majukumu yake inahitaji kuwa na idadi kamili ya watu hivyo Vijana washiriki na wahamasishe watu wengine kushiriki katika zoezi hilo.
Akizungumzia suala la Uchaguzi wa Chama na Jumuiya zake Mwenyekiti huyo wa Chama cha Mapinduzi Taifa, Samia Suluhu Hassan aliwasihi vijana kutokubali kugeuzwa ngazi ya kupandia juu kwa wanaotaka uongozi bali wajitokeze kugombea nafasi hizo wenyewe.
Alisema kuna baadhi ya watu huwafanya vijana kuwa ngazi zao za kupanda juu katika uongozi na kuwapa nafasi watu wasionasifa na hatimae kutowatendea yale waliowaahidi.
“ Kuna baadhi ya watu huwadanganya Vijana kwa kuwapatia mambo mbali mbali pale wanapotaka uongozi lakini baada ya kupata huwasahau hao tambueni hawana imani na nyinyi na wengekuwa na imani nanyi basi changamoto mbali mbali zinazowakabili zisengekuwepo,”alieleza.
Aliwataka vijana kwenda kugombea na wasikubali kuwabeba watu wengine na wasimame kwa kufuata sheria na kanuni za chama kwa kujiepusha na rushwa na kupiga vita vitendo vyote vya udhalilishaji katika kipindi cha Uchaguzi.
“ Inapofika wakati wa Uchaguzi kama huu sisi wenye watoto wa kike huwa tuna wasiwasi juu ya vitendo vya udhalilishaji lakini Chama kikikubaini na vitendo hivyo hutobaki salama , hatutotizama sura tutaangalia sifa za mtu,”alieleza.
Aliwasihi Vijana hao waende kukijenga chama chao cha Mapinduzi na wasiwe tayari kukubali kutumiliwa kukipasua Chama .
Aidha Mwenyekiti huyo wa Chama cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alieleza kuwa Ukombozi wa Mapinduzi umeshapita zamani na uliopo sasa ni ukombozi wa maendeleo hivyo wawe tayari kupigania maendeleo yao.
Aliwataka vijana kukaa na kujitathmini yale waliyoeleza kwenye risala yao lipi wamelitekeleza na lipi hawajalitekeleza na wanahitaji msaada gani , kwani kila watakalolifanya Serikali na Chama kinawaona.
“ Nawahakikishia niko pamoja nanyi na nendeni kufanya kazi zenu kwa weledi ulio mkubwa,”alisisitiza.
Rais Samia alimpongeza Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Mama Maryam Mwinyi kwa kuwa mlezi wa matembezi ya Vijana sambamba na wale wote waliofanikisha matembezi hayo.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt.Sada Mkuya Salum alimuomba Mwnyekiti huyo popote pale penye mkopo nafuu achukuwe kwa ajili ya wananchi wa Tanzania na wataendelea kua na imani nay eye.
Alisema vijana wanapaswa kutambua kuwa mapinduzi ya sasa yana umuhimu mlkubwa katika kuleta maendeleo, kwani serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi zinazofanywa na matunda ya juhudi hizo yanaonekana.
Alifahamisha kuwa fedha zilizoletwa zanzibar Bilioni 230 zimeelekezwa katika miradi ya maendeleo, kwa lengo la kuwasaidia vijana katika suala zima la ajira, ikizingatiwa kauli mbiu ni Uchumu wa Buluu.
“Tanzania imedhamiria ifikapo 2035 itakuwa imeshafika katika uchumi wa kati, vijana ndio wahangaikaji wakubwa katika kuinua uchumi wa nchi,”alisema.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, aliwashukuru vijana wa kwa mikakati yao na juhudi za kuhakikisha wanasimama kidete kuona chama kinasonga mbele.
Alisema maamuzi ya vijana hao kufanya matembezi ya kuadhimisha miaka 58 ya Mapinduzi ni jambo jema na lakupongezwa, kwani wameamua kuadhimisha kwa vitendo maadhimisho hayo.
Akitoa taarifa ya Mtembezi ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Katibu Mkuu UVCCM Taifa Kenani Laban Kihongosi, alisema matembezi yanakumbusha mapinduzi yaliofanywa na viongozi hao, vijana wanakila sababu ya kukumbuka mapinduzi hayo.
Alisema vijana wanampongeza Mwenyekiti huyo kufuatia mabadiliko makubwa anayoendelea kuyafanya katika serikali yake, Vijana wanakila sababu ya kukubali mabadiliko hayo.
Akizungumzia suala ala ajira alisema katika kipindi kifupi kupitia uongozi wake, ajira nyingi zimeweza kutolea katika taasisi mbali mbali, kwa lengo la kuondosha tataizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.
Hata hivyo walimpongeza kwa hatua alizozichukua za kukuchukua Mkoapo wa Trilioni 1.3 na kuingiza katika miradi mbali mbali ya amendeleo vijijini na mjini, huku zanzibar wakipatiwa Bilioni 230.
“Sisi Vijana tunasema hatutokua na imani na mtu yoyote atakae kwenda kinyume na mkakati ya kuinua uchumi wa nchi ambapo serikali tayari imedhamiria mambo makubwa”alisema.
Jumla ya Vijana 700 wa UVCCM wameshiriki katika matemebzi hayo ya kuadhimisha miaka 58 ya Mapinduzi matukufu ya Zanizbar.
MWISHO