Monday, November 25

PPC yapongezwa kuhamasiaha Amani katika jamii

NA ABDI SULEIMAN.

WANANCHI wa Shehia ya Wawi Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, wameipongeza Jumuiya ya waandishi wa habari Pemba (PPC),kwa maamuzi yao ya kuelimisha jamii juu ya suala zima la utunzaji wa Amani iliyopo nchini.

Wamesema ni jumuiya chache zenye moyo wa kufanya jambo kubwa kama hilo, kupita katika shehia mbali mbali na kuhamasisha jamii juu ya suala zima la utunzaji wa amani.

Kauli hiyo imetolewa na sheha wa shehia hiyo, Sharifa Waziri Abdalla, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wazi juu ya kuelimisha jamii kuhusu masuala ya Amani, Umoja na Mshikamano, kupitia mradi wa SAUTI YANGU, AMANI YANGU, HATMA YANGU, naotekelezwa na PPC wakishirikiana na Foundation for civil society na Search for common groud, kwa ufadhili wa umoja wa nchi za ulaya.

Sheha sharifa alisema upo umuhimu mkubwa sana wa kutunza amani katika nchi, ili wananchi wake waendelea kubakia salama na sio kuiga mambo yanayotokea katika nji za jirani.

“Elimu hii ya uhamasishaji utunzaji wa amani ni jambo la muhimu, vizuri jambo hili kuliendelea hata katika shehia nyengine, ila shehia yangu bado elimu hii tunaitaka”alisema.

Mratib wa Mradi huo pia ni Katibu wa PPC Ali Mbarouk Omar, aliwataka wananchi kuachana na tafauti zao za kisiasa katika suala la utunzaji wa amani pamoja na maendeleo.

“Sisi tumekuja hapa kutoa ujumbe wetu na haya yote yaliyotolewa na wasanii yapo katika jamii zetu, shehia ni vizuri kuyatekeleza kwa vitendo,”alisema.

Alisema licha ya kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa haki mfano vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya ukaazi, huku akiwataka wananchi hao kufuata za upatikanaji wa haki hizo katika vyombo vinavyohusika.

Akiwasilisha umuhimu wa amani katika uislamu, Shekh Said Ahmad Mohamed, alisema amani imepewa nafasi kubwa kimali na kiafya, kila mtu ana dhima ya kutunza amani na kila muislamu anatakiwa kumpendelea muislamu mwenzake.

“ulinde ulimi wako na mkono wako kwa kuitunza amani, yoyote ataketokea kushawishi kurejesha ugomvi na uhasama uliokuwepo tunapaswa kumkataa kwa vitendo”,alisema.

Naye Dr.Amour Rashid kutoka PPC, aliwataka wananchi hao kuangalia mifano iliyotokea katika nchi nyingi duniani zinavyopata shida mpaka sasa, kukiwa hakuna linalofanyika lolote zaidi ya vita.

Naye Mwanaidi Khalfani Ali Mkaazi wa shehia ya Wawi, aliwataka vijana ambao hawajapata vitambulisho kutumia njia nzuri kwa kufika kwa shehia wa shehia kupewa fomu maalumu na sio kukaa vijiweni na kuanzisha malumbano.

Aliwaomba wananchi wa wawi kukaa na sheha wa shehia hiyo, katika kudumisha, pamoja na kuwaangalia vijana wa mtemani kuona nini cha kufanya na sio kubakia katika vikundi viovu.

Kwa upande wake Ali Abdalla Mohamed aliwataka wananchi wenzake wa Wawi kuhakikisha wanawafichua wafanyaji wa vitendo viovu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili waweze kurudi na kuwa watu wema.

MWISHO