Thursday, January 16

Profesa Mnyaa akabidhi Bati 150, mbao 450 kwa Ujenzi wa kituo cha Afya Tironi

NA ABDI SULEIMAN.

KUKAMILIKA kwa Ujenzi wa kituo cha Afya Tironi jimbo la Mkoani Wilaya ya Mkoani, kitaweza kuwapunguzia usumbufu wa kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani umbali wa kilomita 3.9.

Wananchi hulazimika kulipia kiasi ya shilingi 3000-2000 hadi 1500 kwa usafiri wa bodaboda, wakati wa kufuata huduma hiyo ya afya kutoka tironi hadi Hospitali ya Abdalla Mzee.

Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi, katika hafala ya kukabidhi Bati 150, mbao 450 zilizogharimu jumla ya shilingi Milioni 10 kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Mkoani Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, hafla iliyofanyika skuli ya Tironi Wilaya ya Mkoani.

Mmoja ya wananchi wa Kijiji hicho Rahma Kombo Mohamed, alisema suala la huduma ya afya kijijini kwao ni taatizo kubwa, kwani mtu anaposhikwa hata kama usiku hulazimaka kukimbilia hospitali ya Abdalla Mzee kwa ajili ya matibabu zaidi.

Alisema kukamilika kwa kituo hicho kitaweza kuwapunguzia shida waliokuwa wakiipata, hususana mama wajawazito, watoto kwenda kilinik, pamoja na kukodi gari kwenda kufuata huduma hiyo.
“Sasa hivi ndio afadhali kwa kua barabara hii imefanyiwa ukarabati, hapo nyuma ilikuwa shuhuli wakati mwengine unatamani upitie baharini kuliko adhabu ya barabarani,”alisema.

Naye Amour Ali Mohamed alisema ujio wa profesa katika jimbo la Mkoani, umeweza kubadilisha maisha ya wananchi wa kijiji cha Tironi, kwani msaada mkubwa ameweza kuwapatia ikiwemo barabara na kituo cha afya.

“hapo awali hali ilikua ngumu masafa marefu wananchi hutembea tena kwa miguu, kutoka hapa tironi hadi Mkoani spitali ila sasa tokea kuja yeye ameweza kututengezea barabara imekua afadhali”alisema.
Kwa upande wake Diwani wa Wadi ya Mkoani Abdalla Gairo, alisema kipindi cha mvua ilikuwa ni shida sana kupitika kwa barabara hiyo, zaidi pale unapouguliwa na mtoto na kumfikisha hospitali.

Mbunge wa Jimbo la Mkoani Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, alisema serikali imekua na mikakati na mipoango mizuri katika kuhakikisha inawaondoshea usumbufu wananchi katika suala la afya.

Alisema kukamilika kituo cha afya hicho kitaweza kutoa matibabu madogo madogo, matibabu makubwa watapelekwa katika hospitali ya Mkoani, hivyo kituo hicho kitaweza kutoa huduma kwa wananchi hata wa vijiji vya jirani.

“Lengo letu ni kuona kila mtu anapata matibabu bure kupitia vituo vyetu vya serikali, haya yote ni malengo ya chama cha mapinduzi katika kukuza sekta ya afya,”alisema.

Aidha mbunge huyo alikabidhi bati 150, mbao 450 zenye thamani ya shilingi Milioni 10, huku fundi wa kuezekea akilipwa shilingi laki nane na mbunge huyo na kumtaka fundi huyo ndani ya wiki moja awe ameshamaliza kazi hiyo.