Thursday, January 16

Skuli ya Ole Msingi yanyamazishwa kilio cha muda mrefu.

NA ABDI SULEIMAN.

BAADA ya kilio cha muda mrefu kwa wanafunzi, wazazi na walimu wa skuli ya Ole Msingi, hatia Mwakilishi wa Viti maalumu UWT wasomi Mkoa wa Kusini Pemba, Lela Mohamed Mussa amekabidhi matundu 12 ya vyoo vya Kisasa vyenye thamani ya shilingi Milioni 40,000,000/=.

Alisema vyoo hivyo licha ya kutokukidhi mahitaji ya wanafunzi wote, lakini kwa hatua ya kwanza vitaweza kuwaondoshea usumbufu wakufuata huduma hiyo majumbani, au baadhi ya wanafunzi kujisaidia msikitini na vichakani.

Mwakilishi huyo aliyaeleza hayo katika hafla ya kukabidhi vyoo hivyo, iliyofanyika skuli ya Ole Msingi na kuhudhuriwa na wanafunzi, walimu na viongozi wa kamati ya skuli.

“Sote ni Mashahidi wanafunzi, walimu na wazazi muda mrefu skuli yetu imekosa huduma hizo, wanafunzi wetu wakipata shida wakati wa kuhitaji kujisaidia, wakati mwengine mtu anakosa mpaka maoso, sasa lei tumekuja kutimiza ahadi yetu,”alisema.

Alisema nia ya Mapinduzi Mtukufu ya 1964 ni kuwasogezea wananchi huduma karibu yao, ikiwemo suala la elimu na huduma zake za kijamii.

Aidha Mwakilishi huyo pia ni Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, aliupongeza uongozi wa skuli hiyo kwa kupasisha wanafunzi wengi katika mitihani ya mwaka jana, yote hayo ni kurudisha ihsani kwa wanaosaidia skuli hiyo.

“Changamoto za Skuli ya Ole mimi sio wa kuombwa ni kuambiwa na kutekeleza, skuli hii mimi ni skuli yangu niliosoma lazima nisaidia kwa hali na mali,”alisema.

Hata hivyo aliwataka walimu, wanafunzi kuhakikisha wanavitunza vyoo hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu, pamoja na kuhakikisha wanadumisha usafi muda wote.

Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Ole Msingi Ali Mussa Ali, alisema kukabidhiwa kwa vyoo hivyo vitaweza kupunguza, kilio kikubwa kwa wanafunzi na walimu wa skuli hiyo na kuwafanya sasa kusoma bila ya hofu.

Alisema kwa sasa kilio kikubwa kwa skuli yake ni uhaba wa madarasa, hivyo aliwaomba viongozi wa jimbo hilo kuangalia ujenzi wa madarasa mapya ili kukidhi idadi ya wanafunzi waliopo skuli hapo.

“Skuli inawanafunzi 1849 na walimu 36, tuna matundu 12 itakuwa tundu moja kwa wanafunzi wasiopungua 168 na walimu 36 wamepata tundu moja, vitaweza kutusaidia japo kidogo tafauti na tulivyokua hatuna hata tundu mmoja”alisema.

Alisema mahitaji halisi ya vyoo ni kuwa na matundu yasiopungua 50 ambapo tundu moja litaweza kutumiwa na wanafunzi 36 hadi 37 kulingana na hali za kiafya.

Mwenyekiti wa kamati ya skuli ya Ole Hamad Omar Mohamed, alisema changamoto zipo nyingi, ikiwemo bado wahitaji vyoo zaidi kulingana na wanafunzi.

Naye Mjumbe wa kamati ya skuli Mwalimu Sultani Nssor Hamad, alisema baada ya kuona idadi ya wanafunzi imekua kubwa, wamelazimika kuchangishana ili kupata fedha za kujenga banda moja lenye vyumba vinne.

Alisema kwa sasa jumla ya shilingi Milioni 1,231,000/= zimepatikana kupitia michango ya wanajamii, walimu, wafanyakazi wanaoishi ole kuchangia kila mmoja elfu 10.

Nao wazazi wamempongeza mwakilishi huyo kwa moyo wake wa kusaidia huduma za elimu, kwani wanafunzi walikuwa wakidhalilika wakati wanapohitaji kujisaidia.

Kwa mujibu wa W.H.O tundu moja la vyoo linapaswa kutumiwa na wanafunzi 15 walioko bodingi na wanafuzi 25 kwa wasio kaa bodingi.